Blogger Widgets
Showing posts with label news. Show all posts
Showing posts with label news. Show all posts

Friday, 24 April 2015

Ajali nyingine ya basi yaua 10 Shinyanga


Jinamizi la ajali za barabarani zikihusisha mabasi zimeendelea kugharimu maisha ya Watanzania baada ya jana watu 10 kupoteza maisha na wengine 50 kujeruhiwa vibaya wakati basi la Unique Express lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Tabora kugongana uso kwa uso na lori la Coca-Cola lililokuwa likitokea Tinde kuelekea Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 8.45 mchana katika Kijiji cha Ibingo, Kata ya Samuye, Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi uliosababisha dereva wake kushindwa kulikwepa lori hilo lililokuwa katikati ya barabara.
Alisema watu tisa walifariki dunia papohapo na mmoja alifia katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga akipatiwa matibabu.
Kamanda Kamugisha alisema dereva wa lori anashikiliwa na polisi mwenzake wa basi hali yake ni mbaya na amelazwa hospitali.
Alisema wengi waliofariki dunia walikuwa wamekandamizwa na vyuma hali iliyowalazimu kuomba msaada wa winchi kuliinua basi hilo na kuwatoa.
Kamanda Kamugisha aliwataka wananchi na abiria kutoa taarifa pindi wanapoona madereva wakiendesha mwendo ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwamo Diwani wa Kata ya Samuye, Amos Shija walisema walishtushwa na kishindo cha kugongana kilichofuatiwa na kelele na vilio vya abiria.
Shuhuda, John Bundala aliitaka Serikali kuendelea kuwachukulia hatua kali madereva ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani na kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia na wengine kupata ulemavu.

ACT yavuna wanachama wapya 6,000

Chama cha ACT-Wazalendo kimehitimisha ziara katika mikoa 10 nchini huku kikijigamba kuingiza wanachama wapya zaidi ya 6,000.
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema jana kuwa ziara hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa.
“Leo tumetimiza kilomita 5,802 katika kituo chetu cha mwisho cha Maswa, Mkoa wa Simiyu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Tumepata wanachama 6,391, katika mikoa mbalimbali na wote wameandikishwa na namba zao za simu zimeingizwa kwenye database (mfumo maalumu wa kutunza kumbukumbu).
“Mkoa ambao umeongoza kwa wanachama kuchukua kadi uwanjani ni Tabora, tuwalipata 815, lakini Makambako walikuwa 104.”
Zitto ambaye aliacha uanachama na ubunge wake katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwishoni mwa mwezi uliopita, kwenye ziara hizo alionekana kivutio na mwenye ushawishi kwa wananchi kutokana na mapokezi aliyopata.
Alisema akiwa Simiyu mijadala waliyozungumza na wananchi katika ziara hizo ni kuhusu mkoa huo kuwa wa mwisho kwenye elimu.
Zitto alisema ni asilimia 3.7 tu ya watu wenye miaka 25 mkoani humo, wana elimu ya sekondari na kuendelea.
Pia alisema walizungumza kuporomoka kwa pamba kwa asilimia 47 baada ya wananchi kususia sera za Serikali ya CCM kuhusu zao hilo.
“Hiyo inatokana na bei ya Sh600 kwa kilo moja anayopewa mkulima wakati katika soko la dunia imefika Dola 1.2 za Marekani,” alisema Zitto ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Pamba ilishuka kwa kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia 32 mwaka 2013 na 2014 imeporomoka kabisa.
Ziara ya chama hicho iliyodumu kwa wiki mbili, ilianzia Ruvuma na kuendelea katika mikoa ya Njombe, Iringa, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mara na Mwanza.
Chama hicho kilikuwa kinajitangaza kwa mara ya kwanza katika mikoa inayodaiwa kuwa ngome ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

MAKAMBA: SINA UTANI KWENYE URAIS

Mbunge wa Bumbuli (CCM) na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema haweki utani katika suala la kugombea urais na akikosa kiti hicho kipindi hiki itakuwa vigumu kukipata miaka ijayo.
Makamba alisema hayo, hivi karibuni jijini hapa, kuwa kauli zinazotolewa na watu, ikiwemo ile ya yeye kutumiwa kutangaza nia ili baadaye aje kumuunga mkono mgombea mwingine wa urais kwa tiketi ya chama hicho, inamkera na ‘kumnyima usingizi’.
“Urais nautaka sasa na si kipindi kingine chochote, na niseme tu wazi kwamba, hizi kauli kuwa natumiwa na watu zinaniumiza sana. Naamini kuwa ninaweza. Kama atakayepewa sasa (urais) ataharibu, ni vigumu sana kugombea tena urais na kuupata,” alisema Makamba ambaye amewahi kuwa mwandishi wa hotuba za Rais Jakaya Kikwete.
Kauli hiyo ya Makamba aliyetangaza nia ya kuwania urais mwaka jana akiwa London, Uingereza imelenga kuwajibu wanaodhani kuwa anatumika kutibua harakati za vigogo wa chama hicho wanaoutaka urais.
Julai 9, mwaka jana Rais Kikwete alizungumzia nia ya Makamba kutaka kuwania urais, akisema mwanasiasa huyo kijana “anataka mambo makubwa, lakini hajamshirikisha”, na kwamba “asilazimishe” kwa kuwa wakati ukifika atapata kile anachokitaka.
“Nasikia kuwa bwana mdogo January anataka mambo makubwa. Mie hajaniambia, na mie nasikia. Hata alipogombea ubunge hakuniambia nilisikia baadaye... asilazimishe, wakati ukifika atapata, na akikosa asilete nongwa,” alisema Kikwete.
Rais Kikwete alitolea mfano wake aliposhindwa katika uteuzi wa mgombea urais wa CCM mwaka 1995, wakati akiwa na miaka 45 (miaka minne zaidi ya umri wa Makamba), akisema kuwa hakukata tamaa na aliendelea kusikiliza ushauri wa wazee hadi alipofanikiwa kukalia nafasi hiyo ya juu mwaka 2005.
Kauli hiyo ilikuwa ya kwanza kutolewa na Rais Kikwete kuhusu wanachama wa CCM wanaotaka kuwania urais, baada ya chama hicho kuwaonya makada sita kwa tuhuma za kuanza mapema kampeni za kutaka nafasi hiyo kubwa.
Akifafanua zaidi nia yake hiyo, Makamba ambaye ni mtoto wa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yussuf Makamba alisema, “Wapo wanaosema kuwa ninautaka urais kwa sababu ninatumiwa na watu. Wapo pia wanaosema kuwa ninautaka urais kwa ajili ya kujitangaza ili niweze kupata nafasi nyingine za uongozi.”
Aliongeza: “Wanasema kuwa ninautaka urais sasa kwa ajili ya kujiwekea mazingira mazuri ya kugombea (urais) mwaka 2025. Unajua kama CCM ikiweka mgombea ambaye si mzuri, mwaka 2025 utakuwa mgumu sana.”
Makamba alisema anaamini kuwa yeye ni miongoni mwa makada wasafi wa chama hicho tawala.
“Kuhusu suala la maadili sina shaka kabisa. Moja ya changamoto kubwa iliyopo nchini kwa sasa ni mmomonyoko wa maadili. Wapo viongozi wengi wanaoomba nafasi ya urais huku kukiwa na mashaka makubwa kuhusu uadilifu wao,” alisema.Alisema wapo viongozi wanaotumia pesa nyingi kutafuta nafasi hiyo kwa kuzigawa nchi nzima ila anaaamni viongozi hao hawawezi kuleta mabadiliko yoyote katika nchi hii yakiwamo ya kupambana na rushwa ambayo ni kansa inayoirudisha nyuma na kuitafuna nchi.

