Blogger Widgets

Monday, 29 July 2013

Jarida la kimataifa lawatuhumu vigogo kuhujumu sera ya dawa


Utafiti uliochapishwa kwenye jarida la kimataifa unaonyesha kuwa mchakato wa mabadiliko ya sera ya uuzaji wa dawa za binadamu nchini, umegubikwa na ufisadi ukihusisha viongozi wa Serikali.
Jarida la Afya la Kimataifa linalochapishiwa nchini Uingereza, limechapisha utafiti huo likisema mabadiliko ya sera hiyo ambayo sasa imebadili mfumo uliokuwapo wa maduka ya dawa baridi za binadamu, kuwa ya dawa muhimu sasa ni janga linalozinyemelea afya za Watanzania.
Kwa mujibu wa jarida hilo hadi upitishwaji wa muswadwa wake bungeni, uliingiliwa na vigogo serikalini pamoja na wafanyabiashara wakubwa kwa malengo ya kujinufaisha.
Jarida hilo linaloitwa BMC Public Health toleo la mwezi huu, limechapisha ripoti hiyo wakati ambapo tayari Serikali imeanza kutekeleza sera hiyo kwa kubadili maduka ya dawa baridi kuwa maduka ya dawa muhimu ambapo yanatatawanywa hadi vijijini na yataruhusiwa kuuza baadhi ya dawa kali za magonjwa makubwa.
Hata hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imetoa msimamo wake ikisema inaichukulia ripoti hiyo kama ni maoni ambayo mtu yeyote anaweza akayatoa, na kwamba hawatarudi nyuma kwa kuwa wanajiamini mchakato ulifuata sheria na taratibu za nchi.
Yaliyomo kwenye ripoti
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa utafiti ulifanyika kati ya mwaka 2011 na 2012, na kubaini kuwa kuundwa kwa sera hiyo, kulizingatia zaidi masilahi binafsi yaliyoandamana na msukumo wa kisiasa na kibinafsi.
Inaeleza sera hiyo haikuzingatia ufanisi wa kitaalamu wa huduma nzuri katika sekta ya afya bali kuweka wigo mpana ambao mtu yeyote mwenye fedha au anayeshawishika na biashara hiyo aweze kuwekeza bila kipingamizi.
Jarida hilo liliipa ripoti hiyo kichwa cha habari: “Mabadiliko ya sera kisekta: Ni kwa ajili ya ufanisi au kuweka wigo mpana ili kila anayevutiwa awekeze? Ni ripoti ya utafiti uliofanyika Tanzania kuhusu mabadiliko ya sera ya uuzaji wa dawa.”
Jambo hilo likatafsiriwa kuwa ni la hatari na ambalo Serikali inapaswa kuingilia kati ili kuepusha janga la kiafya linaloinyemelea jamii.
“Serikali inapaswa kuingilia kati na kupunguza ushawishi wa kisiasa kwa masilahi binafsi kwenye mambo ya kitaaluma,” inashauri sehemu ya taarifa hiyo ikionya:
“Kutoondoa tatizo hilo la udhibiti wa dawa kunaweza kusababisha madhara makubwa ya afya kwa umma.”

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa ilisimamiwa na wataalamu watatu wa afya; Amani Thomas Mori, Eliangiringa Amos Kaale na Peter Risha.
Inaeleza mchakato wa kuunda sera hiyo una kasoro kuanzia uundaji wa kamati, mijadala hadi upitishwaji wa muswada huo bungeni ili kuwa sheria.
Ilielezwa kuwa mfumo mzima ulitawaliwa na ubabe wa uamuzi, ambao wadau ama hawakuhusishwa au walijikuta wanakwepwa kwenye hatua ya kuamua au kufanya majumuisho.
Kwa namna sera hiyo mpya ilivyo, inaelezewa kuwa inaruhusu ushindani wa kibiashara unaoweza kuathiri baadhi ya wawekezaji, hivyo kujenga mazingira ya kuendesha biashara hiyo kwa ujanja jambo ambalo ni hatari kwa watumiaji wa dawa.
Utafiti huo uliofanyika kwa mahojiano na watu mbalimbali unaeleza kuwa baadhi ya wafamasia hawakuridhika na mchakato wa kuunda sera hiyo, kwa sababu ulizingatia maoni na mapendekezo ya watu wengi nje ya fani hiyo ya kifamasia.
Kasoro nyingine inaelezwa baadhi ya watu wasio wa fani hiyo walijipigia kampeni ili wawepo kwenye kamati za kujadili sera na kuna wajumbe wengine nao walishawishiwa ili washiriki bila kuzingatia wako kwenye fani ya dawa au la.
Ripoti hiyo inasema licha ya muswada huo kupata upinzani mkali bungeni, ulipitishwa mabadiliko ya sera ya maduka ya dawa ya mwaka 2011, kifungu cha nne kinachoruhusu usajili wa maeneo na maduka ya dawa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilipewa mamlaka ya kutoa vibali kwa viwanda vya dawa na biashara za jumla, huku Baraza la Famasia ambalo ndilo linasimamia taaluma ya dawa likiachwa katika kusajili biashara za dawa za rejareja.
Mbaya zaidi wakati wa kupitishwa kwa muswada walikwenda baadhi ya watu kuwahamasisha wabunge waukubali ili upite, jambo ambalo watafiti hao wanahoji kulikuwa na sababu gani ya kufanya hivyo kama sera iliandaliwa vizuri.
Kauli ya Serikali
Gazeti hili lilipowasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhusiana na suala hilo, Ofisi ya Habari na Mawasiliano Kwa Umma ilisema kuwa msimamo wa Serikali ni kwamba mchakato wa mabadiliko ya sera ya uuzwaji wa dawa nchini yalizingatia taratibu zote za kuwahusisha wadau.
Msemaji huyo wa Wizara, Nsachris Mwamaja alisema kwenye mchakato huo hakukuwa na ushawishi na kwamba waliotoa utafiti huo walizingatia zaidi maoni yao.

“Sisi tunachukulia ripoti hiyo kama ni maoni waliyotoa wao, kama ambavyo mtu yeyote anaweza akatoa maoni yake kuhusu jambo hilo. Hakuna mtu anayezuiwa,” alisema Mwamaja akisistiza:
“Ninachosema ni msimamo wa Wizara. Mchakato wote uliendeshwa kwa kuzingatia taratibu na sheria za nchi na tunaamini utakuwa na manufaa kwa wananchi.”
Alipoulizwa kuhusu TFDA kuwa msimamizi wa vibali vya uzalishaji dawa na ununuzi wa jumla, badala ya Baraza la Mafamasia ambalo ndilo lenye wataalamu katika fani hiyo alisema:
“Ninachotaka ufahamu ni kwamba hata TFDA wana wataalamu wa dawa. Huo ni utaratibu tu na hakuna jambo linaloharibika.”
Gazeti hili lilipowasiliana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Margaret Sitta alisema jambo hilo ni nyeti na asingependa kusema chochote kwa sababu hajasoma ripoti hiyo kwa undani.
Kamati ya Bunge yanena
Hata hivyo, Sitta alisema ripoti hiyo wakiipata wataijadili kwenye kamati hiyo katika vikao vitakavyoanza mwezi ujao ili kujua hatua ya kuchukua.
Sakata hilo limekuja wakati ambapo hapa nchini imebainika kuwa tayari wafanyabiashara hapa nchini wameuza dawa feki za Kupunguza Makali ya Ukimwi (ARV).
Tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imekiri kwamba Kampuni ya TPI Ltd, iliyopo Arusha iliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) ARV aina ya TT-VIR 30 toleo Na.0C.01.85.
Hali hiyo imezusha mtafaruku kiasi cha kusababisha baadhi ya waathirika kutangaza nia ya kutaka kuishtaki Serikali pamoja na watengenezaji wa dawa hizo, kwa sababu zinaweza zikawa zimewasababishia madhara.
Baraza la Famasia
Msajili wa Bodi ya Wafamasia, Mildred Kinyawa aliwahi kuzungumza na gazeti hili akisema sera ya maduka baridi ilibadilishwa kuwa ya dawa muhimu baada ya Serikali kubaini kuna uuzaji na matumizi holela ya dawa nchini. “Tumegundua hilo na ndiyo maana tumebadilisha mfumo wa maduka ya dawa baridi na kuitwa maduka ya dawa muhimu,” anasema Kinyawa ambaye ni mtaalamu wa dawa.

Anafafanua: “Uuzaji wa dawa ni biashara lakini ni huduma ambayo ni regulated (inayofanyika chini ya usimamizi) na Serikali. Siyo kila mtu anaruhusiwa kuuza dawa.”
Pamoja na msimamo huo, anasema katika miaka ya nyuma kutokana na kuwapo kwa wataalamu wachache wa dawa Serikali ililegeza masharti ya uuzaji wa dawa.
Anasema Serikali iliweka kanuni ya mtu yeyote mwenye akili timamu kuuza dawa baridi, ili mtu yeyote aweze kupata huduma ya kwanza kama vile kutuliza homa au maumivu.
Kulingana na kanuni mpya, alisema maduka ya dawa muhimu yatakuwa nje ya miji wakati yatakayoruhusiwa mijini ni yale yenye wataalamu wa dawa ambayo yatajulikana kwa jina la Famasi.
Sheria mpya ya maduka ya dawa muhimu, anasema yatauza dawa baridi, zikiwepo baadhi moto.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf