Louis Paul Mfede alikuwa gwiji wa soka nchini Cameroon , alikuwa shujaa ndani ya uwanja na balozi mzuri nje ya uwanja .
Fefe aka Bolingo alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichoipeleka Cameroon kwenye robo fainali ya kombe la dunia mwaka 1990 na kuweka historia ambayo haijafikiwa mpaka hii leo .
Lakini tarehe 10 mwezi uliopita alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 52 kutokana na maradhi ya mapafu kwenye hospitali moja huko Yaounde na sababu za kifo chake zaidi ya maradhi ilikuwa ukweli kuwa alishindwa kugharamikia dawa na matibabu ya maradhi yake .
Jeneza la Mfede wakati akienda kuzikwa |
Ulikuwa ni mwisho wa kuhuzunisha kwa maisha ya mtu ambaye aliifanyia Cameroon makubwa sambamba na watu kama Roger Milla , Thomas Nkono, Libih Thomas, Maboang Kessack na wengineo hasa miaka 23 iliyopita nchini Italia kwenye kombe la dunia.
Mafanikio ya Mfede na wenzie yaliwafanya Wacameroon wote kujawa na matumaini na kumbukumbu ya wengi waliomshuhudia akiwapiga chenga wachezaji watatu pamoja na tabia yake ya kuwafanya wenzie wajiamini hadi kuwafunga Argentina 1-0 kwenye mchezo wa kwanza wa kombe la dunia mwaka 90 haitafutika vichwani mwa watu wa Cameroon.
Pamoja na yote haya, viongozi wa chama cha soka cha Cameroon na wizara ya michezo waliotaarifiwa na mkewe Paul juu ya hali ya mumewe hawakufanya chochote .
Mtoto wa Mfede anayeitwa Frederick alifichua kuwa msaada pekee ulitoka kwa Roger Milla ambaye alisaidia kulipa gharama za hospitali wakati familia yake ikiwa imekosa msaada. Siku ya mazishi yake, waziri wa michezo Adam Garoua alimtunuku Mfede medali ya heshima kwa mchango wake kwa taifa la Cameroon huku akiweka shada la maua kwenye kaburi lake kwenye kijiji cha Nkol-kosse huko Lekie kwenye jimbo la kati la Cameroon lakini watu wamehoji kwanini Mfede hakupewa huduma wakati akiwa mgonjwa huduma ambayo ni muhimu kuliko hata nishani isiyo na maana wakati huu akiwa amekufa.
Kikosi cha Cameroon kilichofanya maajabu 1990 - Mfede aliyechuchuma wa kwanza mkono wa kulia. |
Thomas Nkono alilalamika, "Kwanini watu ambao tuliwahi kuitwa mabalozi leo hii maisha yetu yanafifia kwa aibu na shida . Ninapoona watu wachache ambao ni mashabiki halisi wa soka wakiwa wamelizunguka jeneza la Mfede nasikititka huku nikisema kuwa hii ni mbaya kwa shujaa wa taifa . Inauma kuona akiondoka duniani kama mtu ambaye hakuna anayemfahamu."
Thomas Nkono ambaye anaaminika kuwa kipa bora wa afrika kwa miaka yote aliongeza kuwa, "Watu ambao walijitoa kwa ajili ya soka wanapaswa kutambuliwa na serikali lakini kumuona Mfede anakufa mtaani namna hii inaniuma sana."
Beki wa zamani Benjamin Massing alisema, "Ni huruma sana kumuona mwenzetu amekufa kwa namna kama hii akiwa ametelekezwa na kauchwa mwenyewe."
Mfede akimtuliza Rigobert Song baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye moja ya mchezo wa kombe la dunia 1990 |
Pamoja na kukosekana kwa huduma na mazishi ya kitaifa kwa Mfede au the magic foot yaani guu la kushoto la kichawi kama alivyokuwa akifahamika enzi za miaka ya themanini jina ambalo alipewa na mchezaji bora wa afrika mwaka 1980 Jean Manga Onguene atakumbukwa na wenzie kama mtu mwenye furaha na aliwaunganisha wachezaji wenzie .
"Kesi ya Mfede ni kesi ambayo inawakuta wachezaji wengi wa zamani wa Cameroon hasa wale wa miaka ya tisini .
Sisi wanasoka hakuna anayetujali," anasema mchezaji wa zamani Libih , anaongeza, "Mbaya zaidi hakuna umoja miongoni mwetu kwa kuwa sio serikali pekee ambayo itafanya kila kitu . Ni kweli kuwa tunajitolea maisha yetu kupigania bendera ya taifa letu lakini baadaye tunakuwa watu wa kawaida lazima tukutane na maisha ya baada ya soka.
Inatia huruma kuwa wachezaji wakubwa hawaweki misingi yoyote ya kulinda maslahi yetu . Tunakimbilia maisha mabaya ambayo hayafahamiki na ndio maana tunapambana kwenye televisheni kwa kuwa tunataka kurudi mahala fulani, inatia huruma na maisha ni magumu, tunapigana sisi kwa sisi badala ya kujenga."
Mchezaji mwingine Youmbi Ayakan ambaye alicheza kwenye miaka ya tisini aliungana na Libih ambapo alisema kuwa kuna haja ya wachezaji kujipanga na kuweka hali zao za baadaye kuwa nzuri zaidi. "Ni muhimu kwa wale wanaocheza sasa na hata wale waliostaafu, wachezaji wengi wa sasa hata hawafahamu kaka zao waliocheza kabla yao, sisi ndio tuliwafanya waote kufikia mahali hapa walipo leo hii lakini hakuna anayefanya kitu kwa ajili yetu."
Suluhisho la tatizo hili kwa mujibu wa Libih ni kwa wachezaji waliostaafu kutumia uwezo wao kuwasaidia wachezaji wachanga ama kuwa viongozi wa chama cha soka na tawala nyingine za michezo na hata kuingia kwenye ukocha
"Kuna haja ya chama cha soka kulinda maslahi ya wachezaji kwa kuwa sisi wote tumefanya makubwa kwa niaba ya taifa na kuna haja ya wanamichezo wote kwa pamoja kulindwa."
No comments:
Post a Comment