
Hakuna ubishi kwamba kwa siasa za Tanzania, Chadema ndiyo chama kikubwa cha upinzani kinachokinyima usingizi chama tawala CCM.
Vipo vyama zaidi ya 20 vyenye usajili wa kudumu
tangu uliporejeshwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Katika uchaguzi
mkuu wa kwanza chini ya mfumo huo mwaka 1995, NNCR Mageuzi kilikuwa
chama tishiyo, hasa pale Augustine Mrema aliyekuwa Waziri wa Mambo ya
Ndani machachari, kujiunga nacho na kugombea urais.
Hata hivyo, ilikuwa kama mbio za sakafuni tu kwani
haikufika mwaka 2000, chama kilishasambaratika huku yeye mwenyewe
akikimbilia TLP.
Zamu ikahamia Chama cha Wananchi (CUF) hata hivyo,
nacho hakikuvuma kwa muda mrefu, hasa kutokana na kupigwa propaganda za
udini. Isitoshe, nguvu ya chama hicho inajionyesha zaidi upande wa
Zanzibar.
Hauchi hauchi sasa kumekucha Chadema. Chama hicho kimekuwa na mwenendo mzuri tangu kilipoanzishwa mwaka 1993.
Mwaka 1995 chini ya uenyekiti wa Edwin Mtei,
Chadema kilipata wabunge watatu, mwaka 2000 chini ya uenyekiti wa Bob
Makani (Marehemu), chama hicho kilipata wabunge wanne wa kuchaguliwa na
mmoja wa viti maalumu.
Mwaka 2005 chini uenyekiti wa Freeman Mbowe, chama hicho kilipata wabunge watano na wengine sita wa viti maalumu.
Mwaka 2010 chini ya uongozi wa Mbowe tena, chama
hicho kimezidi kuimarika kwa kupata wabunge 23 na wa nyongeza 25 na
kufanya idadi kuwa 48, kabla ya kupata mwingine mwaka jana na kufanya
sasa wawe 49.
Hii ni dalili kwamba wananchi wengi wanakiamini
chama hiki kwamba kitawafikisha kwenye mageuzi ya kweli. Kutokana na
imani hiyo ilivyokuwa kubwa, kungekuwa na uwezekano wa chama hicho hata
kushika madaraka kama vyombo vya usimamizi wa uchaguzi vingekuwa huru.
Kwa hali ilivyo sasa ni vigumu kwa chama cha upinzani kushika madaraka.
Kwanza Tume ya Taifa ya Uchaguzi haiko huru, ni
tume iliyoundwa na rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala CCM.
Sasa kama mshindani wako ndiye anakuwa mwamuzi wa mchezo, unatarajia
nini?
Isitoshe, tume hiyo haina ofisi mikoani, hivyo
huishia kutumia wateule wa Rais na Waziri Mkuu kama vile Wakurugenzi wa
Manispaa na halmashauri kusimamia uchaguzi. Watendaji hao hupokea
maelekezo kutoka juu na wanapaswa kuyatii, hivyo haishangazi kuwa
wanaweza kupewa maelekezo ya kuhakikisha chama tawala kinashinda na
wakayatekeleza.
Mbali na hao, wapo pia wakuu wa majeshi hasa Jeshi la Polisi,
ambao husimamia usalama nyakati za chaguzi. Wanaweza kuathiri uchaguzi
kwa kufuata maelekezo ya aliyewateua ambaye pia ni mgombea.
Kwa kifupi, chaguzi za Tanzania huwa hazina uhalisia katika ushindani kwani watawala wanahofia kupoteza madaraka yao.
Hata hivyo, kuona Chadema kinapata wabunge kilichopata ni faraja kwamba walau sauti ya wananchi inasikilizwa.
Pamoja na hayo, vyama vya upinzani navyo vina madudu mengi mno yanayovirudisha nyuma.
Kuna mengi yanasemwa ndani ya Chadema, ambayo
hayawezi kupita tu bila kujadiliwa. Mengine yalisemwa na aliyekuwa Naibu
Katibu Mkuu, Zitto Kabwe na kambi yake na huenda ndiyo yamesababisha
asimamishwe.
Kwa mfano suala la matumizi ya fedha za chama ni
suala lililozua malalamiko mengi. Achilia mbali suala la hesabu za chama
hicho kukaguliwa, inaonyesha hakuna uwazi wa kutosha katika map
Kama nilivyosema awali, kwamba kwa sasa chama
hicho kimeshajipambanua kama chama chenye upinzania mkali, hivyo
kinapaswa kuwa makini zaidi kwenye hesabu zake, siyo kusubiri hadi
Mkaguzi na Mdhibiti wa Serikali (CAG) aje akague.
Jambo la pili ni madai ya aliyekuwa Mwenyekiti wa
chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba kuhusu kubadilishwa kwa
vipengele vya Katiba.
Katika taarifa yake Mwigamba, amemwomba msajili
kutoa mwongozo kuhusu kipengele cha Katiba ya Chadema ya mwaka 2004
kipengele 5.3.2 (c) kinachogusia ukomo wa uongozi kubadilishwa kinyume
na utaratibu katika mabadiliko ya mwaka 2006.
Kelele za ukabila na upendeleo nazo ni za muda
mrefu, yote siyo mambo ya kupuuza, bali ni kuyafanyia kazi ili
kuendeleza imani ya wananchi kwa chama hicho.
Chadema kwa sasa inapaswa kujitathmini, badala ya
kulaumu tu CCM au wasaliti wa chama hicho. Maana mtu ukifuatwa sana na
inzi inabidi pia ujiangalie, usije ukawa unatembea na uchafu.
Ajidhaniaye kuwa amesimama, aangalie asianguke kwa kuwa lisemwalo lipo,
kama halipo basi laja.
No comments:
Post a Comment