Hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alifika katika Kijiji cha Kapunga wilayani Mbarali na kutamka wazi kwamba mgogoro uliodumu karibu miaka 10 umesababishwa na makosa ya watendaji wa Serikali.
Mgogoro huo unawahusisha wanakijiji zaidi ya
4,000 ambao wanakwaruzana na mwekezaji wa Kampuni ya Kapunga Rice
Project Limited ambaye alianza shughuli zake mwaka 2006.
Tangu kuingia kwa mwekezaji huyo, wananchi wa
kijiji hicho wamekuwa na misukosuko mingi ikiwamo ya kukosa huduma za
afya baada ya mwekezaji kuchukua majengo ya iliyokuwa zahanati ya
kijiji.
Ilielezwa kwamba mgogoro huo umesababisha vifo,
majeraha na hata kuleta madhara katika huduma za elimu, afya na maji.
Naye mwekezaji amekuwa akiwalalamikia wanakijiji kwamba ni wabishi,
wezi na wanafanya hujuma kwenye mashamba yake bila sababu za msingi.
Mgogoro huu unadaiwa kushughulikiwa na viongozi
wengi zikiwamo Kamati za Bunge bila mafanikio jambo ambalo wanakijiji
wanadai baadhi ya wenzao walishapoteza maisha huku naye mwekezaji
akisema amepata hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na mgogoro huo.
Historia ya Kijiji cha Kapunga
Kijiji cha Kapunga kipo Wilaya ya Mbarali mkoani
Mbeya. Ukitaka kufika katika kijiji hicho kama unatokea Barabara ya
Iringa kwenda Mbeya utafika Chimala wilayani humo na kugeukia kulia
ambako utaanza barabara ya vumbi umbali wa karibu kilomita 30.
Kijiji hicho kwa sasa kina karibu watu 4,400
wanaoishi kwenye vitongoji saba vya Lwanji, Mkanada, Tambalale,
Mapogolo, Site one, Matoleo na Ofisini ambacho ndicho chenye ofisi ya
kijiji. Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Peter Kitha anasema kijiji chake
kilisajiliwa kwa Na. MB/KIJ/936 kikiwa na ukubwa wa hekta 11,724.163.
Mwenyekiti wa kijiji Ramadhan Nyoni anasema
historia ya kijiji ni ya tangu miaka ya 60 kwani Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Nyerere alikanyaga kijiji hicho mwaka 1965.
Kijiji chaikaribisha Kampuni ya Kilimo Nafco
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Nyoni anasema mwaka
1985 Serikali kupitia Kampuni ya Chakula ya (Nafco) ilifika kijijini
kuomba eneo la kuanzisha mradi wa kilimo cha kisasa cha mpunga. Anasema
kijiji kilikaa na kuamua kuipatia Nafco hekta 5,500 za ardhi.
Nafco katika kuimarisha ushirikiano na wanakijiji
walitengeneza ramani iliyoonyesha eneo lake la Hekta 5,500 pamoja na
hekta zingine 1870 za kijiji na mashamba yao.
Kwa kutumia ramani hiyo, Nafco ilikwenda kuomba hati na
kuandikiwa hati moja iliyojumuisha hekta zote za Nafco na za wanakijiji
na kuwa na hekta 7,270.Bila kujali suala hilo kisheria, Nafco
iliendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na wananchi katika mradi wake
na kuwasaidia wananchi.
Lakini kama ilivyokuwa kwa mashirika mengine ya
umma, Nafco nayo ilidorora kiuntendaji na kusababisha Serikali itangaze
tenda ya kuliuza mwaka 1995. Mbunge wa Jimbo la Mbarali, Modestus Kilufi
anasema tenda ya Serikali ilitangazwa kuuzwa kwa Mradi wa Kapunga Rice
Project Limited wenye ukubwa wa Hekta 5,500.
Mradi huo kwa bahati nzuri ulipata wateja 2006
ambao waliununua , na kupewa hati inayojumuisha hekta 7,370 zikiwamo za
mashamba madogo ya wanakijiji na makazi ya watu.
Mwekezaji mpya alifika na kukukabidhiwa hati
inayoonyesha umiliki wa miaka 99 wa eneo lote la Hekta 7,370 ikiwamo
miundombinu yote na kiwanda cha kukoboa na kupanga madaraja mchele
ambacho ni cha pili kwa ukubwa katika Bara la Afrika.
Mwekezaji apanga kuwatoa wanakijiji
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Justin
Vermaak chini ya mwekezaji anasema alikabidhiwa hati safi yenye ukubwa
wa hekta 7,370, lakini cha ajabu alikuta ndani yake kuna watu wamejenga
makazi, zahanati na hata shule.
Mwekezaji alitangaza kuivunja zahanati ndani ya eneo lake, kuiondoa shule na wanakijiji pia.
Jambo hilo liliwashtua wanakijiji, lakini
alifanikiwa kuiondoa zahanati na shule iliyokuwa ndani ya eneo la Hekta
5,500. Mgogoro mkubwa ulianza pale alipotangaza kwamba eneo lote la
Kijiji ni mali yake huku akisisitiza kwamba hati aliyopewa imeonyesha
hivyo. Kwa habati mbaya wananchi hawakufahamu suala hilo kwamba hati
imempa umiliki mwekezaj huyo.
