Watu 10 wamekufa maji na wengine wanaendelea kutafutwa baada ya boti mbili kupigwa dhoruba na mojawapo kuzama katika maeneo tofauti ya Bahari ya Hindi.
Vifo vya wanne vimetokea mkoani Pwani baada ya
boti waliyokuwa wanasafiria kuzama baharini, na miili ya watu sita
ilipatikana ikiwa miongoni mwa waliozama majini baada ya boti ya Mv
Kilimanjaro II iliyopigwa dhoruba katika mkondo wa Nungwi ikitokea
Bandari ya Mkoani, Pemba kwenda Unguja jana.
Ajali ya Zanzibar
Boti ya Mv Kilimanjaro II iliyokuwa imebeba abiria
380 ilipigwa na upepo mkali na kuleta taharuki kwa wasafiri, huku watu
waliokuwa wamekaa juu wakidaiwa kuteleza na kutumbukia baharini.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini, Riziki Juma alithibitisha kupatikana kwa miili hiyo sita jana jioni.
Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Rashid Seif
Suleiman alisema kundi la wazamiaji lilikuwa limekwenda wamekwenda
katika eneo la ajali hiyo kwa ajili ya uokoaji.
Waziri Seif alisema Kamati ya Ulinzi na Usalama
ilikutana kwa dharura mchana wa jana kujadili tukio hilo, kisha kwenda
eneo la tukio kushirikiana na wataalamu wengine kuwatafuta watu hao.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai
Zanzibar, Yussuf Ilembo alisema boti hiyo iliondoka Pemba asubuhi na
baada ya kufika katika mkondo wa Nungwi ilipigwa wimbi kali na injini
yake kuzima.
Ilembo alisema abiria waliokuwa wamekaa juu ya
boti hiyo waliteleza na kutumbukia baharini wakiwemo watoto na tayari
mpango wa kwenda katika eneo la tukio kuwatafuta kwa kushirikiana na
wananchi umekamilika.
Hata hivyo, alisema uhakiki wa orodha ya abiria
unaendelea ili kupata majina ya watu ambao hawajaonekana na umri wao,
kwa kuwa kuna meli mbili zilisafiri kwa wakati mmoja.
Meli nyingine ilikuwa ni ya mizigo na abiria iitwayo Sea Link ambayo ilitarajiwa kuwasili Bandari ya Malindi jana jioni.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usafiri wa Baharini
(ZMA), Mhandisi Abdi Maalim alisema jana alasiri mabaharia walianza kazi
ya kuwatafuta watu wanaosadikiwa kuzama
“Ni mapema mno kusema lolote, siwezi kusema kama wamekufa au
wako hai, kuna watu wameripotiwa kutoweka baada ya meli hiyo kupata
dhoruba na hawafahamiki mahali walipo,” alisema Mhandisi Abdi.
Ofisa mmoja wa Kampuni ya Azam Marine, alisema
meli hiyo ilibeba abiria 380 na chanzo cha tukio hilo ni dhoruba
iliyoambatana na upepo mkali.
“Wakati chombo kimezimika watu walianza kukata
maboya ya uokozi na mtafaruku wa abiria kutaka kujinusuru ulikuwa
mkubwa, chombo hakikuzama na kiliendelea na safari na kimefika katika
Bandari ya Malindi,” alisema.
Ajali hiyo ni ya kwanza kutokea mwaka huu ambapo
hadi jana alasiri watu walionekana kukaa katika vikundi vikundi na
wengine wakieleza kutokuwaona ndugu zao.
Vifo Pwani
Wakati hayo yakitokea, watu wanne wamekufa maji na
wengine 12 kuokolewa baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Rufiji
kwenda Mafia mkoani Pwani kupinduka na kuzama majini katika Bahari ya
Hindi kutokana na upepo mkali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei
alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa manane kuamkia jana
katika eneo la Dimani delta, Mafia, na boti iliyohusika ni MV Nyaulele
mali ya kikundi cha ushirika cha Unyaulele.
Matei aliwataja waliopoteza maisha katika ajali
hiyo kuwa ni Tano Shaaban, Swaum Muhidin, Hadija Ntayala pamoja na mtoto
mchanga aliyetambulika kwa jina, Najma Yusuf. Watu 12 waliokolewa.
Alisema boti hiyo iliondoka Rufiji saa 11 jioni
ikiongozwa na Hamisi Mwenga, ilipofika eneo la Dimani ilipigwa na
dhoruba kali na kupinduka kisha kuzama
No comments:
Post a Comment