Baada ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe kuibuka kidedea katika pingamizi lake la kuvuliwa uanachama hivi karibuni, macho na masikio sasa yameelekezwa kwenye hatima yake ndani ya chama hicho.
Akisoma hukumu hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya
Dar es Salaam, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Albert
Msando na kuipiga marufuku Kamati Kuu ya Chadema au chombo chochote,
kujadili uanachama wa Zitto hadi kesi ya msingi itakapotolewa uamuzi.
“Nakubaliana na hoja za Wakili Msando, pande mbili zinapopingana lazima shauri lao lisikilizwe mahakamani ili haki itendeke.
“Mdai akivuliwa uanachama, akapoteza nafasi yake
ya ubunge, Serikali italazimika kufanya uchaguzi mdogo, kufanya uchaguzi
mdogo ni hasara kwa Serikali kwani utahusisha hadi wapiga kura hali
itakayosababisha fedha nyingi kutumika, itakuwa hasara kwa Zitto
kupoteza nafasi mbili, ya ubunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali kabla kesi yake ya msingi haijasikilizwa,” alisema.
Kauli ya Zitto
Akizungumza na mtandao wa ‘Millardayo.com’ baada
ya kutolewa kwa uamuzi huo, Zitto anasema ushindi huo ni kwa Watanzania
wanaopenda siasa safi.
“Kwanza nataka niseme wazi kabisa kwa Watanzania
ambao ni wanachama wa vyama vingine, wasio na vyama na kwa wanachadema,
ushindi huu siyo ushindi dhidi ya Chadema, ni ushindi kwa Watanzania
wote wanaopenda siasa safi, wanaopenda taratibu za utawala bora zifuatwe
kwenye taasisi zetu, ni ushindi dhidi ya wanaotaka kukandamiza
demokrasia ndani ya vyama, ni ushindi dhidi ya wahafidhina wasiotaka
mabadiliko katika vyama,” anasema Zitto na kuongeza:
“Huu siyo ushindi dhidi ya chama kwa sababu siwezi
kushindana na chama changu, ni chama ambacho kimenilea na nimekitumikia
kwa muda wangu wote, zaidi ya nusu ya umri wangu ambao nimeishi... Kwa
hiyo salamu ambazo napenda wananchi wazifahamu ni kwamba tunahitaji
kuheshimu sana demokrasia na misingi ya haki za binadamu.”
Wakati viongozi wa Chadema wakimpiga marufuku
Zitto kujihusisha na kazi zozote za chama wala wanachama wengine kumpa
ushirikiano, mwenyewe anasisitiza yuko tayari kufanya kazi hizo.
“Mimi bado ni mwanachama wa Chadema, pamoja na
kwamba Katibu Mkuu wa Chadema ametoa amri ya watu wasinipe ushirikiano
lakini pale nitakapohitajika nitafanya shughuli za Chadema, nitafanya
shughuli za nchi yangu,” anasema na kuongeza:
“Sasa hivi kuna masuala makubwa kuhusu Katiba ya nchi yetu na ningependa wananchi wajielekeze huko.
Kwa nini Chadema imepoteza?
Akitoa ufafanuzi, Wakili na Mkurugenzi wa Sheria, Katiba na Haki
za Binadamu wa Chadema, Peter Kibatala anasema shauri hilo
lilifunguliwa likiwa na sehemu kuu mbili yaani shauri la msingi na
maombi madogo ya zuio la muda.
“Katika shauri kuu, mwombaji anaiomba Mahakama Kuu
kutoa amri tatu; kwamba Chadema izuiwe kujadili suala la uanachama wake
mpaka pale atapopewa nakala za mwenendo na uamuzi wa Kamati Kuu kumvua
nafasi za uongozi na rufaa yake dhidi ya uamuzi huo kusikilizwa na
Kamati Kuu ya Chadema.
Pia anataka Chadema iamuriwe kuitisha Baraza Kuu ili kujadili Rufaa hiyo,” anasema na kuongeza:
“Msingi wa madai ni kwamba wakati mchakato wa
rufaa haujakamilika na wakati hajapewa nakala za mwenendo na uamuzi wa
kumvua nafasi za uongozi, ameitwa na Kamati Kuu kujadiliwa kuhusu
uanachama wake.
“Katika shauri dogo lililotolewa uamuzi
mahakamani, mwombaji aliomba amri ya zuio ili Kamati Kuu au chombo
kingine cha Chadema kisijadili uanachama wake mpaka shauri la msingi
litakaposikilizwa na kutolewa uamuzi na Mahakama Kuu.”
Shauri hilo lilifunguliwa Januari 2 mwaka huu,
siku ambayo mawakili Kibatala na Tundu Lissu wa Chadema walitoa
mapingamizi dhidi ya maombi hayo na vifungu vya sheria ambavyo havikuwa
sawa.
Hoja za kinaLissu zilisema, hati ya kiapo ina
upungufu na mahakama haina mamlaka kujadili migogoro ya vyama vya siasa
na taasisi zenye tabia ya uhiari. Mahakama ilikataa mapingamizi yao
yote.
“Wakati wa usikilizaji, Mahakama yenyewe (suo
mottu) ikazitaka pande zote ziieleze Mahakama Kuu iwapo ni sahihi wakili
kula kiapo kwa niaba ya mteja katika shauri kama lile. Pande zote
ziliieza Mahakama kwamba ni sahihi, ingawa Wakili Msando alipinga aya ya
nne ya hati ya kiapo kwa sababu za kisheria.
Anaendelea kusema kuwa hoja zao zilisisitiza kuwa
mwombaji amepewa nafasi ya kusikilizwa kwa kuitwa Kamati Kuu, na kwamba
Mahakama haina mamlaka ya kuingilia mambo ya ndani ya taasisi kama
vyama vya siasa.
Majaliwa ya Zitto
Baada ya kushinda katika pingamizi lake la
kuikataza Kamati Kuu kutomjadili wala kumvua uanachama wake, sasa Zitto
anasubiri kusikilizwa kwa kesi yake mwezi ujao ili iwapo atashinda rufaa
yake isikilizwe na Baraza Kuu la Chadema badala ya Kamati Kuu na hayo
ndiyo majaliwa yake.
Inavyoonekana, ana imani na wajumbe wa Baraza Kuu
kuliko Kamati Kuu. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema Ibara ya 7.7.11
Wajumbe wa Baraza Kuu ni pamoja na wajumbe wote wa Kamati Kuu, Wenyeviti
wa Baraza la Uongozi, mikoa na wajumbe wateule wasiozidi sita
watakaoteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa kushauriana na Katibu Mkuu na
kuidhinishwa na Baraza Kuu
Wengine ni wajumbe watano watakaochaguliwa na Mkutano Mkuu wa
kila Baraza la chama, kwa uwiano wa wajumbe wanne kutoka Bara na mmoja
kutoka Zanzibar kwa kila Baraza.
Wengine ni wenyeviti wa wilaya za chama na
mwakilishi wa jimbo na chama. Hawa ndiyo watakaosikiliza na kuamua juu
ya rufaa ya Zitto atakapoiwasilisha kwao. Je, atasalimika?
Hata kama Zitto atatimuliwa na Baraza hilo, bado
anaweza kwenda mahakamani kupinga kutimuliwa, kama walivyofanya wabunge
wenzake, David Kafulila aliyevuliwa uanachama na NCCR-Mageuzi na Hamad
Rashid aliyetimuliwa CUF.
No comments:
Post a Comment