Ndege ya Shirika la Ndege la ZanAir iliyopata ajali jana Mkoa wa Kusini Pemba
Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, Abubakari Khamis Bakar, abiria na marubani wawili wamenusurika kifo baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kupata ajali.
Waziri Bakar pamoja na abiria wapatao 17 walipata
ajali hiyo kisiwani Pemba jana baada ya breki za ndege hiyo ya Shirika
la Ndege la ‘ZANZ AIR’ kushindwa kufanya kazi, muda mfupi baada ya kutua
katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume, nje kidogo ya Mji wa
Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, baada ya
ndege hiyo kutua ikitokea Unguja, ilikwenda kwa kasi na walitarajia
ingepunguza mwendo kama ilivyo kawaida, lakini ilishindwa kufanya hivyo.
Walieleza kushtushwa na ndege hiyo iliyokuwa
ikiendelea kwenda kasi mfano wa gari la mashindano, hali iliyomlazimu
mwongoza ndege aliyekuwa akijiandaa kuiongoza kuikwepa kwa kukimbilia
kando ya uwanja huo kunusuru maisha yake.
Meneja wa uwanja huo Rajabu Ali Mussa, alisema:
“Ni kweli, tukio hilo lilitokea saa 10:30 jioni baada ya ndege hiyo
kupata hitilafu ya kiufundi. Uchunguzi wa awali ulionyesha chanzo cha
ajali ni kufeli kwa breki zake.”
Aliongeza: “Ni kweli jana ndege hiyo ya ‘ZAN AIR’
ilipata hitilafu na kuingia kwenye nyasi, lakini baadaye abiria wote
waliokuwemo na marubani wake wawili, walitoka salama.’’
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Saleh
Mohamed Saleh alisema tangu jana jeshi hilo, limeimarisha ulinzi
kuzunguka eneo la uwanja, ili kulinda ndege hiyo.
No comments:
Post a Comment