Ikulu imetaka kufungwa kwa mjadala wa kuhusu kurudishwa kwa mawaziri wanaodaiwa kuwa ni mizigo kwenye Baraza la Mawaziri na badala imetaka waachwe wafanye kazi.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu
alisema kuendeleza mjadala huo ni kupoteza muda, kwani Rais Jakaya
Kikwete alishamaliza kazi yake.
Rweyemamu alisema Rais ndiye mwenye mamlaka ya
kuteua mawaziri ambao wana wajibu wa kumsaidia katika utekelezaji wa
majukumu yake, hivyo si sahihi wateule hao kuitwa ‘mizigo’ kwani yeye
(Rais) ameona wanafaa.
“Rais anapoteua watu anaangalia wanaofaa kumsaidia
na si vinginevyo. Kwani lengo lake ni kuona nchi ina `move forward’
(inasonga mbele) kimaendeleo,” alisema Rweyemamu. Alisema watu wanapaswa
kukumbuka kuwa mtu anapoteuliwa kwenye uwaziri kuna suala la
uwajibikaji: “Anatakiwa kutekeleza uwajibikaji wa pamoja. Sasa
kumshambulia mtu binafsi na kumwita mzigo siyo sahihi.”
Rweyemamu alisema mjadala huo kwa sasa umepitwa na wakati na kuwataka wananchi na wachambuzi kuwaacha mawaziri hao kuchapa kazi.
“Ni vizuri wananchi wakawapa nafasi mawaziri hawa
ya kufanya kazi na baadaye kuwapima na kuwachambua kutokana na utendaji
wao,” alisema.
Chimbuko la majadala
Mjadala kuhusu suala hilo unatokana na Rais
Kikwete kuwarejesha katika Baraza la Mawaziri baadhi ya mawaziri ambao
walidaiwa kuwa ni mizigo kutokana na udhaifu katika utendaji wao.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na Katibu
wake wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye ndiyo walioasisi mawaziri hao
kuwa ni ‘mizigo’ walipokuwa na ziara ya kikazi mkoani Ruvuma, mwishoni
mwa mwaka jana.
Mawaziri waliolalamikiwa kutokana na utendaji wao
ni wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Kilimo, Chakula
na Ushirika, Christopher Chiza, aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo
na Uvuvi, Dk David Mathayo, Waziri wa zamani wa Fedha, marehemu Dk
William Mgimwa na aliyekuwa Naibu wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam
Malima.
Baadaye baadhi ya wabunge nao walikoleza moto kwa
kushinikiza mawaziri hao wang’oke, huku wakiongeza idadi yao kwa
kuwataja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia na
Manaibu wake, Aggrey Mwanri na Kassim Majaliwa katika kundi hilo.
Mawaziri hao waliitwa kujieleza mbele ya Kamati Kuu ya CCM kuhusu sababu za utendaji wao kuwa wenye matatizo.
Hata hivyo, kabla ya Rais Kikwete kuchukua hatua, alitengua
uteuzi wa Mawaziri wanne, Dk Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi
Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa), Balozi Khamis Kagasheki
(Maliasili na Utalii na Dk Mathayo kutokana na mjadala mkali bungeni
kuhusu jinsi Serikali ilivyotekeleza Operesheni Tokomeza Ujangili.
Kadhalika, Dk Mgimwa aliyefariki dunia Januari 5, mwaka huu alisababisha pengo la mawaziri kufikia watano.
Wakati Rais Kikwete alipofanya mabadiliko katika
Baraza lake Januari 19, mwaka huu, karibu mawaziri wote waliolalamikiwa
walirejeshwa.
Hali hiyo ilizusha mjadala mkali kutoka kwa watu
na makundi mbalimbali, huku CCM kupitia kwa Nape Nnauye kilisema
kitaendelea kupiga kulele pale utendaji wa mawaziri hao utakapokuwa
mbovu.
No comments:
Post a Comment