Blogger Widgets

Friday, 24 April 2015

ACT yavuna wanachama wapya 6,000

Chama cha ACT-Wazalendo kimehitimisha ziara katika mikoa 10 nchini huku kikijigamba kuingiza wanachama wapya zaidi ya 6,000.
Kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema jana kuwa ziara hiyo ilikuwa na mafanikio makubwa.
“Leo tumetimiza kilomita 5,802 katika kituo chetu cha mwisho cha Maswa, Mkoa wa Simiyu,” alisema Zitto na kuongeza:
“Tumepata wanachama 6,391, katika mikoa mbalimbali na wote wameandikishwa na namba zao za simu zimeingizwa kwenye database (mfumo maalumu wa kutunza kumbukumbu).
“Mkoa ambao umeongoza kwa wanachama kuchukua kadi uwanjani ni Tabora, tuwalipata 815, lakini Makambako walikuwa 104.”
Zitto ambaye aliacha uanachama na ubunge wake katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwishoni mwa mwezi uliopita, kwenye ziara hizo alionekana kivutio na mwenye ushawishi kwa wananchi kutokana na mapokezi aliyopata.
Alisema akiwa Simiyu mijadala waliyozungumza na wananchi katika ziara hizo ni kuhusu mkoa huo kuwa wa mwisho kwenye elimu.
Zitto alisema ni asilimia 3.7 tu ya watu wenye miaka 25 mkoani humo, wana elimu ya sekondari na kuendelea.
Pia alisema walizungumza kuporomoka kwa pamba kwa asilimia 47 baada ya wananchi kususia sera za Serikali ya CCM kuhusu zao hilo.
“Hiyo inatokana na bei ya Sh600 kwa kilo moja anayopewa mkulima wakati katika soko la dunia imefika Dola 1.2 za Marekani,” alisema Zitto ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Pamba ilishuka kwa kuingiza fedha za kigeni kwa asilimia 32 mwaka 2013 na 2014 imeporomoka kabisa.
Ziara ya chama hicho iliyodumu kwa wiki mbili, ilianzia Ruvuma na kuendelea katika mikoa ya Njombe, Iringa, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Mara na Mwanza.
Chama hicho kilikuwa kinajitangaza kwa mara ya kwanza katika mikoa inayodaiwa kuwa ngome ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf