Jinamizi la ajali za barabarani zikihusisha mabasi zimeendelea kugharimu maisha ya Watanzania baada ya jana watu 10 kupoteza maisha na wengine 50 kujeruhiwa vibaya wakati basi la Unique Express lililokuwa likitokea Mwanza kuelekea Tabora kugongana uso kwa uso na lori la Coca-Cola lililokuwa likitokea Tinde kuelekea Shinyanga.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 8.45 mchana katika Kijiji cha Ibingo, Kata ya Samuye, Shinyanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye eneo la
tukio, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha alisema
chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa basi uliosababisha dereva wake
kushindwa kulikwepa lori hilo lililokuwa katikati ya barabara.
Alisema watu tisa walifariki dunia papohapo na mmoja alifia katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga akipatiwa matibabu.
Kamanda Kamugisha alisema dereva wa lori anashikiliwa na polisi mwenzake wa basi hali yake ni mbaya na amelazwa hospitali.
Alisema wengi waliofariki dunia walikuwa
wamekandamizwa na vyuma hali iliyowalazimu kuomba msaada wa winchi
kuliinua basi hilo na kuwatoa.
Kamanda Kamugisha aliwataka wananchi na abiria
kutoa taarifa pindi wanapoona madereva wakiendesha mwendo ambao unaweza
kuhatarisha maisha yao.
Baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo akiwamo Diwani
wa Kata ya Samuye, Amos Shija walisema walishtushwa na kishindo cha
kugongana kilichofuatiwa na kelele na vilio vya abiria.
Shuhuda, John Bundala aliitaka Serikali kuendelea
kuwachukulia hatua kali madereva ambao hawazingatii sheria za usalama
barabarani na kupoteza maisha ya watu wasiokuwa na hatia na wengine
kupata ulemavu.