Sunday, 2 February 2014

Dk Ramphele: Mwanamke anayetaka urais Afrika Kusini


Aliwahi kuzipamba kurasa za Jarida la Forbes mwaka 2011 akiwa ni miongoni mwa wanawake tisa wa kiafrika wanaoongoza kwa utajiri.  Siyo hivyo tu, bali ana cheo kikubwa akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji, wa Benki ya Dunia(WB).
Ni Dk Mamphela Ramphele,  mwenye umri wa miaka 66  ambaye hivi karibuni alitangaza kuwania nafasi ya urais nchini humo, kwenye uchaguzi ambao utafanyika miezi minne ijayo nchini Africa Kusini.
Ramphele amedhamiria kuwa mwanamke wa kwanza nchini humo kuwania urais na pia  kuutaja utajiri wake ambao ni  randi 55 milioni (Dola za Marekani 5.5milioni).
 Uchaguzi wa Rais na wabunge ambao unatarajiwa kufanyika Aprili au Mei mwaka huu, ni wa kwanza baada ya kifo cha Rais mstaafu Nelson Mandela.
Ramphele,  ambaye ni mwanasiasa mkongwe, mhadhiri na mhudumu wa afya,  mwenye mafanikio makubwa  na Mkurugenzi wa sekta nyeti ya uchimbaji wa madini, alikaririwa akisema  maamuzi yaliyofanywa na chama chake ya kumchagua kuwa mgombea wa urais ni yenye tija kwa Waafrika wa Kusini.
“Nimefarijika na kukubali mwaliko huu wa chama cha Democratic Alliance,(DA)  kuwa mgombea wa urais kwa mwaka 2014,” alisema Dk Ramphele.
Ramphele alizaliwa jimbo la Bochum, Kaskazini mwa Transvaal,(hivi sasa Limpopo). Alimaliza elimu ya sekondari, Setotolwane, mwaka 1966 na akajiunga na kozi fupi ya tiba kwenye chuo kikuu cha Kaskazini.
Mama yake, Rangoato Rahab, na baba yake Pitsi Eliphaz Ramphele walikuwa walimu wa shule ya msingi. Mwaka 1944 baba yake alipandishwa cheo na kuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Stephanus Hofmeyer.
Akiwa Chuo Kikuu, Ramphele alianza kuvutiwa na siasa za wanafunzi na ubaguzi wa rangi na hapo alikuwa mwanzilishi wa Chama cha Watu Weusi(BCM). Muungano huo wa wanafunzi kupinga ubaguzi wa rangi ulikuwa chanzo cha kukutana na Steve Biko, miongoni mwa wanasiasa wakongwe wa Afrika Kusini. Urafiki kati ya Ramphele na Biko, ulikua na kuzua mapenzi ambayo yaliwapa zawadi ya watoto wawili, Lerato Biko, (aliyezaliwa mwaka 1974) na Hlumelo Biko(1978). Hata hivyo, Lerato alifariki baada ya kuugua nimonia.
 Safari yake kisiasa
Mwaka 1955

Upanuzi wa Bandari bado kizungumkuti

 
Upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam, uliosababisha kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu, umeendelea kupata vikwazo baada ya kampuni ya Kichina iliyopewa zabuni ya upanuzi huo kutofika kwa kazi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari(TPA), Madeni Kipande aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC), iliyofanya ziara jana katika bandari hiyo kuwa hatua  hiyo licha ya kuwasikitisha imesababisha kuchelewa kwa upanuzi huo.
“Hiyo kampuni ya kichina ilitakiwa iwe imeanza kazi tangu Oktoba mwaka jana,  lakini ajabu ni kwamba ipo kimya na hakuna mawasiliano ya aina yoyote. Tumeamua kufuta zabuni hiyo, tutatangaza nyingine mapema mwezi huu kwa kuwa tunakusudia kwamba, Julai tuwe tumeshaanza kazi. Hapa hatutaki siasa zimetuchosha,” alisema Kipande.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto aliisisitiza TPA kuhakikisha kwamba zabuni hiyo inatangazwa na kukamilika mapema akieleza kuwa kuendelea kuchelewesha kuanza kwa upanuzi huo ni kuikosesha mapato Serikali.
“ Upanuzi huo ni muhimu sana kufanyika kwa sababu ukikamilika ndiyo unaoweza kuweka ushindani na Bandari ya Mombasa, pia itasaidia kuiongezea mapato Serikali,” alisema Zitto.
Kamati hiyo pia ilisisitiza TPA kuhakikisha inaanza matumizi ya kupakua mafuta kwa njia ya mita kwa sababu utaratibu wa kupima kwa kijiti(Dip Stick) unaikosesha mapato Serikali.
“ Katika hili tumeamua kuunda kamati maalumu, itakayofuatilia kwa kina kubaini kwa nini tangu utaratibu huo ulipopaswa kuanza kutumika mwaka 2008 umekuwa ukipigwa danadana. Tunahisi kuna jambo, inawezekana hata ni hujuma za wafanyabiashara wa mafuta, tutaujua ukweli,” alisema Zitto.
Akiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Shukuru Kawambwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari, walitafuta mkopo kutoka Serikali ya China kupitia Benki ya Exim ya nchi hiyo iliyoridhia kutoa Dola 524 za Marekani ili zisaidie upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wafaransa wawili wauawa Zanzibar

 
 Kisima kilichopo eneo la Matamwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambamo raia wawili wa Ufaransa wanasadikiwa kuuawa na kisha kufukiwa kwa zege.

