
Mkurugenzi wa Habari na Unezi wa Chadema, John Mnyika
Vyama vya Upinzani vimesema visipopata mwafaka wa mazungumzo baina yao na Rais Jakaya Kikwete juu ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba, vitarudi kwa wananchi kuwaleza hatua ya kuchukua.
Kauli hiyo inatokana na hotuba ya mwisho wa mwezi
iliyotolewa na Kikwete, alipoviomba vyama hivyo kusitisha dhamira ya
kuandamana Oktoba 10 mwaka huu kudai usawa katika mchakato wa katiba.
Kikwete aliviomba vyama hivyo kukaa nao meza moja kwa lengo la kufanya
mazungumzo ya kina ili kuondoa tofauti zilizopo.
Hatua hiyo ilifikiwa na Wabunge wa Upinzania baada
ya kususia Mkutano wa Bunge uliomalizika mwezi uliopita mjini Dodoma,
uliokuwa ukipitisha muswada huo kwa kile walichokilalamikia wananchi
kutowashirikisha ipasavyo.
Wakizungumza jana katika Mkutano wa Mashauriano
juu ya mchakato wa Katiba ulioandaliwa na Jukwaa la Katiba Nchini,
viongozi wa vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, APPT-Maendeleo, National
League of Democracy (NLD) na UPDP walisema, wanakwenda kumsikiliza
Kikwete na wasipofikia mwafaka watajua nini cha kufanya.
Mkurugenzi wa Habari na Unezi wa Chadema, John
Mnyika alisema endapo mwafaka hautafikiwa watarejea kwa wananchi
kuwaeleza kipi kitafuata.
Mnyika alisema Rais Kikwete anafahamu kila kitu
kinachopigiwa kelele na wapinzania na asasi za kiraia, hivyo wanaamini
watafikia mwafaka katika mazungumzo hayo.
“Tunakwenda kumsikiliza, lakini kama hatutafikia
mwafaka tutarudi kwa wananchi na kuwaeleza hatua ya kufuata kuidai
katiba yenye tija kwa wananchi,” alisema Mnyika, Mbunge wa Ubungo.
Mwenyekiti wa APPT-Maendeleo, Peter Mziray
alisema: “Kinachotakiwa ni mchakato kuanza upya na wananchi waelimishwe.
Tukiendelea hivi, maana yake tunaandaa katiba mbovu na isiyo na tija
kwa taifa,” alisema Mziray.
Mwenyekiti wa NLD, Emmanuel Makaidi alisema serikali ikubali kwamba imepoteza fedha hivyo mchakato hauna haja ya kuendelea.
Makaidi alisema katiba haitungwi bungeni, ila nje
ya Bunge hivyo mchakato kupitia bungeni na wabunge kutoweka mbele
masilahi ya taifa ni kuhatarisha mustakabali wa amani.
No comments:
Post a Comment