Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna Msaidizi Omary Mtiga
Askari Magereza wanane, wamefikishwa mahakamani wilayani Mafia mkoani Pwani kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa.
Mbele ya Hakimu Mwandamizi Mfawidhi wa Wilaya ya
Mafia, Hassan Makube, ilidaiwa kuwa, Desemba 19 mwaka jana, askari hao
walimuua Basiri Makungu aliyekuwa akitumikia kifungo katika Gereza la
Kilombero, lililopo kwenye wilaya hiyo. Askari waliofikishwa mahakamani
hapo walitajwa kuwa ni Sajenti Sadick na wenzake ambao walifunguliwa
kesi namba 1/2014.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, watuhumiwa hao kwa
pamoja walimuua Makungu, baada ya kumshambulia kwa kipigo mwishoni mwa
mwaka jana.
Kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo
kisheria kusikiliza kesi hiyo hadi Mahakama Kuu, pamoja na kesi ya
mauaji kutokuwa na dhamana, watuhumiwa hao walirudishwa rumande hadi
Februari 7 mwaka huu.
Akizungumzia tukio hilo, ofisa wa juu wa Jeshi la
Magereza, Menrad Tesha alisema kuwa, jeshi hilo linafahamu taarifa za
askari hao kushtakiwa kwa makosa hayo, lakini akasema suala hilo halipo
chini yao. Tesha alipohojiwa kuhusu mustakabali wa ajira za askari hao
na iwapo wanashtakiwa kama raia au wafungwa alisema hawezi kulizungumzia
hilo kwa sasa.
“Siwezi kuzungumzia ajira zao hapa, huu siyo
utendaji unaotakiwa, kila kitu kina taratibu zake, hivyo siwezi
kulizungumzia hilo,” alisema Tesha.
Alieleza kuwa askari anapotuhumiwa kwa makosa
yoyote suala lake huachwa mikononi mwa vyombo vinavyostahili, ili
kuwachukulia hatua.
“Hivi sasa wale ni watuhumiwa, kwa hiyo mimi
kuliongelea siyo sahihi. Kama kuna kitu ungetaka kufahamu, basi
nakushauri mfuate mkuu wa gereza kule walipo sasa (Mafia), atakueleza
kila unachotaka kufahamu kuhusu askari hao kwani bado wapo huko,”
alisema Tesha.
Matukio ya Askari Magereza kuua wafungwa
Februari mwaka jana ilidaiwa kuwa Willfred Mallya
mwenye namba 315 aliyefungwa mwaka 2003 katika katika Gereza la Kisongo
mjini Arusha aliuawa kutokana na kipigo cha Askari Magereza.
Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Magereza, Kamishna
Msaidizi Omary Mtiga licha ya kukiri kutokea kwa kifo cha mfungwa huyo,
alikanusha kuwa kilitokana na kipigo cha askari hao akisema kifo chake
kilikuwa ni cha kawaida.
Desemba mwaka 2010, askari wanne wa jeshi hilo
waliokuwa wakifanya kazi katika Gereza la Lilungu mkoani Mtwara,
walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za mauaji ya mfungwa.
Watuhumiwa hao walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa
wa Mtwara na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali, Abdulhaman
Mohamed mbele ya Hakimu Stepheni Mbungu.
Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Oktoba 31, mwaka
2010 watuhumiwa hao kwa pamoja walimuua mfungwa aliyekuwa na namba 215,
Kasimu Kumchaya.
No comments:
Post a Comment