Matukio ya Uhasama
Wanakijiji wanadai mwekezaji huyo anawazuia
wananchi wasikatishe kwenye eneo la shamba lake wanapokwenda kulima
kwenye mashamba yaliyo upande wa pili mbele ya shamba lake. Anataka
wazunguke umbali wa kilometa 15 badala ya kukatisha shamba umbali wa
kilometa tano. Pia wanadai aliwahi kubomoa nyumba 18 za wakazi akitaka
waondoke.
Pia aliwahi kusababisha vifo vya watu wawili
aliokuwa akiwafukuza kwa kutumia gari. Na pia wanadai mwekezaji huyo
alinyunyizia sumu kwenye ekari karibu 500 za mashamba yao ya mpunga na
kusababisha kukauka wote. Hata hivyo suala hilo lilimalizwa mahakamani
ambako walioshtaki walishinda kesi.
Mwekezaji naye anasititiza kwamba wanakijiji ni
wavamizi wa eneo lake. Wanaiba vitu vyake ikiwamo mifuniko ya kukinga
maji na hata dawa za mazao. Anasema pia wapo wanakijiji ambao wameamua
kupasua maji kwenye chanzo cha maji na wakati wa kiangazi wanafunga maji
yanayohitajika kwenye mashamba yake.
Ujio wa Waziri Tibaijuka
Waziri Tibaijuka alipofika kijijini hapo Januari
7, mwaka huu alisisitiza kwamba alikuwa ni mwarobaini wa mgogoro huo.
Wanakijiji walimshangilia kwa furaha wakiamini mgogoro anaumaliza siku
hiyohiyo.
Lakini akihutubia kwenye mkutano wa hadhara baada
ya kupata taarifa za pande zote mbili alifafanua kwamba mgogoro huo
bado utendelea kusubiri. Alisema mwekezaji hana kosa kwani ulisababishwa
na makosa ya watendaji wa Serikali kupitia Nafco ambao , walichukua
hati inayojumuisha eneo la kijiji badala ya kuchukua ya eneo la Hekta
5,500 walizopewa na kijiji.
Tibaijuka alitaja kosa lingine kwamba nao maofisa
wa Serikali waliohusika katika kubinafsisha shamba hilo walimkabidhi
hati inayoonyesha hekta 7,370 mwekezaji ambaye kimsingi alitakiwa kupewa
hati ya Hekta 5,500.
Kwa hali hiyo, alisema kilichobaki ni kumwomba
mwekezaji arudishe hati hiyo ili ibadilishwe na kukabidhiwa hati
inayoonyesha Hekta 5,500 tu. Hoja hiyo iliwakatisha tamaa baadhi ya
wanakijiji na kulazimika kupiga kelele za kumpinga.
Mwekezaji akataa maombi ya
Serikali
Mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited akizungumzana Profesa Tibaijuka alikataa eneo lake kupunguzwa.
Ameweka masharti mawili ambayo ni kupewa eneo
lingine lenye ukubwa wa hekta 1,870 ama kufidiwa fedha ambapo kwa hekta
isiyoendelezwa anataka afidiwe Dola 2,000 za Marekani wakati
iliyoendelezwa afidiwe Dola 5,000 za Marekani.
Waziri Tibaigana amtolea macho.
Profesa Tibaijuka alimweleza bayana mwekezaji
huyo kwamba Serikali haiwezi kumfidia ardhi mwekezaji huyo kwa vile
ardhi yote ni ya wananchi. Pia alisema haiwezi kumfidia fedha zozote kwa
vile aliikuta miundombinu yote ikiwa tayari. Aliikuta mifereji,
majaruba, mtambo wa kukoboa mpunga na kutenganisha mchele kwenye
madaraja na kwamba aliinunua kwa bei ya chini ukilinganisha na thamani
halisi ya mradi.
Mwekezaji aomba akatoe jibu faragha
Mwekezaji Justin Vermaak alimwomba Waziri
Tibaijuka akatoe jibu kwenye gari lake wakati akizunguka naye
kumwonyesha mradi mzima. Tibaijuka alikubali na kupanda gari hilo. Baada
ya kukagua shamba lote la mwekezaji, Waziri alifafanua kwamba chanzo
cha mgogoro huo ni makosa ya watendaji wa Serikali. Alisema mwekezaji
hana makosa na kuhusu hati mwekezaji alisema hawezi kuitoa kwa sababu
ana wenzake sita ambao anatakiwa ajadilliane nao kwanza. Hivyo
kinachosubiriwa ni mpaka watakapojadili na ndipo watatoa jibu.
Wananchi wawekwa njia panda
Kauli ya Waziri Tibaijuka imewaweka njia panda
wananchi wa Kapunga. Kimsingi ni nzuri, lakini haina muda wa lini jambo
hilo litatekelezwa.
No comments:
Post a Comment