Aliwahi kuzipamba kurasa za Jarida la Forbes mwaka 2011 akiwa ni miongoni mwa wanawake tisa wa kiafrika wanaoongoza kwa utajiri. Siyo hivyo tu, bali ana cheo kikubwa akiwa ni Mkurugenzi Mtendaji, wa Benki ya Dunia(WB).
Ni Dk Mamphela Ramphele, mwenye umri wa miaka 66
ambaye hivi karibuni alitangaza kuwania nafasi ya urais nchini humo,
kwenye uchaguzi ambao utafanyika miezi minne ijayo nchini Africa Kusini.
Ramphele amedhamiria kuwa mwanamke wa kwanza
nchini humo kuwania urais na pia kuutaja utajiri wake ambao ni randi
55 milioni (Dola za Marekani 5.5milioni).
Uchaguzi wa Rais na wabunge ambao unatarajiwa
kufanyika Aprili au Mei mwaka huu, ni wa kwanza baada ya kifo cha Rais
mstaafu Nelson Mandela.
Ramphele, ambaye ni mwanasiasa mkongwe, mhadhiri
na mhudumu wa afya, mwenye mafanikio makubwa na Mkurugenzi wa sekta
nyeti ya uchimbaji wa madini, alikaririwa akisema maamuzi yaliyofanywa
na chama chake ya kumchagua kuwa mgombea wa urais ni yenye tija kwa
Waafrika wa Kusini.
“Nimefarijika na kukubali mwaliko huu wa chama cha
Democratic Alliance,(DA) kuwa mgombea wa urais kwa mwaka 2014,”
alisema Dk Ramphele.
Ramphele alizaliwa jimbo la Bochum, Kaskazini mwa
Transvaal,(hivi sasa Limpopo). Alimaliza elimu ya sekondari,
Setotolwane, mwaka 1966 na akajiunga na kozi fupi ya tiba kwenye chuo
kikuu cha Kaskazini.
Mama yake, Rangoato Rahab, na baba yake Pitsi
Eliphaz Ramphele walikuwa walimu wa shule ya msingi. Mwaka 1944 baba
yake alipandishwa cheo na kuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Stephanus
Hofmeyer.
Akiwa Chuo Kikuu, Ramphele alianza kuvutiwa na
siasa za wanafunzi na ubaguzi wa rangi na hapo alikuwa mwanzilishi wa
Chama cha Watu Weusi(BCM). Muungano huo wa wanafunzi kupinga ubaguzi wa
rangi ulikuwa chanzo cha kukutana na Steve Biko, miongoni mwa wanasiasa
wakongwe wa Afrika Kusini. Urafiki kati ya Ramphele na Biko, ulikua na
kuzua mapenzi ambayo yaliwapa zawadi ya watoto wawili, Lerato Biko,
(aliyezaliwa mwaka 1974) na Hlumelo Biko(1978). Hata hivyo, Lerato
alifariki baada ya kuugua nimonia.
Safari yake kisiasa
Mwaka 1955
Ramphele alishuhudia mgogoro kati ya mbaguzi wa rangi, Dominee na watu wa Kijiji cha Kranspoort jambo ambalo liliamsha ari yake ya kuwa mwanasiasa.
Ramphele alishuhudia mgogoro kati ya mbaguzi wa rangi, Dominee na watu wa Kijiji cha Kranspoort jambo ambalo liliamsha ari yake ya kuwa mwanasiasa.
Miaka ya 1970 na kuendelea, Ramphele aliendelea
na shughuli za kisiasa akiwa bega kwa bega na Steven Biko, Barney
Pityana pamoja na wanafunzi wengine wanaharakati wa chuo cha tiba.
Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tawi la chama kabla ya kupata cheti
chake cha Chuo Kikuu.
Alipata nusu ajira katika Hospitali ya Mfalme Edward wa nane na baadaye alihamia Hospitali ya Livingstone, Port Elizabeth.
Mwaka 1974, Ramphele aliendeleza harakati zake
ambapo alikuwa akiwahamasisha watu wajiunge kwenye miradi ya kijamii.
Akijumuisha na elimu yake ya tiba, alikuwa pia mkurugenzi wa Mpango wa
Wanajamii Weusi(BCP) Mashariki ambako Biko alipigiwa marufuku kuonekana.
Agosti mwaka 1976, Ramphele aliwekwa kizuizini
chini ya sheria namba 10 ya ugaidi akiwa ni mtu wa kwanza kuwekwa
kizuizini kwa sheria hiyo mpya.
Mwaka 1977, Ramphele alizuiwa asitoke maeneo ya
Tzaneen, Kaskazini mwa Transvaal ambako alibaki hadi mwaka 1984. Hata
hivyo, muumini mmoja wa kanisa la kijijini hapo aliwaandaa watawa
wawili, wa Kiafrika, ambao walimtoa mafichoni na kumtafutia nyumba
kwenye Lenyenye, Tzaneen ingawa aliendelea kufuatiliwa na polisi.
Akiwa hapo, alipata msaada wa hati ya kusafiria
kutoka kwa Mbunge wa Chama cha PP, Helen Suzman ambayo aliitumia
kusafiria kwenda nchi za nje kujinoa kielimu na kisiasa.
Mwaka 1983 alimaliza shahada yake ya kwanza ya
Mawasliano kwenye Uongozi kutoka Chuo Kikuu cha UNISA ambako alijiunga
tangu mwaka 1975. Alimaliza pia Diploma ya Afya ya Umma Chuo Kikuu cha
Witwatersand.
Nyadhifa alizoshika
Mwaka 1991 alichaguliwa kuwa msaidizi wa masuala
ya utafiri chuo Kikuu cha Cape Town, na mwaka 1996 wakati huo huo
aliteuliwa kuwa Makamu Mkuu wa Chuo hicho akiwa ni mwanamke wa kwanza
mwafrika kushika nafasi hiyo kwenye Vyuo Vikuu vya Afrika Kusini.
Mwaka 2000, Ramphele alikuwa miongoni mwa
Wakurugenzi wakuu wanne wa Benki ya Dunia akiwa na majukumu ya
kuangalia shughuli zinazofanywa na benki hiyo. Ni mwafrika Kusini wa
kwanza kushika nafasi hiyo.
Pamoja na nafasi nyeti ya WB, Ramphele aliwahi
kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Taasisi ya Mo Ibrahim ambayo
inashughulikia utawala bora na uongozi Afrika.
Mwaka 2013, alionyesha dalili za kurejea kwenye
siasa za nchini Afrika Kusni akiachia ngazi kwenye nafasi yake ya
Uenyekiti wa Gold Fields. Februari 18, 2013 alitanganza kuanzisha chama
kipya cha siasa, kilichopewa jina la Agang(maana yake ni Jenga) ambacho
kilipanga kukipa changamoto chama cha ANC, kinachotawala nchini humo.
Hata hivyo, kuingia kwa Ramphele kwenye siasa
kumepokelewa kwa changamoto na ukosoaji mwingi kutoka kwa wachambuzi wa
masuala ya siasa. Wakosoaji hao walidai kuwa amekuwa akitoa taswira
mbaya kwa marehemu Biko katika mikutano yake ya siasa.
Kujiunga na kuteuliwa kwa Ramphele na chama cha DA kama mgombea
wa Urais kunatajwa kuwa ni sehemu ya mapinduzi ya chama hicho ambacho
kina wazungu wengi kukusanya kura za watu weusi.
Tathmini ya hivi karibuni imeonyesha kuwa, Chama
cha ABCM kimeshuka kwa asilimia 53 na Chama cha DA kimepanda kwa
asilimia 18. Wakati huo huo, mwanachama mkongwe wa ANC, Julius Malema,
alikihama chama hicho na kuunda chama kipya cha Economic Freedom
Fighter.
No comments:
Post a Comment