Ni jambo la kusikitisha lakini ndiyo ukweli kwamba kuna baadhi ya wenye mamlaka katika shule wanatumia madaraka yao kujipatia ngono kutoka kwa wanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi tayari wamenaswa, huku wengine
wakiambukizwa virusi vya Ukimwi au kuwa nyumba ndogo; sababu kubwa ni
umalaya wa baadhi ya walimu, huku kukiwa na hofu juu ya nini hatma ya
hali hii.
Mbaya zaidi ni kwamba mwalimu akiomba uhusiano kwa
msichana, akikataa, baadhi yao huwaharibia wanafunzi hao kwa maana ya
kuwapa alama mbaya katika mitihani yao, hata kama walifanya vizuri.
Wapo ambao wanashawishiwa na walimu kuingia kwenye
ngono, pia wapo wanafunzi wanawashawishi walimu kuanzisha uhusiano nao
ili kufanya masomo yawe mepesi.
Uhalisia wenyewe
Ngono inapandisha alama za kufaulu vyuoni, inamfanya aliye na uwezo mdogo kuwa kinara darasani.
Imefika hatua baadhi ya wanachuo wanajipanga
wakati wa mitihani yao, wanamtoa mmoja kafara kwa ajili ya wengine,
anashawishiwa akajipendekeze, agawe penzi kwa mwalimu ikibidi ilimradi
tu mambo yawe mepesi kwenye mtihani. Staili hii sasa inaitwa ‘kuzima
moto’.
Mchezo huu umekuwa maarufu, si kwenye vyuo vingi.
Linapotamkwa neno rushwa mara nyingi baadhi ya watu wanayaelekeza mawazo
yao kwenye sehemu zinazotoa huduma muhimu kama vile mahakama,
hospitali, polisi kutokana na sababu kuwa ni rahisi kuonekana.
Kupenyeza kwa kasi rushwa kwenye sekta ya elimu
kunaweza kuelezwa kuwa kunachochea kwa kasi kushuka kwa elimu miongoni
mwa wanajamii nchini. Kushuka huko kunaanzia ngazi za chini na katika
kwenda ngazi za juu.
Hali hiyo inatia shaka ya kuwepo kwa wataalamu
wasio na uwezo. Haya mambo ndiyo yanafanya kuwepo kudharauliwa kwa
wasomi wengi siku hivi, na hata maisha ya baadhi ya wasomi
yanadhihitisha hilo kwamba wengine elimu haiendani na uhalisia wao.
Lakini ni mara chache sana watuhumiwa wa kutoa au
kupokea rushwa hiyo wamekuwa wanakamatwa kwa kuwa sehemu kubwa ya utoaji
na upokeaji hufanyika kwa faragha.
Baadhi ya kesi za rushwa
Agosti 20, 2007, Mhadhiri wa chuo kikuu kimoja, alifikishwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu kwa tuhuma za kudai na kupokea
rushwa ya Dola za Marekani 1,000 kutoka kwa mwanafunzi wake.
Mshtakiwa aliachishwa kazi na mwajiri wake siku
mbili baada ya kufikishwa mahakamani. Hakuna waliofuatilia kesi hiyo
hadi mwisho na kama mhadhiri alipatikana na hatia au aliishinda.
Utafiti uliofanywa takriban miaka kumi iliyopita
ulibainisha kwamba sekta ya elimu hapa Tanzania, imechafuliwa na rushwa
za ngono au fedha.
Msichana anayefanikiwa kuhitimu kwa rushwa za
ngono huendeleza dhambi hiyo kupata ajira, vyeo kazini na hatimaye
nyadhifa za juu za uongozi. Wanawake waliofanikiwa kwa njia hii wapo
wengi katika utumishi serikalini, katika mahakama, vyama vya siasa,
Bunge nakadhalika.
Kinachotafutwa siku hizi na wasomi ni “bora elimu”
na siyo “elimu bora”. Wasomi wanajivunia vyeti vya kuhitimu vyuo vikuu
hata kama hawana maarifa yoyote ya kuboresha maisha ya binadamu.
No comments:
Post a Comment