By EDO KUMWEMBE,MWANASPOTI
WAKATI mwingine kila shujaa anaishi na hukumu yake ya maisha yote aliyoishi. Yupo askari aliyerusha risasi ya mwisho kwa dikteta fulani. Daima Dunia itamkumbuka kwa risasi hiyo kwa maisha yake yote.
Wengine wanaonekana wazembe na wanakumbukwa kwa
uzembe wao kwa maisha yao yote duniani. Kipa wa Brazil katika fainali za
Kombe la Dunia mwaka 1950 zilizofanyika Brazil, Moacir Barbosa, mpaka
sasa hajasamehewa na wananchi wa Brazil.
Anatajwa kufungisha bao la pili la Uruguay katika
mechi ya fainali. Mpaka sasa Wabrazili hawajamsamehe. Hata kaburi lake
lililopo Campinas, Brazil nalo halijasamehewa. Majuzi kipa wa zamani wa
Brazil, Dida, alikuwa anamuombea msamaha. Sioni kama watamsikiliza.
Lakini wengine ni mashujaa na wanakumbukwa kwa ushujaa wao kwa maisha
yao yote.
Zinedine Zidane wa Kombe la Dunia mwaka 1998
atakumbuka na Wafaransa kwa maisha yake yote. Ni kama Pele wa 1958 au
Diego Maradona wa Mexico ya mwaka 1986.
Ni kama Cristiano Ronaldo wa Jumanne usiku jijini
Stockholm kule Sweden atakavyokumbukwa maisha yake yote na Wareno. Hata
kaburi lake litakumbukwa kwa miaka mingi ijayo. Popote atakapolazwa, iwe
Santo Antonio au Funchal pale Madeira.
Wareno walihitaji sana kwenda Brazil. Nililiandika
hili wiki chache kabla ya mechi. Unajua kwa nini? Hawa ndiyo watoto zao
wakubwa miongoni mwa mataifa waliyoyatawala. Achana na Angola, Cape
Verde na Msumbiji, Brazil ndiyo taifa kubwa zaidi lililotawaliwa na
Ureno.
Kwa bahati mbaya, Ureno na makoloni yao yote
kasoro Brazil hawajawahi kuandaa Kombe la Dunia. Wakati Brazil
ilipoandaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1950 na Barbosa
kufanya kosa lisilosameheka, Ureno haikushiriki mashindano hayo.
Jumanne usiku, ilikuwa fursa yao ya mwisho kwenda
Kombe la Dunia katika koloni lao. Nani anajua ni lini Kombe la Dunia
litarudia tena Brazil? Hasa ukizingatia nafasi ya mwisho waliipata miaka
63 iliyopita. Walihitaji timu yao iende. Lakini zaidi walimhitaji
Ronaldo kuwapeleka katika fukwe za Copacabana pengine kuliko mchezaji
yeyote yule katika kikosi chao. Shujaa hapimwi katika klabu. Anapimwa
katika timu ya taifa.
Ushujaa wa klabu ni rahisi kuupata kwa sababu
unautumikia mshahara wako. Ushujaa wa timu ya taifa ni mgumu kwa sababu
hauna malipo. Unaitumikia damu yako na ya watu wako. Unaitumikia bendera
yako, unaitumikia historia yako, unaitumikia nchi yako.
Kwa Wareno, kama ilivyo duniani kote, Ronaldo
anaonekana kijana mwenye kipaji, mpenda magari mazuri, malaya,
anayekesha katika kioo, tajiri. Lakini ushujaa kwa watu wake ulikuwa
mbali.
Jumanne usiku ameibadili historia yake. Kaburi
lake halitachapwa viboko kama lile la Barbosa. Ameliingiza jina lake
katika historia kama Zidane alipofanya usiku ule wa Julai 12, 1998
katika Uwanja wa Stade de France jijini Paris, Ufaransa.
Ameliingiza jina lake katika historia kama vile
Maradona alivyofanya Juni 29, 1986 katika Uwanja wa Azteca. Ni kama Pele
alivyofanya katika Uwanja wa Rasunda jijini Stockholm Juni 29, 1958.
Ronaldo alihitajika afanye alichofanya usiku ule wa Jumanne
jijini Stockholm. Kweli hakuwaangusha. Alifunga la kwanza, akafunga la
pili, akafunga la tatu. Aliwaweka Waswedeni mfukoni kwake. Akawafanya
alichojisikia.
Kombe la Dunia bado. Sioni kama Ureno watafanya
vizuri licha ya kuwa na Ronaldo. Lakini katika historia yao, Wareno
walihitaji jeshi la mtu mmoja kuwafikisha fukwe za Copacabana. Ndani ya
siku nne, Ronaldo alifunga mabao manne ya kuwapeleka Copacabana.
Ronaldo na Messi hawaingizwi katika kundi la Pele,
Maradona, Ronaldo de Lima, Gerd Muller na Zidane kwa sababu heshima yao
ndani ya taifa iko chini. Messi anampita Maradona katika idadi ya
mabao, lakini sasa anahitaji kuwa jeshi la mtu mmoja ndani ya Brazil
miezi saba ijayo.
Kama Ronaldo anaweza kufanya kitu zaidi katika
fainali za Maracana msimu ujao atakuwa zaidi ya Maradona. Kikosi chake
hakina mastaa wa kumwezesha kufanya jambo la maana Brazil. Amezungukwa
na mastaa wa kawaida.
Ni kama ilivyokuwa kwa Maradona. Lakini Maradona
alitoa maajabu. Hata hivyo hadi alipofika inatosha kumwingiza Ronaldo
katika kundi la Luis Figo na Eusebio ambao katika mitaa ya Lisbon,
Ureno wanaonekana kama miungu watu.
Ronaldo alikuwa anaonekana kama mvaa hereni mwenye
maringo anayetisha Santiago Bernabeu. Amefanikiwa kuvuka mtihani huu
akiwa na kitambaa chao begani. Kwa lolote atakalofanya ataonekana
shujaa. Hata kama akifanya ujinga, kaburi lake litasamehewa.
Ni kama unavyomwona Maradona. Anavuta bangi,
anakula unga, anafanya vurugu za kila aina, lakini Waargentina
walishamsamehe kwa mambo aliyowafanyia. Hata akifa, kaburi lake
lilishasamehewa kutokana na usiku ule wa Azteca Mexico.
Ni kama usiku wa Stockholm ulivyosababisha Wareno
wamsamehe Ronaldo. Kwa lolote baya litakalotokea mbele, tayari
ameshaingia katika vitabu vyao.
No comments:
Post a Comment