Msanii wa vichekesho ambaye pia ni mcheza ngoma za makabila mbalimbali wa Tanzania, Small Wangamba ‘Mzee Small’ anavyosimulia mateso yake ya sasa yanayotokana na maradhi ya kiharusi. Bado hajapata matibabu ya maana kutokana na sababu mbalimbali kubwa ikiwa kukosa uwezo kifedha, endelea…
Mzee Samal anasema alihangaika maeneo tofauti kupata tiba na kuna wakati shabiki wake mmoja aliwekeza fedha katika zahanati moja (jina halikumbuki) iliyopo eneo la Kariakoo ambao alikuwa anapata huduma ya kuchuliwa misuli.
“Huyo mtu alisikia naumwa akatafuta namba zangu za
simu kisha akanipigia na kunielekeza sehemu ya kwenda kuchuliwa kwani
nae aliwahi kukumbwa na tatizo kama hilo la kupooza mkono, lakini
alipata nafuu kidogo,” anasema.
Small anasema tiba hiyo ya kuchuliwa viungo ilimpa
nafuu kiasi lakini haikumuwezesha kurejea hali ya kawaida na siku za
karibuni mambo yamebadilika. Hivi sasa sehemu ya mkono inapoungana na
bega inaachana hali ambayo anasema inazidi kumchanganya.
Hali yake kiuchumi
“Mkono unakuwa kama unatengana na bega na mbaya
zaidi nazidi kuishiwa nguvu na sina uwezo walau wa kujikokota na
kutembea,” anasema na kuongeza kuwa hivi sasa hawezi kufanya shughuli
yoyote zaidi ya kula na kulala.
Jambo baya zaidi kwake ni kuwa hana vyanzo vya mapato vya kueleweka.
“Pesa pekee ambazo zinanisaidia kidogo ni za kuuza
maji, haponndiyo napata fedha ya kula na mke wangu Fatma Binti Saidi,”
anasema.
Anaendelea kusimulia kwamba wakati anaugua
amekumbwa na mkasa wa binti yake (jina linahifadhiwa) kukatiza masomo
kutokana na ujauzito.
Ilikuwa mwaka jana wakati binti hiyo akiwa Kidato cha Tatu.
“Watu wamemtia mimba mwanangu wa kike ambaye
alikuwa ni wa tatu, lakini bahati nzuri aliyefanya hivyo ameamua kumuoa,
basi sasa nitafanya nini na mimi hali yangu kama unavyoiona?” Anasema
na kuongeza kuwa hata hivyo hajakata tamaa.
Mahusiano yake na Bi Chau
Small anasema Bi. Chau ni mke wake katika majukwaa ya sanaa tu
si katika maisha halisi. Anasema anaye mke na pia Bi Chau katika siku
za karibuni ameolewa.
“Familia zetu ni marafiki, mke wangu anafahamiana vizuri na Bi Chau,” anasema.
“Yule ni mke wangu kikazi na sijawahi kuwa na
uhusiano nae. Mashahidi wa jambo hili ni watu ambao huwa tunasafiri wote
kikazi kuanzia wale wa mbio za Mwenge hadi makampuni ya sabuni na
bidhaa zingine ambao huwa wanatutumia katika promosheni.”
Anasema msanii huyo nguli kuwa yeye na Bi Chau
watu wengi walidhani ni mke na mume na hata wakisafiri kuna watu ambao
wamekuwa wakiwachukulia chumba kimoja wakijua ni lazima watalala wote
lakini haikuwahi kutokea kitu kama hicho.
“Walikuwa wanatuchukulia chumba kimoja lakini
ikawa haiwezekani lazima tupate kingine na taratibu walituelewa hadi
hivi sasa,” anasema na kuongeza kuwa wengi wanaamini kuwa ni mkewe au
wana mahusiano ya kimapenzi dhana ambayo sio sahihi.
Anasema mke wake na Bi Chau wanaitana mtu na dada
yake na anabainisha kuwa kama angekuwa na uhusiano wa kimapenzi na
mwanamke huyo, wasingefika mbali na hata ushirikiano wao kikazi
ungevurugika.
“Tena vurugu hizo zingehamia katika familia zetu,” anasema.
“Nashukuru Bi Chau tunaheshimiana sana na huwa anafika kunijulia hali na mwanamke huyo amekuwa na msaada mkubwa kwangu.
“Tunashirikiana katika masuala mbalimbali ya kimaisha na amekuwa akiniheshimu.”
Anasema kwa kuwa na Bi Chau kunafanya wanawake
wengine wasimsogelee wanapokuwa safarini kwa kuamini kuwa yupo na mkewe
wake hali ambayo anasema ni kama afadhari hususani kipindi hiki cha
maradhi hususan Ukimwi.
“Wenzetu wengi hawapo tena kutokana na vifo
ambavyo vinahusishwa na Ukimwi na wengi wao nyendo zao tulikuwa wote
tunaziona na kutufanya tupate simulizi katika gari wakati wa kurudi au
kutoka sehemu moja kwenda nyingine” anasema.
Alipotokea
Alipotokea
Wangamba anasema alizaliwa kati ya mwaka 1952 au 1953 katika
Kijiji cha Njia nne Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi na kwa bahati mbaya
hakupata nafasi kusoma elimu yoyote.
Baada ya kufanya kazi tofauti kunako miaka ya
sabini, alijiunga na Kundi la Agizo lililokuwa na maskani yake Mtaa wa
Arusha Ilala.
Kama umeguswa na unataka kumsaidia Mzee Small, wasiliana nasi kwa simu 0718826468
No comments:
Post a Comment