Akiwa anaendelea na ngoma yake wananchi wa Kijiji cha Sekke waliibiwa ng’ombe wengi sana na watu kutoka Kabila la Wamasai ambao walienda kuwahifadhi katika Pori la Mwanima karibu na Kijiji cha Bubiki.
Ng’wanamalundi na kikosi chake waliondoka Wilaya
ya Kwimba mkoani Mwanza na kuelekea Sekke wilayani Kishapu mkoani
Shinyanga kwa lengo la kusaidia kuzikomboa ng’ombe zilizoibwa.
Hata hivyo kabla hawajafika uwanja wa vita,
Ng’wanamalundi alifanya utabiri wake uliotokana na nguvu ambazo
alizipata kutoka kwa Bibi Kizee wa porini.
Sitta anasema aliwaambia kuwa kabla ya vita,
itatokea mvua kubwa sana na ikikatika watakuja ndege hai aina ya mwewe
watakaokuwa wanazungukazunguka kwenye zile ng’ombe na hapo sasa wafuasi
wake wakate miti mifupi mifupi (Lubugu).
Sitta anasema utabiri huo ulitimia, kwani mvua
ilinyesha kubwa sana na baada ya kukatika wale mwewe walijitokeza wengi
sana wakawa wanazunguka kwenye zile ng’ombe na ndipo yale mapigano ya
Wamasai na wafuasi wake yalipoanza.
Aliwaeleza kuwa baada ya kuwa na fimbo ya Lubugu
wale wenye upinde na mishale watakaa nyuma na kazi yao watakuwa
wanazipiga zile ngao za Kimasai na zikidondoka chini ndipo wenye pinde
na mishale waanze kushambulia.
Mwanamalundi alipigana hiyo vita ya Wamasai mpaka
akazirejesha zile ng’ombe na aliwatokomeza Wamasai mpaka kwenye mpaka wa
Mto Manonga unaotenganisha Tinde Shinyanga na Nzega mkoani Tabora.
Hapo ndipo ilibainika Wamasai hao walikuwa
wametumwa kuiba ng’ombe Usukumani na Mtemi Tinginya wa Busongo Nzega,
ambapo baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi na kundi lake walirudi Sekke na
kupewa jina la Kishosha Mang’ombe tafsiri ikiwa ni mrudisha ng’ombe.
Baada ya vita hiyo Ng’wanamalundi alirudi nyumbani
kwao wilayani Kwimba kuoa, lakini bahati mbaya ilimkuta, kwani kila mke
aliyejifungua, mtoto alikufa. Baba yake Bugomola akaenda Ntuzu kwa sasa
Bariadi kufanyiwa tambiko kuhusu uzazi kwa mwanaye.
Akiwa huko Ntuzu, Bugomola alielezwa mwanaye
Ng’wanamalundi hatapata mtoto kwa wake zake alionao. Hivyo aoe msichana
atakayempata upande wa Mashariki ambaye atakuwa akiitwa Nkamba na atazaa
watoto watatu; wa kwanza ataitwa Sitta, wa pili Ngassa na wa tatu
Marieta.
Baada ya kurudi Bugomola, haikumchukua muda
mwanaye Ng’wanamalundi akapata msichana akaoa na akaendelea na shughuli
yake ya kuendesha kikundi cha ngoma.
Ng’wanamalundi kuwekwa kizuizini
Akiwa anaendelea na ngoma zake katika maeneo ya Kanda ya Ziwa,
Sitta anasema siku moja yeye na kikundi chake walipokuwa wakiburudisha
katika maeneo ya Bukumbi mkoani Mwanza, wafuasi wake walipumzika kwenye
mti mkubwa ambapo pia kilikuwa Kituo cha Wajerumani, Ng’wanamalundi
aliwaambia wafuasi wake waondoke waende kwenye ngoma, wafuasi wake
waligoma wakadai wanapumzika kwenye kivuli hicho ili wavute sigara.
Baada ya kuwabembeleza vya kutosha akabaini
hawataki kumsikiliza ndipo alipounyooshea kidole ule mti akisema
“Ngh’walemelaga hanti gunugo aliyo gumaga,” akiwa na maana “Mmekatalia
kwenye mti huo huku ukiwa umekauka.” Ghafla mti huo wote ulikauka.
