Blogger Widgets

Sunday, 22 December 2013

Mauaji Sudan Kusini UN wakaa kikao cha dharura

 
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limefanya kikao cha dharura kuhusu Sudan Kusini, baada ya wanajeshi wa Umoja huo kuuawa katika ghasi nchini humo.
Wanajeshi watatu wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India, waliuawa nchini Sudan Kusini katika shambulio lililotokea kwenye kambi ya Umoja wa Mataifa.
Mauaji hayo yalifanyika wakati ambapo mapigano kati ya vikosi vya waasi na majeshi ya Serikali yakiongezeka, hali inayozusha wasiwasi wa nchi hiyo kuingia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Balozi wa India katika Umoja wa Mataifa, Asoke Mukerji alisema wanajeshi hao wameuawa katika shambulio lililofanywa na vijana wa kabila la Nuer kwenye kambi ya Akobo, jimbo la Jonglei.
Wakati huohuo, Marekani imepeleka wanajeshi 45 Sudan Kusini ili kuwalinda raia wake na mali zao.
Wanajeshi hao watabakia Sudan Kusini hadi usalama utakapoimarika. Rais wa Marekani, Barack Obama alitoa wito mapigano hayo kusitishwa mara moja, akionya nchi hiyo inaweza ikatumbukia katika vita.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq alisema “Mapigano yametokea na hatujathibitisha hali ilivyo’’
Alisema  Tume ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS itaondoa wafanyakazi wake wasiyo wa kijeshi kutoka Akobo.
Habari nyingine zinasema, wafanyakazi wenyeji 14 wa kampuni ya mafuta nchini Sudan Kusini wameuawa katika mapigano kati ya makundi ya wapiganaji kutoka makabila ya wa Dinka na wa Nuer.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametaka kufanyike mazungumzo ya kisiasa ili kulinusuru taifa hilo ambalo bado ni changa.
Katika taarifa yake, kiongozi huyo wa Umoja wa Mataifa alisema hatma ya taifa hilo changa ipo katika mikono ya uongozi wake wa sasa ambao unapaswa kufanya kila liwezekanalo kudhibiti machafuko ambayo yatakuwa usaliti mkubwa kwa zile jitihada za muda mrefu za kutafuta uhuru wake.
Alisema viongozi wa nchi hiyo wanatakiwa kudhihirisha uhuru wao waliopata kwa kuutafuta kwa muda mrefu ambapo walifanikiwa.
Raia wa nchi hiyo mpaka sasa wamekosa amani kwani wanahaha kutafuta pa kukimbilia huku wakitafuta msaada kutoka nchi jirani.

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf