Dar es Salaam. Serikali ya Marekani imeipongeza Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL, kwa kazi nzuri ya kusimamia mawasiliano wakati wa ziara ya Rais Barrack Obama wa nchi hiyo mwanzoni mwa mwezi huu.
TTCL ilipewa dhamana ya kusimamia mawasiliano yote tangu kufika kwa kiongozi huyo hadi kuondoka.
Ofisa Ubalozi wa Marekani nchini, Jeff Shrader
alitoa pongezi hizo alipoongoza ujumbe wa maofisa wa ubalozi huo
kutembelea makao makuu ya TTCL na kuzungumza na viongozi na wafanyakazi
waliohakikisha kuwa sekta ya mawasiliano inakwenda vizuri na kwa
ufanisi.
Ujumbe huo wa Marekani umeahidi kutoa vyeti kwa kutambua mchango wa TTCL na wafanyakazi wake hivi karibuni.
Mkuu wa Masoko na Mauzo wa TTCL, Peter Ngota
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa kampuni hiyo
imepata faraja kubwa kwa kupata mrejesho huo kutoka Serikali ya
Marekani.
“Tumepata faraja…hii inaonyesha uwezo wetu
kitaaluma na ubora wa vifaa tulivyonavyo katika kutoa huduma za
mawasiliano,” alisema.
Alisema kuwa TTCL ilipewa sifa hasa kutokana na
utaalamu, uchapaji kazi na weledi ulioonyeshwa na wafanyakazi wa kampuni
hiyo kwa timu ya Wamarekani waliokuwa wakifanya kazi nayo.
Ngota alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kufanya juhudi kuhakikisha inatoa huduma bora za kimataifa wa mawasiliano nchini.
Kampuni hiyo ya simu inaendesha na kusimamia
mkongo wa taifa wa mawasiliano kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kupitia
Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia.
Mkongo huo unalenga kuwezesha matumizi ya Tehama katika sekta mbalimbali hapa nchini kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mkongo wa taifa unaifanya Tanzania kuwa kitovu cha
mawasiliano kikanda na kimataifa kwa kuunganishwa na mikongo ya
kimataifa iliyopita baharini kama ya Seacom na Eassy ambayo imefikishwa
Dar es Salaam.
Tayari baadhi ya kampuni ya mawasiliano ya nchi jirani yameshaunganishwa kupitia Tanzania.
No comments:
Post a Comment