Hali ya usalama Tarime imezidi kutoweka baada ya jambazi lisilofahamika likiwa na bunduki ambayo haijafahamika aina yake kuendelea kuua watu kwa risasi hasa wa jinsi ya kiume, ambapo idadi ya waliouawa imefikia saba hadi sasa na inadaiwa huwaua watu na kupotea bila kutambuliwa.
Jambazi hilo lisilofahamika liliua watu hao usiku
wa Januari 27, mwaka huu katika maeneo ya Nkende likianza na kumuua
Mwendesha Bodaboda, Juma Marwa Mkazi wa Nkende mjini Tarime akiwa
anaelekea nyumbani kwake ambaye alikufa akiwa hospitali akipatiwa
matibabu.
Mganga wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa
Tarime, Marco Nega alisema tangu Januari 27 hadi sasa hospitali
imeendelea kupokea watu waliouawa na majeruhi ambao wamefanyiwa
uchunguzi na kugundulika wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi katika sehemu
mbalimbali za mwili na kwamba watu wapatao 7 wamekwisha kufa mpaka sasa.
“Tumepokea maiti za watu na majeruhi na
tumewafanyia uchunguzi wakagundulika wana majeraha ya risasi sehemu
mbalimbali za mwili, ambapo tayari watu saba wamekufa wengine wamekufa
wakiwa njiani wakienda kwenye matibabu Musoma, marehemu hadi ni saba,”
alisema Nega.
Waliojeruhiwa wakosa huduma ya X-ray
Watu waliojeruhiwa wameshindwa kupatiwa huduma ya
X-Ray kutokana na Hospitali ya Wilaya kutokuwa na huduma hiyo kwa muda
wa zaidi ya miezi 3 na kusababisha wagonjwa kusafirishwa kwenda Musoma
na Mwanza kwa matibabu, ambapo Samweli Richard amekufa akiwa njiani
kuelekea Musoma kwenye matibabu ikiwamo huduma hiyo ya X-ray.
Hospitali ya Wilaya yashindwa kutoa huduma
Huduma kwa wagonjwa mbalimbali katika Hospitali ya
Wilaya imeshindwa kuendela vilivyo baada ya kupatwa na misiba miwili ya
watumishi wawili, ni baada ya waume zao kuuawa na jambazi hilo
lisilofahamika.
Awali Januari 26 jambazi hilo lilimuuwa Robert
Kisiri (45) mkazi wa Mugabiri ambapo Mstaafu wa JWTZ Zacharia Mwita(58)
na Erick Makanya (25)wote wakazi wa Kijiji cha Mogabiri Kata ya Kitare
Wilayani Tarime walikutwa wakiwa wameuawa na miili yao ikiwa na majeraha
ya risasi mbavuni kushoto na mgongoni.
Pia jambazi hilo liliwajeruhi watu watano kwa
risasi ambao ni Mgosi Marwa Mkazi wa Mogabiri, Joseph Richard Mkazi wa
Rebu, Gastor Richard Mkazi wa Rebu, Juma Mwita Mkazi wa Mogabiri na
Mkandarasi Binafsi wa ujenzi, Mwasi Yomami ambao kati ya hao wawili
wamefariki wakati wakipatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Kipolisi Tarime/Rorya, Justus Kamugisha amesema wamemkamata mtu mmoja
anayeshukiwa kuwa mhusika wa mauaji ambaye yuko chini ya ulinzi kwa
mahojiano na kwamba anazidi kuongeza vikosi vya doria kuimarisha ulinzi
na usalama na kuwasaka wahalifu.
Wananchi wacharuka
Wananchi Mjini Tarime waliitaka polisi kuhakikisha jambazi hilo
linapatikana vinginevyo walitaka polisi kuwakabidhi bunduki ili waweze
kumsaka jambazi huyo.
‘Kamanda kashindwa kazi haiwezekani mtu mmoja aue
watu 7 ndani ya siku mbili, huu ni uzembe wa polisi katika kuimarisha
ulinzi, tunaomba tukabidhiwe bunduki tulisake jambazi,” alisema
mwananchi mmoja.
No comments:
Post a Comment