Raia wawili wa Ufaransa wameuawa na kutumbukizwa katika kisima cha maji kilichomo ndani ya uwanja wa nyumba yao na watu wasiojulikana katika eneo la Shehia ya Matemwe Kaskazini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Zanzibar (DCI), Yussuf Ilembo zinaeleza kuwa watu hao mtu na mkewe waliuawa hivi karibuni.
DCI Ilembo aliliambia gazeti hili jana kuwa tayari vikosi vya Zimamoto na Uokozi (KZU) na Polisi vimeanza kufukua kisima hicho na kwamba katika hatua ya awali wamefanikiwa kukuta mfupa wa mguu wa kushoto wa mmoja wa watu hao.
Aliwataja wazungu hao kutoka Ufaransa kuwa ni Francois Cherer Robert Daniel na Brigette Mary ambao walikuwa wakiishi kama mtu na mkewe wakiwa na mbwa wao anayeitwa Allan ambaye pia amekutwa amekufa ndani ya nyumba hiyo.
Alisema uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa Wafaransa hao waliingia nchini kihalali mwaka 2013, na kununua nyumba kwenye ufukwe wa mwambao wa Bahari ya Hindi eneo la Matemwe na kuanza kuishi eneo hilo.
DCI Ilembo alisema polisi tayari wanawashikilia watu watatu wakazi wa Shangani katika Mjimkongwe wa Zanzibar na mmoja anayeishi katika eneo la Kilimani katika wilaya ya Mjini Unguja.
“Kuna

Wednesday, 29 January 2014

Lowassa ameanza safari, ni ndefu kiasi gani?


“Nimefarijika sana leo kuwaona hapa marafiki zangu wengi. Ninapowatazama hadi machozi yananitoka na kwa uwezo wa Mungu tutashinda kwani nyote mnajua nia na ndoto yangu…WanaCCM msiwe na shaka, tutavuka kwa nguvu zetu... Wingi wenu huu unanipa faraja katika safari yetu na kwa kumtegemea Mungu tutashinda.”  ni kauli ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
Lowassa alitangaza hivi karibuni kuanza rasmi kwa safari hiyo aliyoiita ya matumaini ya ndoto zake, ambayo anasema itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure, majisafi na maendeleo ya uhakika.
Alitoa kauli hiyo katika ibada ya shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT),Usharika ya Monduli Mjini mkoani Arusha.
Bila ya kutaja safari hiyo ni ipi, Lowassa anawataka waliohudhuria ibada hiyo waungane na kaulimbiu yake, ‘Tulifurahi pamoja, tulihuzunika pamoja na tutashinda pamoja’.
Hafla hiyo ya kimkakati, ilihudhuriwa  na baadhi ya wabunge, wengi wakiwa wa CCM, wenyeviti wa mikoa kadhaa wa chama hicho, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wenyeviti wa CCM, viongozi wa jumuiya za chama na wengineo.
Licha ya kutoweka bayana aina ya safari anayoanza, Lowassa ni miongoni mwa wanaCCM wanaotajwa kuwa wanaowania urais, kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Dalili hizi za Lowassa kuutaka urais na kutafuta kabla ya kipenga kupulizwa, zimeishtua CCM na kumtahadharisha kuwa atapoteza sifa ya kupitishwa ifikapo 2015.
Safari tangu 1995

Westgate: Maswali kwa Rais Uhuru Kenyatta

 
Wakenya wangali wanasubiri tume aliyoahidi Rais Uhuru Kenyatta  baada ya tukio la kigaidi katika jengo la Westgate hasa baada ya uamuzi wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama, ambayo ilisema Serikali ya Kenya ilionywa takriban siku 19 kabla ya uvamizi huo lakini haikuchukua hatua yoyote.
Jeshi la Polisi pia lilielekezewa kidole cha lawama na kamati hiyo kwa kukosa ushirikiano na kikosi cha JeshiUlinzi wakati wa uokoaji na kusababisha maisha ya watu wengi kuangamizwa.
Kuhusu uchunguzi huu, familia za walioathiriwa wakati wa uvamizi huo wa Septemba 21, mwaka jana wanaweza kuamua kwenda mahakamani kuishtaka Serikali kwa kukosa kuchukua hatua kuzuia vifo na majeruhi.
Watu 67 walifariki dunia katika tukio hilo la waasi wa Al-Shabaab waliovamia Jengo la Westgate ambalo lilikuwa na maduka na hoteli za kifahari.
Uchunguzi wa wabunge ulionyesha kwamba, Kikosi cha Jeshi la General Service Unit (GSU) kilikuwa kimefanikiwa kuwapata wavamizi ndani ya jengo hilo, lakini kilichofanya wasiwaue ni hatua ya kikosi  cha Jeshi la Kenya Defence Force (KDF) kuwasili na kuwatimua (GSU) kabla ya kufanikiwa kuwavamia waasi hao.
Mwaka mmoja kabla ya uvamizi huo, Idara ya Upelelezi na Jinai iligundua kwamba waasi wa Al-Shabaab walikuwa wanapanga kuvamia Westgate. Walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Onyo jingine lilitolewa kati ya Agosti 6 na Septemba 2, 2013. Inasikitisha kuwa, licha ya kupewa habari hizo, Serikali iliendelea kulala na kuwapa nafasi waasi kupanga na kuvamia bila wasiwasi wowote.
Vikosi vyote vya usalama havina budi kuwajibika wakati wote na kuweka mpaka kati ubinafsi, ufisadi na kuzembea kazini ili waweze kuwatumikia na kuwalinda Wakenya. Kwa kufanya hivi tutaepukana na hali iliyotokea, ambapo watu wanapoteza maisha na wengine kujeruhiwa.
Wataalamu waliohojiwa na kamati hiyo walisema KDF hawangefaa kutumwa kuokoa watu kwenye jengo hilo kwa sababu kitengo maalumu cha GSU tayari kilikuwa kimetumwa Westgate na walikuwa wanafanya kazi nzuri ya kuwanasa au kuwaua waasi.
Maswali ya kuuliza
Kwa nini hakuna hatua iliyochukuliwa na polisi baada ya Idara ya Upelelezi kutoa habari kuhusu uvamizi huo?
Kwa nini vikosi mbalimbali vya jeshi na polisi vilikosa kutimiza majukumu yao? Je, kulikuwa na kutoelewana kati ya vikosi hivi ama kila mmoja alikuwa anahisi kwamba ni bora kuliko mwingine?
Je, kwa nini KDF ilipowasili Westgate ilianza kuwatumia GSU ilhali walikuwa kwenye harakati za kumnasa na kumwangamiza adui?
Bunge litafunguliwa mwezi ujao na ripoti hii bila shaka litazua hisia mbalimbali itakapoanza kujadiliwa na wabunge.
Wabunge wanasema kwa vikosi vya usalama kukosa kuchukua hatua ya kuzuia uvamizi, waasi waliweza kufanya uvamizi kama ule uliofanywa Mumbai, India miaka michache iliyopita.
Kuna habari kwamba ingawa wavamizi wanne walitambuliwa, idadi kamili ya waasi waliotekeleza unyama huo haijulikani. Inasadikika kwamba walikuwa 15.
Kamati hiyo ya Bunge inasema waasi walionaswa na kamera za usalama ni Abu Baraal, Al Sudani, Omar Naban na Khatab Al Kene. Inaaminika kwamba wavamizi hao wote walifariki kwenye uvamizi huo.
Mawasiliano
Wabunge walisema kwamba mipango ya uokoaji ilisambaratishwa tangu mwanzo wake. Waliongeza kwamba mawasiliano kati ya kituo cha kutoa habari kuhusu mambo yaliyokuwa yanaendelea katika Westgate na idara za Serikali zinazohusika na usalama yalikuwa na  dosari.
Wakati huo baadhi ya habari ilikuwa kwamba, wavamizi wengine walifanikiwa kutoroka kupitia kwa bomba la majitaka, huku wengine wakisema wote waliuawa.
Hii ni kizungumkuti. Na swali ni je; wavamizi walitoroka au waliuliwa. Je, mwanamke aliyejulikana kama “The White Widow” alikuwa mmoja wa wavamizi au ulikuwa uvumi mwingine wa vikosi vya usalama?
Awali, Mkuu wa KDF, Jenerali Joseph Karangi alitangaza kwamba licha ya tuhuma za wizi dhidi ya KDF, kikosi hicho hakikuiba chochote kutoka Westgate. Karangi alipoulizwa kwa nini KDF walinaswa wakibeba mifugo ya plastiki iliyokuwa imejaa pomoni, alisema hayo yalikuwa maji.
Alisema jeshi lilichukua maji kutoka katika duka la jumla la Nakumatt kwa sababu walikuwa wanahisi kiu. Lakini kamati hiyo imeikuta KDF na kosa la kuiba bidhaa na pengine na pesa wakati wa shughuli za uokoaji uliochukua siku nne.
KDF ikipatikana na kosa la kuiba, wafanyabiashara wengi waliopoteza bidhaa na pesa zao wanaweza kwenda kortini wakitaka kulipwa na serikali.

Ripoti hii haitaji watu binafsi waliohusika na kuzembea kazini na kupelekea wavamizi kutekeleza unyama wao Septemba 21 mwaka jana.
Si vikosi vya usalama tu ambavyo vimepatikana na kosa la kutotimiza wajibu wao inavyotakikana. Wizara ya Uhamiaji ilipatikana na maswali ya kujibu kuhusu ni vipi wageni waliingia nchini na kupata vibali vya kukaa Kenya na kutekeleza uvamizi huo mbaya zaidi tangu ule wa 1998 ambao Ubalozi wa Amerika ulivamia na watu zaidi ya 200 kupoteza maisha.
Wizara hii, kwa muda mrefu imekuwa ikituhumiwa kwa kutoa vibali kama vile pasipoti na vitambulisho kwa wageni baada ya kupewa hongo. Wengi wa wanaopewa vibali na stakabadhi za kuishi Kenya wamegunduliwa kuwa ni waasi au washiriki wao.
Mwaka jana, akizungumza na vyombo vya habari vya Ufaransa, Mkuu wa Sheria, Profesa Githu Muigai alisema Rais angeunda jopo la kuchunguza Westgate punde tu baada ya Kamati za Bunge kumaliza uchunguzi wake.
Ripoti ya kamati
Ripoti ya Kamati imejumuisha uchunguzi wa kitaalamu uliofanywa na mashirika mbalimbali ya kigeni, likiwamo Shirika la Kijasusi la Marekani (FBI).
Kulingana na  taarifa hiyo ya kitaalamu, ni wavamizi wanne tu waliohusika kwenye uvamizi wa Westgate na wote waliuawa. Taarifa hiyo inaongeza kwamba baadhi ya miili iliyopatikana kwenye vifusi vya Westgate ilikuwa ya waasi hao.
Iliongeza kwamba, silaha zilizopatikana kwenye jengo hilo zilikuwa za waasi.
Ripoti hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa ili uwezekano wa nchi kuvamiwa tena upunguzwe; Serikali ya Kenya itangaze vita dhidi ya Al-Shabaab ndani na nje ya Kenya na pia kituo cha kuwezesha vikosi vyote vya usalama kupokea habari za kiusalama kibuniwe haraka iwezekanavyo.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kwamba, Wizara ya Uhamiaji ifanyiwe mabadiliko ili wafanyakazi wenye ujuzi wa usalama waweze kuajiriwa.
Pengine pendekezo litakalozua utata ya kitaifa na kimataifa ni lile linalotaka kambi zote za wakimbizi zifungwe na wote warejeshwe makwao ili usalama wa Wakenya upewe kipaumbele.
Kwa hamu Wakenya wanasubiri Rais wao awaambie ni lini ukweli kuhusu uvamizi huu utajulikana baada ya kubuniwa kwa jopo la kutafuta ukweli kuhusu tukio hilo lililobadilisha historia ya Kenya.

Godoro, miti ilivyowaokoa na kifo kwenye mafuriko


Watoto wadogo walibebwa au kusimama kwenye mabega ya watu wazima, huku chumba kikiwa kimejaa maji. Hii ni hali ambayo ilitokea katika mafuriko ya hivi karibuni yaliyotokea Kilosa, mkoani Morogoro.
Hali ya mambo
Ilikuwa siku yenye mateso makubwa na uchungu wa kupotelewa na mali mbalimbali kwa wananchi wa Kijiji cha Magole, ambao walizingirwa na mafuriko.
Kila mtu alikuwa na aina yake ya kujiokoa; wapo niliowaona wakiwa juu ya miti  ilimradi tu ni namna gani ya kutafuta njia ya kujinusuru na kifo.
 Mwalimu wa Shule ya Msingi Magole Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro, Marthin Kongera (42) anaeleza mkasa mzima uliyoikumba familia yake pamoja na yeye mwenyewe na majirani waliokimbilia katika nyumba yake iliyojengwa na matofali ya saruji yenye vyumba viwili na ukumbi mmoja ili kuweza kujihifadhi na mafuriko yaliyoikumba tarafa ya Magole Januari 22 mwaka huu saa 12 asubuhi.
 
