Wakenya wangali wanasubiri tume aliyoahidi Rais Uhuru Kenyatta baada ya tukio la kigaidi katika jengo la Westgate hasa baada ya uamuzi wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama, ambayo ilisema Serikali ya Kenya ilionywa takriban siku 19 kabla ya uvamizi huo lakini haikuchukua hatua yoyote.
Jeshi la Polisi pia lilielekezewa kidole cha
lawama na kamati hiyo kwa kukosa ushirikiano na kikosi cha JeshiUlinzi
wakati wa uokoaji na kusababisha maisha ya watu wengi kuangamizwa.
Kuhusu uchunguzi huu, familia za walioathiriwa
wakati wa uvamizi huo wa Septemba 21, mwaka jana wanaweza kuamua kwenda
mahakamani kuishtaka Serikali kwa kukosa kuchukua hatua kuzuia vifo na
majeruhi.
Watu 67 walifariki dunia katika tukio hilo la
waasi wa Al-Shabaab waliovamia Jengo la Westgate ambalo lilikuwa na
maduka na hoteli za kifahari.
Uchunguzi wa wabunge ulionyesha kwamba, Kikosi cha
Jeshi la General Service Unit (GSU) kilikuwa kimefanikiwa kuwapata
wavamizi ndani ya jengo hilo, lakini kilichofanya wasiwaue ni hatua ya
kikosi cha Jeshi la Kenya Defence Force (KDF) kuwasili na kuwatimua
(GSU) kabla ya kufanikiwa kuwavamia waasi hao.
Mwaka mmoja kabla ya uvamizi huo, Idara ya
Upelelezi na Jinai iligundua kwamba waasi wa Al-Shabaab walikuwa
wanapanga kuvamia Westgate. Walitoa taarifa kwa vyombo vya usalama
lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Onyo jingine lilitolewa kati ya Agosti 6 na
Septemba 2, 2013. Inasikitisha kuwa, licha ya kupewa habari hizo,
Serikali iliendelea kulala na kuwapa nafasi waasi kupanga na kuvamia
bila wasiwasi wowote.
Vikosi vyote vya usalama havina budi kuwajibika
wakati wote na kuweka mpaka kati ubinafsi, ufisadi na kuzembea kazini
ili waweze kuwatumikia na kuwalinda Wakenya. Kwa kufanya hivi
tutaepukana na hali iliyotokea, ambapo watu wanapoteza maisha na wengine
kujeruhiwa.
Wataalamu waliohojiwa na kamati hiyo walisema KDF
hawangefaa kutumwa kuokoa watu kwenye jengo hilo kwa sababu kitengo
maalumu cha GSU tayari kilikuwa kimetumwa Westgate na walikuwa wanafanya
kazi nzuri ya kuwanasa au kuwaua waasi.
Maswali ya kuuliza
Kwa nini hakuna hatua iliyochukuliwa na polisi baada ya Idara ya Upelelezi kutoa habari kuhusu uvamizi huo?
Kwa nini vikosi mbalimbali vya jeshi na polisi
vilikosa kutimiza majukumu yao? Je, kulikuwa na kutoelewana kati ya
vikosi hivi ama kila mmoja alikuwa anahisi kwamba ni bora kuliko
mwingine?
Je, kwa nini KDF ilipowasili Westgate ilianza kuwatumia GSU ilhali walikuwa kwenye harakati za kumnasa na kumwangamiza adui?
Bunge litafunguliwa mwezi ujao na ripoti hii bila shaka litazua hisia mbalimbali itakapoanza kujadiliwa na wabunge.
Wabunge wanasema kwa vikosi vya usalama kukosa
kuchukua hatua ya kuzuia uvamizi, waasi waliweza kufanya uvamizi kama
ule uliofanywa Mumbai, India miaka michache iliyopita.
Kuna habari kwamba ingawa wavamizi wanne
walitambuliwa, idadi kamili ya waasi waliotekeleza unyama huo
haijulikani. Inasadikika kwamba walikuwa 15.
Kamati hiyo ya Bunge inasema waasi walionaswa na
kamera za usalama ni Abu Baraal, Al Sudani, Omar Naban na Khatab Al
Kene. Inaaminika kwamba wavamizi hao wote walifariki kwenye uvamizi huo.
Mawasiliano
Wabunge walisema kwamba mipango ya uokoaji
ilisambaratishwa tangu mwanzo wake. Waliongeza kwamba mawasiliano kati
ya kituo cha kutoa habari kuhusu mambo yaliyokuwa yanaendelea katika
Westgate na idara za Serikali zinazohusika na usalama yalikuwa na
dosari.
