Si urithi wa mali, isipokuwa ni mapenzi kwa binadamu wenzake na
hekima ambavyo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
ameviacha katika vitabu, maandiko mbalimbali na kwa familia yake, tangu
afariki dunia miaka 14 iliyopita.
Unapofika katika nyumba yake iliyopo jijini Dar es
Salaam maeneo ya Msasani maarufu kwa Mwalimu Nyerere,
kinachoyatofautisha maisha ndani ya nyumba hiyo na zile za Magomeni na
Ilala ni mazingira nadhifu.
Wenyeji ndani ya nyumba hii kwa mwonekano na
mazungumzo hawana tofauti na Watanzania wa kawaida, hawana majivuno na
wanamkaribisha mgeni kama ndugu au jamaa waliyemfahamu miaka mingi.
Pamoja na kuwa nyumba ni kubwa na wenyeji ni
wengi, lakini kwenye maegesho ya magari lipo gari moja tu. Mwonekano wa
nje wa nyumba hii unaweza kukufanya ufikiri ndani kuna magari zaidi ya
matatu tena ya kifahari.
Wanafamilia ni wakarimu sana, kwa kawaida
ungetarajia kusikia wenyeji wakitumia maneno kama “Yes, No” na maneno
mengine ya Kiingereza kwa kuwa hiki ni kitambulisho cha vijana waliopata
elimu angalau ya sekondari, lakini hapa ni tofauti, wote wanazungumza
Kiswahili na bahati mbaya wakichanganya huwa ni lugha ya Kizanaki.
Wajukuu wa Baba wa Taifa, Moringe Magige na Julius
Makongoro wanasema huu ndiyo urithi ambao Baba wa Taifa aliwaachia
ndugu zake wakisema kuwa walilelewa kuamini kuwa mali siyo kitu kuliko
utu na ndivyo walivyo.
Maisha ya Mwalimu Nyerere kama babu
Wengi tunafahamu historia ya Baba wa Taifa hasa
katika majukumu yake ya uongozi wa Tanzania na ukombozi wa bara la
Afrika, lakini Moringe na Julius wanaturudisha nyumbani wakisimulia
walivyomfahamu babu yao.
Moringe anasimulia akisema; “Kwanza mimi
sikufahamu kwa jinsi gani babu alikuwa mtu muhimu katika nchi hii na
bara la Afrika kwa ujumla, nilijua baada ya kufariki dunia na kuanza
kusoma historia yake na kugundua vitu vingi alivyofanya,”
“Sikuiona tofauti yake na mababu wengine kwani
shuleni nilisikia watu wakisimulia jinsi walivyoishi na babu zao na
sikuona tofauti na babu yangu,” anasema Moringe.
Anasema Mwalimu Nyerere aliwapenda wajukuu zake,
alipenda kufanya shughuli za shamba akiwa na wajukuu zake, hakutaka hata
mmoja azembee kwenda shambani.
“Babu aliipenda familia yake, tumeishi na ndugu
wengi kwa sababu hakutaka kukaa mbali na ndugu zake na kila mmoja
alihakikisha anapata wasaa wa kukaa naye na kuzungumza naye, mfano
alikuwa na utaratibu wa kula chakula cha jioni na sisi wajukuu zake,”
anasema Moringe
Aidha anasema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa akiwahimiza kuongeza juhudi shuleni hasa katika masomo ya Kiingereza na Hisabati.
“Babu alikuwa akifuatilia maendeleo yetu shuleni,
kila mwisho wa muhula alikagua matokeo ya kila mmoja wetu na alikuwa
akisisitiza zaidi masomo ya Kiingereza na Hesabu akisema hayo ndiyo ya
msingi,” anasema Moringe.
Alikuwa anapenda kupiga makonzi
Kila mtu anakumbuka adhabu gani alikuwa anapewa na
bibi au babu yake pale anapokosea, lakini Julius anatuambia kuwa
Mwalimu Nyerere alikuwa akiwapiga makonzi wajukuu zake pale wanapokosea.
Julius anasema adhabu kubwa waliyokuwa wakipewa na
babu yao ni kupigwa makonzi hata hivyo utaokoka tu kwa juhudi zako za
kutoka mbio kwani ukisimama anaendelea kukupiga. “Babu alikuwa na tabia
ya kutupiga makonzi hasa ukiwa mtundu au ukimpitia karibu wakati
anacheza bao lazima atakupiga japo konzi moja,” anasema.
Pia anasema kamwe hatasahau siku moja alipomuomba
babu yake akaangalie mkanda wa video mchana;” Nilimwambia babu tunaomba
kuangalia mkanda kwa sababu Tv ilikuwa inakaa Maktaba, alinikubalia na
kuniambia nenda ukawaite na wenzako unaotaka kuangalia nao. Basi
nikaenda kuwaita tulivyofika alitufungia na kuanza kutupiga makonzi ,”
anasema Julius.
Aidha anasema babu yao aliwapangia muda maalumu wa
kuangalia televisheni pia aliwachagulia mikanda ya kutazama kwa kuwa
alipenda wawe na maadili mema.
Vituko,utani wa babu na wajukuu zake
Pamoja na kuwapiga makonzi wajukuu zake lakini
kuna wakati alikuwa akiketi chini na kufanya utani na kushuhudia vituko
vya wajukuu zake.
Moringe anasema moja kati ya maswali ya utani
waliokuwa wakimuuliza babu yao ni iwapo enzi za ujana wake alikuwa
akifanya starehe za aina mbalimbali.
“Tulikuwa tunamuuliza babu hivi unajua kuogelea au
kucheza muziki kwa sababu hatujawahi kukuona hata siku moja ukicheza,
alijibu ‘siwezi’, tukawa tunamuuliza sasa wewe ujana wako ulikuwa
unafanya nini, alisema ‘kusoma tu’, anasema Moringe.
Aidha wanasema utani mwingine kwa babu yao ilikuwa
ni kuwa hajui kuendesha gari. Julius anasema “Tangu nimepata akili
sijawahi kumuona akiendesha gari, nina wasiwasi alikuwa hajui
kuendesha”.
Julius pia anasema hajawahi kumuona babu yake akiwa amevaa suti
au kuchomekea huku akisema inawezekana zamani alikuwa analazimishwa
kuvaa hivyo. “Sijawahi kumuona babu amevaa suti au amechomekea shati,
hata hakupenda ndugu wavae suti hasa tukiwa Butiama, alipenda kuvaa
‘simple’.
Alisisitiza maadili
Moringe na Julius wanasema wanaamini babu yao
alikuwa akilinda maadili kwa kutowaachia watazame televisheni ovyo na
kuwahimiza kushiriki kanisani.
“Babu hakuwa na mchezo linapokuja suala la
kanisani, yaani usipoenda kanisani ni ugomvi mkubwa anaweza hata
kukufukuza usile naye chakula cha jioni,” anasema Moringe.
Wakizungumzia iwapo Baba wa Taifa angekuwa hai leo
angebariki matumizi ya mitandao ya kijamii kama ‘facebook’ na ‘twitter’
kwa pamoja walisema asingepinga kwani alikuwa mpenda maendeleo.
“Watu wengi huwa wanazungumza wakisema kuwa babu
alikuwa hataki watu waendelee kwa kutumia teknolojia, sio kweli, babu
alikuwa anapenda maendeleo lakini aliheshimu utamaduni,” anasema Julius.
Akitolea mfano wa dada yao mmoja aliyekuwa akiishi
Ulaya walisema, babu yao hakuwa na tatizo na mavazi yake lakini
alimwonya kuwa ni lazima aangalie anavaa wapi.
“Mfano tukiwa hapa Msasani babu hakumkataza kuvaa
nguo zake anazopenda, lakini tulipoenda Butiama alikuwa akimrudisha pale
anapovaa nguo anazoona haziendani na utamaduni wa watu wa kule,”
anasema Julius.
Anaongeza kuwa Mwalimu asingekuwa na tabu na
mitandao hiyo au teknolojia yoyote isipokuwa pale itakapotumikwa visivyo
kama wafanyavyo wengi.
“Ukiukwaji wa maadili unaotokana na teknolojia
unawakwaza watu wengi, watu wanatumia ndivyo sivyo na hiki pengine
kingemkera babu,” anasema Julius.
Siri ya kifimbo cha babu yao
Moringe na Julius wanasema wamesikia hadithi
nyingi kuhusu kifimbo cha Mwalimu Nyerere alichokuwa akipenda kukibeba,
wengine wamediriki kusema alizikwa nacho.
Julius anasema kwanza wanavyofahamu wao babu yao alikuwa nazo
zaidi ya nne, nyingine alinunua mwenyewe na nyingine alipewa zawadi.
“Babu alikuwa na fimbo nyingi, alibeba yoyote
anapotoka nyumbani, wakati mwingine aliweza kuisahau na kutuagiza
tumpelekee nje kama ameshatoka,” anasema Julius.
Aidha Moringe anasema amewahi kusikia kuwa asili
ya babu yao kutembea na fimbo hiyo ilitokana na nia yake ya kuacha
kuvuta sigara. “Niliwahi kusikia babu alikuwa akivuta sigara, sasa
alipotaka kuacha alipewa fimbo kama njia mbadala ya kushika kitu mkononi
ili aweze kuacha,” anasema Moringe.
Wasifu wa Julius na Moringe
Julius Kambarage (28) ni mtoto wa Makongoro ambaye
ni mtoto wa tano wa Mwalimu Nyerere na Moringe ni mtoto wa Magige
ambaye ni mtoto wa tatu.
Hivi sasa Julius anafanya kazi katika Kampuni ya
Uingizaji na Utoaji wa Mizigo (Clearing and Forwading) iitwayo Tesna
Quality wakati Moringe ni Ofisa Uwekezaji katika Mfuko wa Hifadhi za
Jamii (NSSF).
No comments:
Post a Comment