Akizungumza na mwandishi wa makala haya katika nyumba za Shule ya Msingi Magole, Kongera anasema kuwa ilikuwa siku ya Jumanne, yeye na familia yake waliamka salama saa 12 asubuhi,  baada ya muda mfupi akijiandaa kwenda kazini (shule mita 40 tu kutoka nyumbani kwake). Alianza kuona maji yakitiririka huku yakiwa yamesomba uchafu na kadiri muda ulivyozidi kusogea mbele maji yaliendelea kufika eneo la shule na kuanza kusambaa sehemu kubwa.
Maji hayo yalielekea kwa kusambaa kwa kasi katika mitaa ya kijiji hicho.
“Ni miujiza ya
KWA HABARI ZAIDI

Mauaji yazidi kutikisa Tarime


Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.
Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa matibabu.
Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.
“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,” alisema Nega.
Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray
Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.
Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma
Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo lisilofahamika.
Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58) na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.
Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi na usalama na kuwasaka wahalifu.
Wananchi wacharuka

Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze kumsaka jambazi huyo.
‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema mwananchi mmoja.

Ikulu yavunja ukimya kuhusu 'mawaziri mizigo'

 
Ikulu imetaka kufungwa kwa mjadala wa kuhusu kurudishwa kwa mawaziri wanaodaiwa kuwa ni mizigo kwenye Baraza la Mawaziri na badala imetaka waachwe wafanye kazi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu alisema kuendeleza mjadala huo ni kupoteza muda, kwani Rais Jakaya Kikwete alishamaliza kazi yake.
Rweyemamu alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya kuteua mawaziri ambao wana wajibu wa kumsaidia katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo si sahihi wateule hao kuitwa ‘mizigo’ kwani yeye (Rais) ameona wanafaa.
“Rais anapoteua watu anaangalia wanaofaa kumsaidia na si vinginevyo. Kwani lengo lake ni kuona nchi ina `move forward’ (inasonga mbele) kimaendeleo,” alisema Rweyemamu. Alisema watu wanapaswa kukumbuka kuwa mtu anapoteuliwa kwenye uwaziri kuna suala la uwajibikaji: “Anatakiwa kutekeleza uwajibikaji wa pamoja. Sasa kumshambulia mtu binafsi na kumwita mzigo siyo sahihi.”
Rweyemamu alisema mjadala huo kwa sasa umepitwa na wakati na kuwataka wananchi na wachambuzi kuwaacha mawaziri hao kuchapa kazi.
“Ni vizuri wananchi wakawapa nafasi mawaziri hawa ya kufanya kazi na baadaye kuwapima na kuwachambua kutokana na utendaji wao,” alisema.
Chimbuko la majadala
Mjadala kuhusu suala hilo unatokana na Rais Kikwete kuwarejesha katika Baraza la Mawaziri baadhi ya mawaziri ambao walidaiwa kuwa ni mizigo kutokana na udhaifu katika utendaji wao.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na Katibu wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ndiyo walioasisi mawaziri hao kuwa ni ‘mizigo’ walipokuwa na ziara ya kikazi mkoani Ruvuma, mwishoni mwa mwaka jana.
Mawaziri waliolalamikiwa kutokana na utendaji wao ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo, Waziri wa zamani wa Fedha, marehemu Dk William Mgimwa na aliyekuwa Naibu wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima.
Baadaye baadhi ya wabunge nao walikoleza moto kwa kushinikiza mawaziri hao wang’oke, huku wakiongeza idadi yao kwa kuwataja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa katika kundi hilo.
Mawaziri hao waliitwa kujieleza mbele ya Kamati Kuu ya CCM kuhusu sababu za utendaji wao kuwa wenye matatizo.
Hata hivyo, kabla ya Rais Kikwete kuchukua hatua, alitengua uteuzi wa Mawaziri wanne, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii na Dk Mathayo kutokana na mjadala mkali bungeni kuhusu jinsi Serikali ilivyotekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kadhalika, Dk Mgimwa aliyefariki dunia Januari 5, mwaka huu alisababisha pengo la mawaziri kufikia watano.
Wakati Rais Kikwete alipofanya mabadiliko katika Baraza lake Januari 19, mwaka huu, karibu mawaziri wote waliolalamikiwa walirejeshwa.
Hali hiyo ilizusha mjadala mkali kutoka kwa watu na makundi mbalimbali, huku CCM kupitia kwa Nape Nnauye kilisema kitaendelea kupiga kulele pale utendaji wa mawaziri hao utakapokuwa mbovu.

Jaribio la kumuua waziri Libya latibuka

 
Kumekuwa na jaribio lililotibuka la kumuua kaimu waziri wa ndani nchini Libya Al-Sidik Abdel-Karim.
Shirika la kitaifa la habari LANA na lile la AFP yamethibitisha tukio. Inaarifiwa kwamba gari alimokuwa Abdel Karim lilipigwa risasi alipokuwa akielekea katika mkutano katika makao makuu ya bunge.
Abdel-Karim anatarajiwa kuhutubia waandishi habari hivi punde.
Abdel Karim aliteuliwa na waziri mkuu nchini Libya kuwa kaimu waziri wa ndani baada ya waziri Mohamed Sheikh kujiuzulu mnamo Agosti mwaka jana.
Seddik Abdelkarim, alikuwa katika gari lake aliposhambuliwa na watu wasiojulikana waliomfyatulia risasi. Inaarifiwa hakuna aliyeuawa kwenye shambulizi hilo.
Libya imekuwa ikikabiliwa na hali ngumu ya kisiasa tangu waasi kuipindua serikali na kumuua aliyekuwa Rais Muamer Kadhafi mwaka 2011.
Waziri huyo alikuwa njiani kuelekea bungeni wakati gari lake liliposhambuliwa.
Shambulizi lenyewe limetokea chini ya wiki tatu baada ya mauaji ya naibu waziri wa viwanda Hassan al-Droui, aliyeuawa mjini Sirte

Sunday, 26 January 2014

Mchungaji Mtikila kufungua kesi kupinga Katiba Mpya


Mwenyekiti wa Chama cha Demokratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila anatarajia kufungua kesi Mahakama Kuu ya Tanzania kupinga kuendelea kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba Mpya.
Mchungaji Mtikila akizungumza na gazeti hili alisema, madhumuni ya kufungua kesi hiyo ni mchakato huo kukiuka hatua mbalimbali muhimu wakati wa kuiandaa ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi kipi wanatakiwa kukifanya kabla ya kutoa maoni.
“Nakwenda kufungua kesi hiyo, kutaka mchakato huu unaoendelea ufutwe na utupiliwe mbali, tunataka mchakato unaowashirikisha Watanzania wote, walio katika vyama vya siasa,makundi mbalimbali ya kiraia na madhehebu ya dini na wasio na makundi wala madhehebu,” alisema Mtikila
Aliongeza “Nilikuwa kimya najipanga, najua nitashinda sijajua Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataniletea mawakili wangapi lakini nitampangua mmoja baada ya mwingine.” Mchungaji Mtikila alisema, endapo majaji wa mahakama hizo watakaoisimamia kesi hawatatenda haki kutokana na matakwa ya Serikali ya CCM atakata rufaa.

Askari Magereza wadaiwa kuua mfungwa


Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Omary Mtiga
Askari Magereza wanane, wamefikishwa mahakamani wilayani Mafia mkoani Pwani kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa.
Mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Wilaya ya Mafia, Hassan Makube, ilidaiwa kuwa, Desemba 19 mwaka jana, askari hao walimuua Basiri Makungu aliyekuwa akitumikia kifungo katika Gereza la Kilombero, lililopo kwenye wilaya hiyo. Askari waliofikishwa mahakamani hapo walitajwa kuwa ni Sajenti Sadick na wenzake ambao walifunguliwa kesi namba 1/2014.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua Makungu, baada ya kumshambulia kwa kipigo mwishoni mwa mwaka jana.
Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu, pamoja na kesi ya mauaji kutokuwa na dhamana, watuhumiwa hao walirudishwa rumande hadi Februari 7 mwaka huu.
Akizungumzia tukio hilo, ofisa wa juu wa Jeshi la Magereza, Menrad Tesha alisema kuwa, jeshi hilo linafahamu taarifa za askari hao kushtakiwa kwa makosa hayo, lakini akasema suala hilo halipo chini yao. Tesha alipohojiwa kuhusu mustakabali wa ajira za askari hao na iwapo wanashtakiwa kama raia au wafungwa alisema hawezi kulizungumzia hilo kwa sasa.
“Siwezi kuzungumzia ajira zao hapa, huu siyo utendaji unaotakiwa, kila kitu kina taratibu zake, hivyo siwezi kulizungumzia hilo,” alisema Tesha.
Alieleza kuwa askari anapotuhumiwa kwa makosa yoyote suala lake huachwa mikononi mwa vyombo vinavyostahili, ili kuwachukulia hatua.
“Hivi sasa wale ni watuhumiwa, kwa hiyo mimi kuliongelea siyo sahihi. Kama kuna kitu ungetaka kufahamu, basi nakushauri mfuate mkuu wa gereza kule walipo sasa (Mafia), atakueleza kila unachotaka kufahamu kuhusu askari hao kwani bado wapo huko,” alisema Tesha.
Matukio ya Askari Magereza kuua wafungwa
Februari mwaka jana ilidaiwa kuwa Willfred Mallya mwenye namba 315 aliyefungwa mwaka 2003 katika katika Gereza la Kisongo mjini Arusha aliuawa kutokana na kipigo cha Askari Magereza.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Omary Mtiga licha ya kukiri kutokea kwa kifo cha mfungwa huyo, alikanusha kuwa kilitokana na kipigo cha askari hao akisema kifo chake kilikuwa ni cha kawaida.
Desemba mwaka 2010, askari wanne wa jeshi hilo waliokuwa wakifanya kazi katika Gereza la Lilungu mkoani Mtwara, walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji ya mfungwa.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mtwara na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Abdulhaman Mohamed mbele ya Hakimu Stepheni Mbungu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Oktoba 31, mwaka 2010 watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua mfungwa aliyekuwa na namba 215, Kasimu Kumchaya.

Waziri anusurika ajali ya ndege


Ndege ya Shirika la Ndege la ZanAir iliyopata ajali jana Mkoa wa Kusini Pemba

Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakari Khamis Bakar, abiria na marubani wawili wamenusurika kifo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata ajali.
Waziri Bakar pamoja na abiria wapatao 17 walipata ajali hiyo kisiwani Pemba jana baada ya breki za ndege hiyo ya Shirika la Ndege la ‘ZANZ AIR’ kushindwa kufanya kazi, muda mfupi baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, nje kidogo ya Mji wa Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya ndege hiyo kutua ikitokea Unguja, ilikwenda kwa kasi na walitarajia ingepunguza mwendo kama ilivyo kawaida, lakini ilishindwa kufanya hivyo.
Walieleza kushtushwa na ndege hiyo iliyokuwa ikiendelea kwenda kasi mfano wa gari la mashindano, hali iliyomlazimu mwongoza ndege aliyekuwa akijiandaa kuiongoza kuikwepa kwa kukimbilia kando ya uwanja huo kunusuru maisha yake.
Meneja wa uwanja huo Rajabu Ali Mussa, alisema: “Ni kweli, tukio hilo lilitokea saa 10:30 jioni baada ya ndege hiyo kupata hitilafu ya kiufundi. Uchunguzi wa awali ulionyesha chanzo cha ajali ni kufeli kwa breki zake.”
Aliongeza: “Ni kweli jana ndege hiyo ya ‘ZAN AIR’ ilipata hitilafu na kuingia kwenye nyasi, lakini baadaye abiria wote waliokuwemo na marubani wake wawili, walitoka salama.’’
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Saleh Mohamed Saleh alisema tangu jana jeshi hilo, limeimarisha ulinzi kuzunguka eneo la uwanja, ili kulinda ndege hiyo.