Wakati huo baadhi ya habari ilikuwa kwamba,
wavamizi wengine walifanikiwa kutoroka kupitia kwa bomba la majitaka,
huku wengine wakisema wote waliuawa.
Hii ni kizungumkuti. Na swali ni je; wavamizi
walitoroka au waliuliwa. Je, mwanamke aliyejulikana kama “The White
Widow” alikuwa mmoja wa wavamizi au ulikuwa uvumi mwingine wa vikosi vya
usalama?
Awali, Mkuu wa KDF, Jenerali Joseph Karangi
alitangaza kwamba licha ya tuhuma za wizi dhidi ya KDF, kikosi hicho
hakikuiba chochote kutoka Westgate. Karangi alipoulizwa kwa nini KDF
walinaswa wakibeba mifugo ya plastiki iliyokuwa imejaa pomoni, alisema
hayo yalikuwa maji.
Alisema jeshi lilichukua maji kutoka katika duka
la jumla la Nakumatt kwa sababu walikuwa wanahisi kiu. Lakini kamati
hiyo imeikuta KDF na kosa la kuiba bidhaa na pengine na pesa wakati wa
shughuli za uokoaji uliochukua siku nne.
KDF ikipatikana na kosa la kuiba, wafanyabiashara
wengi waliopoteza bidhaa na pesa zao wanaweza kwenda kortini wakitaka
kulipwa na serikali.
Ripoti hii haitaji watu binafsi waliohusika na kuzembea kazini
na kupelekea wavamizi kutekeleza unyama wao Septemba 21 mwaka jana.
Si vikosi vya usalama tu ambavyo vimepatikana na
kosa la kutotimiza wajibu wao inavyotakikana. Wizara ya Uhamiaji
ilipatikana na maswali ya kujibu kuhusu ni vipi wageni waliingia nchini
na kupata vibali vya kukaa Kenya na kutekeleza uvamizi huo mbaya zaidi
tangu ule wa 1998 ambao Ubalozi wa Amerika ulivamia na watu zaidi ya 200
kupoteza maisha.
Wizara hii, kwa muda mrefu imekuwa ikituhumiwa kwa
kutoa vibali kama vile pasipoti na vitambulisho kwa wageni baada ya
kupewa hongo. Wengi wa wanaopewa vibali na stakabadhi za kuishi Kenya
wamegunduliwa kuwa ni waasi au washiriki wao.
Mwaka jana, akizungumza na vyombo vya habari vya
Ufaransa, Mkuu wa Sheria, Profesa Githu Muigai alisema Rais angeunda
jopo la kuchunguza Westgate punde tu baada ya Kamati za Bunge kumaliza
uchunguzi wake.
Ripoti ya kamati
Ripoti ya Kamati imejumuisha uchunguzi wa
kitaalamu uliofanywa na mashirika mbalimbali ya kigeni, likiwamo Shirika
la Kijasusi la Marekani (FBI).
Kulingana na taarifa hiyo ya kitaalamu, ni
wavamizi wanne tu waliohusika kwenye uvamizi wa Westgate na wote
waliuawa. Taarifa hiyo inaongeza kwamba baadhi ya miili iliyopatikana
kwenye vifusi vya Westgate ilikuwa ya waasi hao.
Iliongeza kwamba, silaha zilizopatikana kwenye jengo hilo zilikuwa za waasi.
Ripoti hiyo ilitoa mapendekezo kadhaa ili
uwezekano wa nchi kuvamiwa tena upunguzwe; Serikali ya Kenya itangaze
vita dhidi ya Al-Shabaab ndani na nje ya Kenya na pia kituo cha
kuwezesha vikosi vyote vya usalama kupokea habari za kiusalama kibuniwe
haraka iwezekanavyo.
Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kwamba, Wizara ya
Uhamiaji ifanyiwe mabadiliko ili wafanyakazi wenye ujuzi wa usalama
waweze kuajiriwa.
Pengine pendekezo litakalozua utata ya kitaifa na
kimataifa ni lile linalotaka kambi zote za wakimbizi zifungwe na wote
warejeshwe makwao ili usalama wa Wakenya upewe kipaumbele.
Kwa hamu Wakenya wanasubiri Rais wao awaambie ni
lini ukweli kuhusu uvamizi huu utajulikana baada ya kubuniwa kwa jopo la
kutafuta ukweli kuhusu tukio hilo lililobadilisha historia ya Kenya.
No comments:
Post a Comment