Kuona hivyo wafuasi wake wakaondoka wote kwenye
huo mti wakaenda kuendelea na ngoma yao ambayo walicheza katika eneo la
Bukumbi na Busagara karibu na Mji wa Mwanza na walipomaliza walirejea
Kwimba.
Akiwa Kwimba alicheza ngoma moja na Gindu Nkima,
ngoma hiyo ilikuwa ngumu kwake ilichezwa sehemu za Mwanagwa. Baada ya
kuwa amezidiwa Ng’wanamalundi, wapishi wake walimfuata na kumtaka
awasaidie namna ya kupata kuni za kupikia.
Kutokana na uharaka aliokuwa nao Ng’wanamalundi
alielekeza kidole chake kwenye miti ya minyaa iliyokuwa mbele yake huku
akisema “Batemagi pye abenababa mkazugile,” akiwa na maana “Yakateni
yote haya mkapikie.” Baada ya kauli hiyo minyaa yote ilikauka na kuwa
kuni na wafuasi wake walikata wakaenda kupikia chakula.
Akiwa katika ngoma hiyo wakati huo barabara ya
kutoka Shinyanga kwenda Mwanza ilikuwa inachongwa na manamba waliokuwa
wakikamatwa na Wajerumani kwa ajili ya kazi hiyo, Gavana wa Kijerumani
wa eneo la Mwanza alipita eneo hilo akiwa amepanda punda alikuta kazi
imesimama, alipohoji kwanini kazi imesimama alielezwa wananchi wote
wamekwenda kwenye ngoma ya Ng’wanamalundi.
Kitendo hicho kilimchukiza sana Mjerumani huyo,
ambaye aliondoka akaenda Mwanza na baada ya siku mbili walikuja askari
waliomkamata Ng’wanamalundi na kumfunga mnyororo na watuhumiwa wengine
walipelekwa Mwanza na kuwekwa gerezani.
Kosa hilo kwa utawala wa Ujerumani lilihesabiwa
kuwa ni uhaini wa kupinga utawala wao hivyo alitakiwa kupewa adhabu ya
kunyongwa. Kabla hajapelekwa Mwanza, kwa kuwa ilikuwa ni safari ya
kwenda kunyogwa, alipelekwa nyumbani kwa wazazi wake kuaga.
Alipofika nyumbani kwao alimpa mama yake shoka aliloliweka pembezoni mwa ukuta chumbani na maziwa, huku akitoa maelekezo.
“Mayu imbasa yeneye ulu yulina ng’wigulya
mumhonatwalwa ulu yika hase mumhonashoka amabele genaya ulu guganda
mumhonacha, ulu gita lububhi mumhonasata.” Akiwa na maana hii shoka
ikipanda juu basi nitakuwa nimepelekwa ikishuka chini nitakuwa
nimerudishwa.”
Sitta anasema Ng’wanamalundi aliendelea kumpa
maelekezo mama yake kuwa haya maziwa yakiganda atakuwa amekufa na pindi
yakipata utando atakuwa anaumwa, baada ya maelezo hayo Ng’wanamalundi
alipelekwa Mwanza gerezani ambako alikutana na Mtemi Makongoro wa
Mwanza.
Siku iliyofuata walitolewa wote ambapo Sitta
alieleza kuwa walikutana pia na mganga aliyemtabiria kuzaa watoto watatu
ambaye naye alikuwa amekamatwa kwa kosa la kupiga ramli iliyosababisha
mauaji ya kishirikina
Asubuhi kila mmoja alisomewa mashtaka yake ambapo Ng’wanamalundi
alisomewa mashtaka matatu, shtaka la kwanza kuukausha mti uliokuwa
ukitumiwa na maofisa wa utawala wa Wajerumani kama kituo cha kupumzikia
huko Bukumbi Mwanza.
Shtaka la pili kuwatungia na kuwaimbia nyimbo
mbaya Wajerumani na la tatu ni kukwamisha ujenzi wa Barabara ya Mwanza
kwenda Shinyanga.
Ng’wanamalundi alidaiwa kuchezesha ngoma eneo la
Mwanangwa hali iliyosababisha wafanyakazi wa manamba waliokuwa wakilima
barabara hiyo kuacha na kwenda kuangalia ngoma yake hali iliyowachukiza
Wajerumani…
Inaendelea wiki ijayo
No comments:
Post a Comment