
Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema kauli zinazotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo dhidi yake kuhusu uwekezaji katika sekta ya gesi nchini hazina ukweli wowote.
Mengi jana alitoa taarifa yake katika vyombo vya
habari na kueleza kuwa waziri huyo ni mtu mwenye hulka ya kusema uongo,
kauli ambayo ameitoa ikiwa zimepita siku mbili tangu waziri huyo kudai
kuwa Mengi anamiliki vitalu vingi vya gesi, kwamba anataka kupewa
upendeleo wa kupewa wakati hawezi kuviendeleza.
Huku akitaja mambo kadhaa ya uongo kuhusu waziri
huyo, Mengi alisema,“Sikutegemea kama Muhongo ataendeleza vita dhidi
yangu. Mtu huyu ana hulka ya kusema uongo, amewahi kuwaahidi Watanzania
kuwa hakutakuwa na mgawo wa umeme, lakini upo mpaka sasa.”
Alisema hamiliki migodi mingi ya madini kama
inavyodaiwa “Ukweli ni kwamba, mimi namiliki kwa ubia na Watanzania
wenzangu mgodi mmoja wa uchimbaji wa madini ya Tanzanite wenye eneo
lisilofikia hata kilomita moja ya mraba.”
Alifafanua, “Muhongo anafahamu kwamba kuna aina sita za leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini.
Lakini kwa makusudi kabisa anafananisha leseni ya
Mtanzania anayetafuta au kuchimba kokoto na leseni ya mwekezaji wa
kigeni anayetafuta au kuchimba urani au dhahabu. Kweli unaweza
kufananisha kokoto na dhahabu.”
Alisema kuwa licha ya kuwa utafutaji wa madini
ndiyo husababisha watu kugundua eneo lenye madini, kuanzia Julai mwaka
jana Waziri Muhongo amepandisha tozo za vitalu kwa asilimia kati ya 100
na 500 na kusababisha Watanzania wengi kurudisha leseni zao.
No comments:
Post a Comment