Rais, ndiyo ataamua kusaini ama kutosaini, huwa kuna mambo mengi yanayoangaliwa
Wadhifa wa Urais wa Tanzania umeendelea kujikuta
njia panda kila unapofika wakati wa kuidhinisha kutekelezwa kwa adhabu
ya kifo kwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na mahakama, na suala hilo
limekuwa gumu kutekelezwa katika awamu zote nne za uongozi.
Hukumu hiyo ni kama haitekelezeki na pengine
mafaili yaliyobeba uamuzi wa mahakama wenye adhabu za vifo, yameendelea
kusubiri kusainiwa tangu enzi za uongozi wa awamu ya kwanza wa Hayati
Mwalimu Julius Nyerere na hata sasa Rais Jakaya Kikwete.
Watangulizi wengine wa Rais Kikwete ni Mzee Ali
Hassan Mwinyi aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Pili na Mzee Benjamin
Mkapa, aliyeongoza Serikali ya Awamu ya Tatu. Wote wanatajwa kwamba
walikuwa wazito kuidhinisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya kuondoa uhai
wa mtu.
Inaaminika kuwa Serikali za awamu ya kwanza na ya
pili zilitekeleza kwa sehemu hukumu hizo, lakini Serikali zilizofuata
hazikuwahi kufanya hivyo. Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu aliyewahi
kunyongwa kwa miaka 18 iliyopita.
Takwimu zilizotolewa na Jeshi la Magereza kwa
gazeti hili zinaonyesha kuwa, hadi Oktoba 15, 2013 kulikuwa na watu 364
katika magereza mbalimbali nchini wanaosubiri kunyongwa, baada ya
kuhukumiwa na Mahakama Kuu ya Tanzania. Taarifa hiyo iliyosainiwa na
Kamishna wa Magezera (CP), Dk Juma Malewa iliweka bayana kuwa hadi
wakati huo, wafungwa 86 walikuwa wamekata rufani za kupinga hukumu
katika Mahakama ya Rufani Tanzania.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Werema anasema hawezi kufahamu kwanini Marais wameshindwa kusaini hukumu
za vifo kwa muda mrefu, kwani suala hilo lina michakato na mambo mengi
ndani yake.
Hata hivyo anaongeza kuwa kutokana na Tanzania
kufuata utaratibu wa maadili (moral) katika utawala wake, inaweza kuwa
chanzo cha ugumu wa utekelezaji wake.
Hukumu ya Kifo hutolewa chini ya Sheria ya
Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Criminal Procedure Act. 1985) ambayo
inasisitiza kuwa utekelezaji wa hukumu hiyo ni muhukumiwa kunyongwa na
siyo vinginevyo.
Kifungu cha 322 cha sheria hiyo kinasema endapo mtu atahukumiwa kwa sheria hiyo, atalazimika kunyongwa mpaka kufa.
Utata wa kusaini
Akifafanua utaratibu wa kufikia hatua ya mwisho
katika utekelezaji wa hukumu hiyo, Jaji Werema anasema kabla ya rais
kusaini, hukumu hiyo hupitia Mahakama Kuu na ile ya Rufani.
“Ikitoka Mahakama Kuu inapelekwa rufaa ndiyo inapitishwa ili
kujithibitishia na kuondoa utata wote unaoweza kuleta matatizo ya hukumu
hiyo, ni lazima kujihakikishia vya kutosha maana mtu akishanyogwa kwa
bahati mbaya huwezi kurejesha uhai wake,” anasema Werema.
Alisema kabla ya rais kusaini katika hatua ya
mwisho ni lazima Rais akutane na kamati ya huruma inayomshauri juu ya
kusaini hukumu hiyo. “Kitakachoshauriwa na kamati hiyo kwa Rais, ndiyo
ataamua kusaini ama kutosaini, huwa kuna mambo mengi yanayoangaliwa,”
alisema.
Wakati kukiwa na utata wa kusaini hukumu za kifo,
Mtaalamu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila
Mkumbo anasema mtu anayesubiria hukumu ya kunyongwa ni sawa na mtu
aliyekufa kiakili.
Anasema kinachobakia ni maumbile ya mwili na roho
tu visivyokuwa na msaada wowote kwake katika mazingira hayo. “Huishi
kipindi kigumu sana kuliko mwanadamu yeyote yule anayeishi hapa duniani,
utashi, hisia na kufikiri kwake hakufanyi kazi,” anasema Dk Ktila.
Dk Kitila anasema kisaikolojia hukumu hiyo
imegundulika kuwa na madhara makubwa kuliko zote duniani, kwani inaweza
kumuathiri kwa muda mrefu hata kama atabahatika kupata msamaha wa
kutohukumiwa hukumu hiyo.
Dk Kitila anasema endapo atasamehewa hukumu hiyo
na kurudi kwenye jamii, atalazimika kuwa chini ya uangalizi kwa kipindi
kirefu mpaka atakaporudia hali yake kama binadamu wa kawaida.
“Anakuwa kama amezaliwa upya, ni vigumu ubongo
kurudia hali yake kwa haraka hivyo ili kuepusha madhara ya
kuchanganyikiwa akili, kichaa au vinginevyo ni lazima apate mtu wa
kuishi naye,” anasema.
Anabainisha kuwa kwa mujibu wa matokeo ya kisaikolojia, asilimia kubwa wanawake ndiyo huathirika zaidi kuliko wanaume.
Msimamo wa Tanzania
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa
zikishinikizwa na mashirika ya kimataifa hasa yale ya utetezi wa haki za
binadamu kufuta sheria hiyo.
Machi 6 mwaka huu Kamishna wa haki za binadamu
katika Umoja wa Mataifa, Navi Pillay alinukuliwa kupitia Idhaa ya
Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) akilaani kuendelea
kwa adhabu hiyo alioyoiita kuwa ni “ukatili dhidi ya binadamu”.
Hata hivyo Jaji Werema anasema hukumu ya kifo
itaendelea kutolewa mpaka pale sheria husika itakapofanyiwa marekebisho
na kwamba Serikali inalazimika kuendelea na adhabu hiyo kutokana na
matukio ya kinyama yanayoendelea katika jamii.
Sheria ya hukumu hiyo bado ipo katika vitabu vya Serikali hivyo mahakama itaendelea na utekelezaji wake, hata wananchi ukiwaambia wapige kura kuifuta hawatakubali kwa sasa kutokana na mauaji ya albino,” anasema Jaji Werema.
Sheria ya hukumu hiyo bado ipo katika vitabu vya Serikali hivyo mahakama itaendelea na utekelezaji wake, hata wananchi ukiwaambia wapige kura kuifuta hawatakubali kwa sasa kutokana na mauaji ya albino,” anasema Jaji Werema.
Werema anaungwa mkono na Mkurugenzi wa Shirika
linalojihusisha na utetezi kwa watu wenye ulemavu wa ngozi ‘Under the
Same Sun’, Vicky Ntetema ambaye anasisitiza kwamba utekelezaji wa
hukumu hiyo ni muhimu hususani kwa wauaji wa albino ili kukomesha
ukatili huo.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na Sheria,
Mathias Chikawe akizungumza kupitia mahojiano ya kipindi cha dakika 45
cha Kituo cha Televisheni cha ITV alisema “hukumu hiyo ni mbaya na
haipaswi kuendelea kwa sasa”.
Chikawe anasema tangu adhabu hiyo imeanza kutumika, haijaonyesha mafanikio yoyote ya kupunguza matukio ya uharifu nchini.
“Imepitwa na wakati na ndiyo maana hata nchi
nyingine zimeshaiacha, binafsi nisingependa tuendelee kuwa nayo na
badala yake tuwe na mbadala wa hukumu kifungo cha jela pekee,” alisema.
Kauli ya Chikawe inaungwa mkono na Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ambacho pia kinapinga adhabu hiyo na
kusisitiza kufutwa kwa sheria husika.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba anasema
adhabu hiyo inatakiwa kupigwa vita hapa nchini na duniani kote kwani
imepitwa na wakati na kwamba ni adhabu inayoharibu taswira ya nchi na
kulifanya taifa lionekane kama eneo la wahalifu wa mauaji (degrading).
“Lakini pia hukumu hiyo ni vigumu kuthibitisha ukweli wa uhalifu
uliotendwa na wahukumiwa hao na ikitolewa kwa makosa huwezi kurudisha
uhai wa mtu aliyenyongwa kwani kumekuwapo na ushahidi huo,”anasema Dk.
Bisimba.
Anaongeza kuwa adhabu hiyo mpaka sasa haina ushahidi wowote wa kuzuia watu wengine kutenda makosa husika.
Ripoti ya Dunia
Aprili 10, mwaka huu shirika la kimataifa la
kutetea haki za binadamu, Amnesty International linalopinga adhabu hiyo
lilitoa ripoti juu ya hukumu hiyo likisema mwaka 2012 kuna baadhi ya
nchi duniani ziliendelea na ukutekelezaji wa hukumu hiyo.
Katika mataifa mbalimbali duniani, hukumu hiyo imekuwa ikipungua na nyingine zikiifuta.
Shirika hilo limeripoti kuwa mwaka jana nchini
Iran takribani watu 314 walinyongwa, wengine 79 nchini Saudi Arabia huku
Marekani ikitekeleza hukumu hiyo kwa majimbo kadhaa ikiwanyonga watu
43, idadi sawa na mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment