Mbunge wa Ubungo (Chadema) na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika amezidi kumng’ang’ania Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, safari hii akimtaka waziri huyo ajieleze mbele ya Rais Jakaya Kikwete sababu za kupanda kwa gharama za umeme.
Mnyika alianza kumshambulia waziri huyo baada ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kubariki
ongezeko la kupanda kwa gharama za umeme kuanzia Januari Mosi mwaka
huu,ikiwa ni miezi miwili tangu Shirika la Umeme Nchini(Tanesco)
lilipowasilisha ombi la kupandisha gharama hizo.
“Kwanza Profesa Muhongo alisema uongo kwa nyakati
mbalimbali mwaka 2012 na 2013, aliwahakikishia wananchi kwamba bei ya
umeme haitapanda, matokeo yake bei imepanda kulingana na makundi
mbalimbali ya matumizi ya wateja,” alisema Mnyika na kuongeza;
“Tanesco ilipendekeza kuongeza bei kwa asilimia
67.87 kuanzia Oktoba Mosi, 2013, asilimia 12.74 kuanzia Januari Mosi
mwaka huu na asilimia 9.17 kuanzia Januari Mosi, 2015.”
Alisema kitendo cha Tanesco kuomba kuidhinishwa
kwa kanuni kwa ya kurekebisha bei ya umeme kulingana na mabadiliko ya
bei za mafuta, mfumuko wa bei na mabadiliko ya thamani ya shilingi,
kutaathiri uchumi na maisha ya wananchi.
Mnyika alisema, katika kipindi cha wiki moja tangu
kutangazwa kwa viwango vipya vya umeme, amechukua maoni ya wananchi, na
hakuna aliyeridhika na ongezeko hilo.
“Wameeleza athari wanazozipata na wamependekeza
hatua za kuchukuliwa na kushauri kufanyika maandamano kuishinikiza
Serikali kupunguza ongezeko hilo,” alisema Mnyika.
No comments:
Post a Comment