
Habari kwamba Kamati nane za Bunge zinatarajiwa kwenda nje ya nchi kufanya kile kinachoitwa ziara za kikazi na mafunzo, zimeibua hisia miongoni mwa wananchi kwamba ziara hizo hazina tija kwa taifa, isipokuwa ni mkakati uliosukwa na wabunge kwa lengo la kujinufaisha kifedha.
Badala ya kupeleka wataalamu wetu nje ya nchi kwa
ziara za mafunzo, wanapelekwa wanasiasa ambao mchango wao katika kuinua
uchumi na kuimarisha huduma za jamii ni kama sifuri.
Pamoja na kwamba ziara hizo zinazoitwa za mafunzo na kikazi zimekuwa zikitumia mabilioni ya fedha za walipakodi.
Kamati hizo zimekuwa hazifanyi majumuisho ya ziara
hizo au kuonyesha jinsi gani wabunge na wananchi kwa jumla
walivyonufaika au watakavyonufaika na ziara hizo.
Hayo ni kama mashindano ya Kamati hizo, kuona ipi
inafanya ziara nyingi zaidi kuliko nyingine au ipi inayowapeleka wajumbe
wake katika nchi zenye ‘neema’ zaidi kuliko nyingine. Tunasita kusema
kwamba ziara hizo ni za kitalii na matanuzi zaidi kuliko kitu kingine,
kwa maana ya kutoleta tija kwa Bunge wala taifa.
Hivi sasa Kamati ya Maendeleo ya Jamii yenye
wajumbe 21 iko Malaysia na baadaye itakwenda India eti kwa ziara ya
mafunzo ya hifadhi na huduma za jamii.
Kamati ya Miundombinu yenye wajumbe 20 nayo
ilitazamiwa kwenda Malaysia juzi eti kujifunza maendeleo ya miundombinu,
wakati Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa yenye wajumbe 18 itafanya
ziara nchini Uingereza na Ireland eti kujifunza masuala ya serikali za
mitaa.
Kamati ya Hesabu za Serikali yenye wajumbe 18 iko
Dubai kwenye mkutano wa kamati zinazosimamia hesabu za serikali na
inatazamiwa kwenda Uingereza baada ya mkutano huo wa Dubai.
Wakati Kamati inayoshughulikia masuala ya Ukimwi
yenye wajumbe 22 ikienda Afrika Kusini, Kamati ya Uchumi, Viwanda na
Biashara ambayo pia ina wajumbe 22 itaondoka wakati wowote, kwani Ofisi
ya Bunge inasema bado ratiba yake haijakamilika.
Hata hivyo, Kamati za Katiba, Utawala na Sheria;
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa; Kilimo, Mifugo, Maji, Ardhi na
nyingine tayari zimefanya ziara kama hizo katika nchi mbalimbali.
Siyo lazima kuwa na shahada ya chuo kikuu kuweza
kugundua kwamba ziara hizo zinazoitwa za mafunzo na kikazi ni ziara za
ujanja ujanja na ulaji wa kupindukia.
Kama zingekuwa za manufaa, tungeona taswira ya
Bunge ikibadilika, kwa maana ya wabunge kutanguliza masilahi ya taifa;
kupigania ustawi wa wanyonge; kuzingatia maadili ya uongozi; kuacha
siasa za majitaka na kuheshimu kanuni zinazoongoza siasa za ushindani
nje na ndani ya Bunge.
Tungeona wakiweka msisitizo katika masuala ya ajira za vijana na
kufuta umaskini, badala ya madai yao binafsi ya nyongeza za mishahara
na posho.
Tungeona mabadiliko ya kweli katika hulka za
wabunge kutokana na kauli zao na matendo yao. Tungeona wabunge
wakihudhuria vikao vya Bunge na kuchambua miswada kwa umakini mkubwa,
badala ya kuvikacha au kuhudhuria lakini wakapiga porojo au kuchapa
usingizi wa pono.
Tungeona wakitoa hoja zenye kuwaleta wananchi
pamoja badala ya kuwagawa. Ndiyo maana tunasema mabilioni ya fedha ya
kuwapeleka wabunge katika kile kinachoitwa ziara za mafunzo na kikazi ni
matumizi mabaya ya fedha za walipakodi.
No comments:
Post a Comment