Ana umri wa miaka 12, aolewa kwa ng’ombe 15


Wamasai ni miongoni wa jamii chache duniani, ambazo zimefanikiwa hadi sasa kudumisha mila zake. Katika mila za jamii hii, zipo ambazo zinapaswa kuendelezwa na nyingine zinapaswa kupigwa marufuku.
Miongoni mwa mila ambazo zinapaswa kuendelezwa ni pamoja na kuendelea kutambua na kuheshimu viongozi wa mila ‘Laigwanaji’ kuheshimu viongozi wa rika na Serikali, kuishi kwa umoja na kudumisha tamaduni.
Mila ambazo zimepitwa na wakati katika jamii hii ni pamoja na kurithi wajane, ukeketaji watoto na kuoa watoto wadogo.
Katika makala hii, leo nitazungumzia mila ya kuoa watoto wadogo kama nilivyobaini katika vijiji kadhaa wanapoishi Wamasai, wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara.
Nikiwa katika uchunguzi wa mapigano baina ya wafugaji wa Kimasai na wakulima katika vijiji saba vinavyozunguka eneo la Hifadhi ya Emborey Murtangosi nakutana na mtoto wa miaka 12 aliyeolewa.
Nilipata bahati ya kufika katika familia ya mtoto huyu, katika Kitongoji cha Ndiligishi kaya ya Engusero Sidani baada ya kuwa ni moja ya familia ambazo zimeathirika na mapigano baada ya kuchomewa makazi na kuibiwa vyakula.
Wakati nahojiana na wanafamilia napata fursa ya kuonana na mtoto huyo aliyegeuzwa kuwa mke, nashawishika kumuhoji baada ya kuona akiwa amejitenga na watoto wenzake huku akiwa na mawazo.
Mtoto huyo ambaye jina lake tumelihifadhi kutokana na sababu za kimaadili, hajui kiswahili  vizuri, hivyo nalazimika kumuomba mtoto mwenzake, Stela Paulo aje anisaidie kuongea naye.
Ananieleza kuwa yeye ni mke wa Lembau Leseri  na ameolewa  mke wa pili na ana miaka miwili ya ndoa.
Akiwa  anaonekana kutokuwa na raha ya maisha, mtoto huyo anasema wazazi wake, ndio walimpeleka kwa mwanaume baada ya kupewa mahali.
Anasema hajui kusoma wala kuandika kwani hakufanikiwa kupelekwa shule na wazazi wake.
Ninapomdadisi kama angependa kusoma, anasema angepata fursa hiyo angefurahi lakini sasa haiwezekani tena kwani ni mke mtu.
Kwa umri wake na umbile bado ni mdogo lakini, anaeleza huku akiwa kichwa chini na kwa aibu kuwa majukumu yote muhimu kwa mume wake aliyepewa na wazazi anafanya.
Hata hivyo, mtoto huyu anaonekana afya yake kudhoofika kutokana na maradhi ya ngozi na huenda na majukumu ya kifamilia.
Mume wa mtoto azungumza.
Mume wa mtoto huyo, Lembau Leseri hivi sasa ni mgonjwa na takriban wiki mbili, alikuwa amelazwa hospitali ya kiteto kutokana na kutokewa na majipu mwilini.
Ananieleza kuwa, mtoto huyo ni mke wake wa pili, ambaye alimuoa kutoka kijiji jirani cha Taiko.
Anasema mke wake wa kwanza, Kawie Lembau sasa ana watoto saba.
Lembau haoni kama amefanya makosa kuoa mtoto mdogo, kwani ananieleza kuwa alimuoa kwa ng’ombe 15.
Hata hivyo, anaeleza maisha yake ya ndoa na mtoto huyo, hayakuwa ya taabu kwa mwaka mmoja uliopita lakini sasa ana matatizo kutokana na kukabiliwa na maradhi.
“Sijui naumwa nini kwani nimelazwa hospitali na wamenipa dawa nirudi nyumbani,” anasema.
Anasema licha ya maradhi yanayomkabili,  maisha yamekuwa ya magumu, mapigano ya ardhi yameifanya familia yake kukosa chakula kwani zaidi ya magunia 50 ya mahindi yaliibwa.
Anasema pia vijana wa kiume wa familia yao, wamekimbia kwa sababu  polisi wanaendesha msako kuwakamata waliohusika na mauwaji ya wakulima tisa kutokana na mapigano ya ardhi.
“Hali ni ngumu, mimi naumwa siwezi kutembelea umbali mrefu kutafuta chakula, vijana wa hapa wamekimbia wanaogopa polisi,”anasema Lembau

Hali ya njaa katika familia hiyo yenye maboma matatu, inathibitishwa na jinsi nilivyoikuta akina mama wazee na watoto wadogo walikuwa wakichemsha mchicha majira ya saa saba lakini hadi naondoka takriban saa tisa walikuwa hawajala chakula kingine.
Mke mkubwa
Mke mwingine wa Lembau ambaye anaonekana ni mtu mzima ni mkimya na nilipotaka anieleze kuhusiana na mke mwenza wake  anashindwa kusema kitu na anaingia ndani ya boma lao.
Lakini natambua kwa mila za kimasai ni nadra sana mwanamke kuwa na ujasiri kupingana na mwanaume kutokana na misingi ya mila na desturi zao.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu wazungumza.
Shilinde Ngalula ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), anapatwa na mshangao anapoelezwa mtoto huyo ni mke wa mtu hasa kutokana na umri wake mdogo.
Hata hivyo, baada ya kuzungumza naye anaeleza kusikitishwa na maisha ya ndoa ya mtoto huyu.
“Hili ni tatizo kubwa katika jamii hizi kwani mtoto huyu alipaswa kuwa shule lakini kaolewa na mtu mzima ambaye sasa ni mgonjwa,”anasema Shillinde.
Shilinde na maafisa wengine wa LHRC ambao wanafanya uchunguzi wa mapigano baina ya wakulima na wafugaji wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, anaahidi kutafuta muda muafaka kufuatilia maisha ya mtoto huyo.
“Jamii hizi za pembezoni zinakabiliwa na matatizo mengi ambayo mengine yanatokana na kutokuwa na mazingira bora ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu”
Shillinde hata hivyo, anaongeza kuwa umefika wakati, Serikali na wadau wengine kufika maeneo ya vijiji katika jamii kama za kimasai ili kusaidia kutatua matatizo yao ikiwepo ya umasikini,elimu na mila zilizopitwa na wakati.
Je, maisha ya ndoa ya mtoto huyu yataendelea vipi kwa sasa kwani licha ya kuwa na umri mdogo bado ana mzigo mkubwa wa kumuuguza mume wake na je, nani atamuokoa na ndoa ya utotoni na kumrejesha shule kwa watoto wenzake?
 Hili ni swali zito lisilo na jibu kwa sasa hata hivyo huenda LHRC wakalivalia njuga suala hilo na haki kupatikana kama ambavyo tayari wameahidi.

Ng’wanamalundi; Mtu wa miujiza aliyeutesa utawala wa Wajerumani

 
Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.
Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa.
Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita, Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini.
Sitta anasema aliwaambia kuwa kabla ya vita, itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).
Sitta anasema utabiri huo ulitimia, kwani mvua ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya Wamasai na wafuasi wake yalipoanza.
Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde na mishale waanze kushambulia.
Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.
Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega, ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe.
Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke aliyejifungua, mtoto alikufa. Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye.
Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao. Hivyo aoe msichana atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu Marieta.
Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli yake ya kuendesha kikundi cha ngoma.
Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini

Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa, Sitta anasema siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.
Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema “Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.
Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea Kwimba.
Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima, ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia.
Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni yote haya mkapikie.” Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula.
Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi imesimama, alipohoji kwanini kazi imesimama alielezwa wananchi wote wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi.
Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo, ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.
Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga.
Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo.
“Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.” Akiwa na maana hii shoka ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa nimerudishwa.”
Sitta anasema Ng’wanamalundi aliendelea kumpa maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa Mwanza.
Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo Sitta alieleza kuwa walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha mauaji ya kishirikina
Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia huko Bukumbi Mwanza.
Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza kwenda Shinyanga.
Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza Wajerumani…
Inaendelea wiki ijayo
 

Dk Slaa: Uswahiba wa JK, Kawambwa unaua elimu


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema, uswahiba wa Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ndiyo chanzo cha kuporomoka kwa cha elimu nchini.
Dk Slaa alisema hayo jana kwenye Viwanja vya Jojo Kata ya Santilya, Mbeya Vijijini ikiwa ni siku ya tatu ya Operesheni la Vuguvugu la Mabadiliko (M4C), Pamoja Daima.
Alisema Dk Kawambwa hana uwezo wa kuongoza wizara hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa na Chadema kilishangazwa na mabadiliko aliyoyafanya Rais Kikwete katika baraza lake huku akimwacha waziri huyo katika nafasi hiyo.
“Kawambwa ni janga la elimu, hana uwezo. Chadema tutaendelea kumshtaki kwa wananchi. Mfumo mzima wa elimu nchini unahitaji mabadiliko, ili kufika huko wanahitajika viongozi wabunifu,” alisema Dk Slaa huku akishangiliwa na mamia ya wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Aliongeza: “Elimu yetu iko shakani, sasa hivi mwenye shahada mbili anafanana na aliyemaliza darasa la nne la zamani.”
Alisema viongozi wa Serikali na CCM hawana uchungu kwa kuwa watoto wao wanasoma nje ya nchi hivyo aliwataka wananchi kuitosa CCM katika kila ngazi ya uchaguzi.
Dk Slaa alitumia nafasi hiyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu.
Naye Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama ‘Sugu’ aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea Udiwani wa Chadema, Elisha Mwandele katika uchaguzi mdogo wa Kata ya Santilya utakaofanyika mwezi ujao.
“Ninyi wananchi ndiyo wenye mamlaka kwa kila kitu, nawaombeni mumchangue Mwandele ili awe diwani wa kata hii na mabadiliko yataendelea nchi nzima ili tutume salamu kwa CCM,” alisema Mbilinyi.
Katika hatua nyingine, Helikopta ‘Chopa’ inayotumika katika ziara hiyo ililazimika kukaa kwa zaidi ya saa mbili katika uwanja wa Jojo kutokana na mvua na ukungu.
Kabla ya kufika hapo helikopta hiyo ilikuwa ikitokea Kyela mkoani humo na baadaye hali ya hewa iliporejea katika hali ya kawaida ziara iliendelea kwa Jimbo la Mbozi, kisha kuelekea katika Mkoa wa Katavi.
Heche awabana Kinana, Nape 

Kutoka Arusha, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche amesema Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape wanapaswa kujiuzulu, kutokana na mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, kuwapuuza na kuwateua mawaziri waliowaita ni mizigo.
Mkutano huo ambao ulifanyika viwanja vya Ngusero Kata ya Sombetini, Heche alisema kama viongozi hao, walikuwa wanatoa kauli za kuwapinga kwa dhati mawaziri mizigo na siyo kuwalaghai wananchi wanapaswa kuwajibika wao kwa kupuuzwa na mwenyekiti wao.
“Sisi Chadema msimamo wetu upo wazi, hao mawaziri mizigo, tunajua hawana uwezo lakini CCM haina ubavu wa kuwang’oa,” alisema Heche.
Kwa upande wake, mwanasheria na Chadema, Tundu Lissu alisema Watanzania wasitarajie mabadiliko yoyote katika utendaji wa mawaziri.
Hata hivyo, Lissu alisema kazi kubwa ambayo wanapaswa kuifanya ni kujitokeza kuandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura ili wawe na uwezo wa kupitisha Katiba Mpya na kushiriki katika chaguzi.
Alisema msimamo wa chama hicho ni kuwa kama daftari la kura halitafanyiwa marekebisho wanachama wote wa chama hicho, watasusia kura ya maoni ya Katiba Mpya. Lissu alisema wanajua CCM ndio inafanya njama za kutoboreshwa daftari la kura kwa kuwa wanajua vijana wengi wakijiandikisha ndio utakuwa mwisho wa CCM.
Lissu pia alisema, CCM imeshindwa kuongoza ndiyo sababu imekuwa ikishindwa kusimamia hata rasilimali za nchi, yakiwamo madini, hifadhi za taifa na mambo mengi muhimu.
Awali, Lissu aliwataka wakazi wa kata hiyo kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili wamchague mgombea udiwani wa kata hiyo ya Sombetini kupitia Chadema, Ally Benanga.
“Mgombea wetu ni kijana wenu mnamjua, hivyo kazi ni moja tu kumpa kura siku ya uchaguzi Februari 9 mwaka huu,”alisema Lissu.

Friday, 17 January 2014

Makamanda wa jeshi watimuliwa Nigeria

 Jeshi la Nigeria limekuwa likipambana na wapiganaji wa Boko Haram lakini changamoto ni nyingi
Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan, amewafuta kazi makamanda wake wakuu wa jeshi ,na kufanya mabadiliko ambapo amemteuawa mkuu wake wa ulinzi, wakuu wa majeshi ya anga na majini .
Hakuna sababu iliyotolewa kuhusu hatua hiyo .
Mkuu wa mpya wa majeshi Alex Badeh, anatoka kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
Jeshi la Nigeria limekuwa likihangaika kudhibiti uasi wa kundi la kiislam la , Boko Haram, ambalo limekuwa likiendesha harakati zake zaidi katika maeneo ya Kaskazini Mashariki mwa nchi.

Muigizaji Suchtra afariki dunia India

 
Muigizaji nguli wa Sinema nchini India Suchitra Sen amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 82 kutokana na maradhi ya kifua.
Mwana filamu huyo alilazwa hospitali nchini humo kwa zaidi ya mwezi mmoja kutokana na matatizo kifua lakini bado hali yake ilizidi kuzorota zaidi jana usiku na kisha kumsababishia kifo.
Suchitra Sen aliyejulikana kwa jina la Greta Garbo wa India maisha yake yalikuwa ni ya kujitenga na watu wengine. Sen alijipatia umaarufu mkubwa katika uigizaji ambapo aliigiza filamu nyingi za Bollywood kama vile Devdas na Aandhi.
Alikuwa miongozi mwa waigizaji nguli kati ya waigizaji wa Bengali, aliungana na waigizaji wengine kama Uttam Kumar na wakaweza kutengeneza mfululizo wa filamu iliyochukua miongo miwili.
Baadhi ya waigizaji waliowahi fanya kazi na Sen wanamuelezea kuwa alikuwa ni mtu wa tofauti na mwenye kipaji kikubwa katika fani ya uigizaji.
Sen alianza uigizaji 1953 na filamu yake ya kwanza ilikuwa Seventy-four-and-a-half ambayo yeye aliigiza kama muuguzi na kuonekana kumudu sana nafasi hiyo.
Familia ya Sen ni waigizaji akiwemo mtoto wake wa kike Moon Moon Sen na wajukuu zake Riya na Raima Sen.
- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf