Dar es salaam. Waziri
Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye amewatahadharisha Watanzania kuwa makini
na watu wanaotaka madaraka kwa kugawa fedha katika sehemu mbalimbali za
nchi au majimbo akionya wanaweza kujikuta wakimweka madarakani kiongozi
anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Hivi kama mtu anaweza kuhonga sehemu kubwa ya wapigakura katika jimbo
la uchaguzi au hata katika nchi kama nafasi anayosaka ni urais;
tumeshajiuliza hizo fedha nyingi hivyo anapata wapi? Kama anajihusisha
na biashara hizo chafu akipata nafasi hiyo watoto wetu watapona?”
alisema Sumaye jana na kuongeza:
“Haya ni maswali muhimu ya kujiuliza tunapoelekea mwaka kesho kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa na mwaka 2015 wakati wa Uchaguzi Mkuu.”
Alisema hayo mjini Morogoro kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata).
Akizungumza kwa tahadhari alisema haizungumzii Serikali yake iliyoko
madarakani wala mtu yeyote, bali tabia mbaya, Sumaye alisema biashara ya
dawa za kulevya inahusisha fedha nyingi na mitandao mipana ambayo
isipodhibitiwa inaweza kulitumbukiza taifa katika janga.
Alisema Katiba Mpya siyo mwarobaini wa matatizo yanayolikabili taifa
bali, utekelezaji na usimamizi wa sheria na kwamba jambo muhimu ni kuwa
na Serikali itakayosimamia na kutekeleza sheria ili kulinda yale
yaliyoelekezwa katika Katiba.
“Katiba haiwezi kumzuia mwizi kwenda kuiba na sheria haitamzuia mwizi
kwenda kuiba ila itatamka adhabu ya kupewa huyo mwizi. Kwa hiyo ili
vyote hivi viwe na maana ni lazima awepo mtu au chombo cha kumkamata
huyo mwizi na kumfikisha katika mikono ya sheria na chombo hicho ni
Serikali. Kama haiwezi kufanya hiyo kazi kwa ukamilifu tutaishia
kulalamika tu na maonevu na maumivu yataendelea kuumiza jamii.”
“Kwa hiyo hata Katiba iwe nzuri namna gani na ikatamka kuwa rushwa ni
adui wa haki na hata ikatoa adhabu kali sana kwa kosa hilo; kama
tutaweka viongozi madarakani kwa rushwa, hiyo Katiba wala haitatusaidia.
Hivyo Katiba nzuri mpya lazima iambatane na Serikali safi yenye
kusimamia masilahi ya umma. Huwezi kumweka madarakani mwenyekiti wa
kijiji au diwani au mbunge au hata Rais kwa rushwa ya kuwanunua
wapigakura halafu utegemee Katiba Mpya itajibu matatizo ya jamii.”
Azungumzia Mviwata
Sumaye alisema Mtandao huo wa Wakulima Wadogo Tanzania ndiyo unaojua
tatizo la kilimo na shida zao na ndiyo unaotakiwa kuulizwa cha kufanya
ili kilimo chetu kibadilike na mkulima afaidike...
“Kama hatuwahusishi na kuwashirikisha katika sera, mipango na programu
za kilimo, basi tujue kuwa sera, mipango na programu hizo zitashindwa.”
Alisema Tanzania ni nchi ambayo wananchi wake wengi wanategemea kilimo
kwa maisha yao na uchumi wa taifa pia kwa kiasi kikubwa hutegemea sekta
hiyo, lakini bado ni duni na hakijamkomboa mkulima mwenyewe wala uchumi
wa taifa... “Nchi na watu wake bado ni maskini pamoja na kuwa watu
wachapakazi wapo na ardhi kubwa na nzuri yenye rutuba ipo.”
Alisema suala la usindikaji wa mazao lazima lipewe kipaumbele vinginevyo kilimo hakitamwondoa mkulima katika umaskini.
“Kama tutaendelea kuuza mazao ghafi ambayo bei yake katika masoko ya nje
ni duni na haitabiriki, basi wakulima wetu na uchumi wa taifa letu
vitazidi kudidimia. Mazao yaliyoongezwa thamani kwa usindikaji yanapata
bei nzuri na usindikaji nao pia hutoa ajira kwa watu wetu.”
“Kwa mfano, badala ya kuuza pamba ghafi tubadilishe pamba yetu kuwa
nyuzi na vitambaa, katani yetu iwe katika kamba na mazulia, chai na
kahawa ziwe katika paketi za kutumia, matunda yasindikwe katika makopo
na kadhalika. Kwa msaada wa Serikali yetu, Mviwata inaweza kabisa
kufanya kazi hii ama peke yake au kwa kushirikiana na wadau wengine wa
uwekezaji ili kujenga viwanda vya usindikaji mazao. Tusiisubiri Serikali
peke yake haitaweza na tutajichelewesha.”
No comments:
Post a Comment