Moja ya malengo ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januri 12,1964 ni kuleta usawa na wananchi wanyonge kupewa ardhi yenye rutuba iwasaidie kwa kilimo na kujiletea maendeleo.
Ndoto hiyo ilitimia baada ya utawala wa Kisultani
kuangushwa na chama cha ASP na baadaye Rais wa kwanza wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ) marehemu Abeid Amani Karume kutangaza kuwapa
wananchi ekari tatu kila mmoja.
Tangazo hilo lilitolewa Dole Novemba 11, 1965,
mahali ambapo sasa pamejengwa mnara wa kumbukumbu ya tukio hilo, ikiwa
sehemu ya kuhitimisha utawala wa Kisultani uliodumu kwa miaka 160 tangu
mwaka 1804.
Maeneo mazuri ya ardhi yakiwamo ya Mwera,
Bumbwini, Dole, Gamba, Bambi, Cheju, Upenja na kwingineko yalikabidhiwa
kwa wazalendo na hivyo kuondoka mikononi mwa masetla wa kikoloni
waliokuwa wakiyamiliki.
Mageuzi ya mambo
Mambo sasa ni kinyume. Maeneo hayo kwa sehemu
kubwa yameanza kuchukuliwa tena na vigogo na watu wenye fedha wakiwamo
waliokuwa wamenyang’anywa na SMZ mwaka 1964 baada ya mapinduzi.
Maeneo hayo ndiyo yanayoongoza kwa uzalishaji wa
mazao ya chakula kwa wingi, lakini sasa yameanza kuvamiwa kwa ajili ya
ujenzi nyumba za makazi na maeneo ya biashara, huku wananchi waliokuwa
wakiyatumia kwa kilimo wakiachwa kwenye mataa.
Mussa Shaaban Masele (63), mkazi wa Dole anasema
kwamba malengo ya kuwapatia wananchi ardhi yameanza kuvurugwa kwa kasi
ya ajabu, hasa baada ya ardhi kuwa ya thamani na kuingia kwa wawekezaji
Zanzibar.
Kwa mujibu wa Masele, ardhi ya Zanzibar sasa ni
mali na utajiri mkubwa. Anasema vigogo serikalini na watu wenye fedha
hutengeneza hati bandia na kuwafukuza wanyonge kwa madai kuwa ardhi hiyo
inamilikiwa kisheria na watu wengine, huku wakionyesha hati ‘feki’ za
umiliki.
Kosa la kisheria
Kosa lililofanyika baada ya tamko la SMZ
kutangazwa na Rais wa kwanza Abeid Karume, wananchi wengi hawakupewa
hati, hivyo ikawa rahisi kuondoshwa kwa madai kuwa hawana hati za
kisheria.
“Huu ni utumwa mpya unaoisakama Zanzibar baada ya
miaka 50 ya Mapinduzi. Tunarejea tulikotoka, hakuna mtetezi wa hayo,
watu wanajali fedha na si utu kama ilivyokuwa enzi za ASP na uhai wa
Karume,” anasema Masele.
Anasema hata mashamba makubwa ya SMZ waliyopewa wananchi kwa
shughuli za kilimo huko Dole, Kilombero, Mwakaje na Cheju yameanza
kuchukuliwa na kupewa baadhi ya wakubwa serikalini bila huruma wala
aibu.
Anatoa mfano wa wakulima 145 huko Dole wako katika
mgogoro mkubwa na Wizara ya Ardhi na Wizara ya Kilimo baada ya kutakiwa
wahame na ili maeneo hayo wapewe watu wengine.
“Iwapo SMZ ilitaka maeneo hayo yagawiwe upya na
kumilikiwa, ilistahili waliokuwapo na kuendesha kazi za kilimo
wafikiriwe kwanza, kinyume chake wanaporwa na wakubwa wenye nguvu za
kifedha na madaraka. Huu ni ukatili mpya kuliko ule wa Waarabu,”
anasema.
Anasema mgogoro huo tayari umefika hadi katika
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais baada ya ngazi ya shehia, wilaya na mkoa
kushindiwa huku zikiwapo dalili za vigogo kubebena na kuwakandamiza
wanyonge.
Maeneo wanayodai kuporwa, wakulima hao wamepanda mazao ya kudumu ikiwamo mishelisheli, mitufaa, minazi, midimu na michungwa.
“Tunachokitaka sasa kukutana na Rais ana kwa ana,
tumechoka kuonewa. Tutamkabili na kutaka atuambie ukweli kama nia hii
mbaya ni ya SMZ au inafanywa na majambazi wa ardhi wanaosaka utajiri.
haitakuwa ajabu kumwaga tena damu kutetea haki yetu,” anaonya.
Kwa upande wake Khadija Omar anasema ataendelea
kumkumbuka Mzee Karume kwa uamuzi wa kuwapatia wananchi ekari tatu za
ardhi na kusema ilikuwa ni kazi ya kijasiri na kiimani.
Hata hivyo amesema inashangaza sana leo baada ya
miaka 50 kupita viongozi wale wale walioachiwa nchi wanaanza ukatili,
manyanyaso na uonevu.
Kilimo duni
Hata hivyo, anasema pamoja na wananchi kulilia
ardhi hiyo, bado wanakabiliwa na ukosefu wa zana na nyenzo za kisiasa za
kilimo na utaalamu. Wamejikuta wakibaki pale pale katika mkakati wa
kuzalisha mazao ya chakula yasiyo na tija huku wakiambulia chakula cha
miezi miwili tu baada ya msimu.
Anasema kabla ya 1964 ardhi ya Zanzibar
ilimilikiwa na masetla na mabepari walikuwa wakiwatumia wananchi
wanyonge kuwalimia mashamba bila kunufaika kwa lolote huku wakilipwa
ujira mdogo.
“Nafikiri kazi ya kuwakomboa Waafrika wanyonge na
mateso ya mabepari weupe imekwisha, sasa ipo haja ya kuwatazama wakoloni
weusi wasiojali haki, usawa wala utu wa kila binadamu,” anasema
Khadija.
Kadhia ya migogoro ya ardhi Zanzibar imekithiri pamoja na kuwepo
kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1992 bado wananchi hawaijui sheria na
kuwafanya wamiliki wapya wa ardhi kutengeneza nyaraka na kupora
wanyonge.
Suluhu ya migororo
Kamati ya Kushughulia Migogoro ya Ardhi chini ya
Ali Mzee Ali imetoa mapendekezo yake likiwamo la kutungwa kwa kanuni kwa
kila shehia, baada ya kubainika kukosekana kwa kanuni ya ardhi
kunakosababisha kukosekana mwongozo wa matumizi bora ya ardhi.
Kamati inasema inataka kufanya utambuzi wa ardhi
kama njia mojawapo kwa Wazanzibari kupata haki kutokana na kukosekana
kwa kumbukumbu za maeno ya ardhi yaliotolewa kwa watu mbalimbali.
Kukosekana kwa mfumo wa hifadhi ya kumbukumbu (data base) pia kunachangia hati ya moja ya ardhi kutolewa kwa mtu zaidi ya mmoja.
No comments:
Post a Comment