Blogger Widgets

Sunday, 2 February 2014

Upanuzi wa Bandari bado kizungumkuti

 
Upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam, uliosababisha kung’olewa kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Omary Nundu, umeendelea kupata vikwazo baada ya kampuni ya Kichina iliyopewa zabuni ya upanuzi huo kutofika kwa kazi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari(TPA), Madeni Kipande aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC), iliyofanya ziara jana katika bandari hiyo kuwa hatua  hiyo licha ya kuwasikitisha imesababisha kuchelewa kwa upanuzi huo.
“Hiyo kampuni ya kichina ilitakiwa iwe imeanza kazi tangu Oktoba mwaka jana,  lakini ajabu ni kwamba ipo kimya na hakuna mawasiliano ya aina yoyote. Tumeamua kufuta zabuni hiyo, tutatangaza nyingine mapema mwezi huu kwa kuwa tunakusudia kwamba, Julai tuwe tumeshaanza kazi. Hapa hatutaki siasa zimetuchosha,” alisema Kipande.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kabwe Zitto aliisisitiza TPA kuhakikisha kwamba zabuni hiyo inatangazwa na kukamilika mapema akieleza kuwa kuendelea kuchelewesha kuanza kwa upanuzi huo ni kuikosesha mapato Serikali.
“ Upanuzi huo ni muhimu sana kufanyika kwa sababu ukikamilika ndiyo unaoweza kuweka ushindani na Bandari ya Mombasa, pia itasaidia kuiongezea mapato Serikali,” alisema Zitto.
Kamati hiyo pia ilisisitiza TPA kuhakikisha inaanza matumizi ya kupakua mafuta kwa njia ya mita kwa sababu utaratibu wa kupima kwa kijiti(Dip Stick) unaikosesha mapato Serikali.
“ Katika hili tumeamua kuunda kamati maalumu, itakayofuatilia kwa kina kubaini kwa nini tangu utaratibu huo ulipopaswa kuanza kutumika mwaka 2008 umekuwa ukipigwa danadana. Tunahisi kuna jambo, inawezekana hata ni hujuma za wafanyabiashara wa mafuta, tutaujua ukweli,” alisema Zitto.
Akiwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Shukuru Kawambwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Bandari, walitafuta mkopo kutoka Serikali ya China kupitia Benki ya Exim ya nchi hiyo iliyoridhia kutoa Dola 524 za Marekani ili zisaidie upanuzi wa Gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf