BABU mwenye furaha wa kinda wa Liverpool, Harry Wilson, amefanikiwa kuibuka na kitita cha Pauni 125,000 baada ya kutabiri kuwa siku moja mjukuu wake angeichezea timu ya taifa ya Wales wakati huo kinda huyo alipokuwa na umri wa miezi 18 tu.
Wilson ambaye yupo katika timu ya vijana ya
Liverpool, aliingia katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia baina ya
Wales na Ubelgiji Jumanne ya wiki iliyopita huku akiwa na umri wa miaka
16 na siku 207.
Peter Edwards, 62, aliingia katika jumba la kamari
la William Hill eneo la Wrexham mwaka 2000 na kuweka kiasi cha Pauni 50
akitabiri kwamba siku moja mjukuu wake atakipiga katika timu ya taifa
ya Wales.
Lakini kocha, Chris Coleman wa Wales, alimwita
mchezaji huyo kikosini kwa mara ya kwanza baada ya kuibuka nyota katika
timu ya vijana ya Wales na Jumanne iliyopita usiku alimwingiza uwanjani
akitokea katika benchi. Jambo hilo ndilo limempatia babu wa kinda huyo
mamilioni ya pesa.
Kutokana na pesa hizo pia, babu huyo ameamua
kustaafu kazi zake za kuendesha pikipiki eneo la Buckingham alikokuwa
akifuatilia mechi hiyo kwa karibu akitumia iPad yake.
Kwa mwaka mzima, Edwards ambaye anafanya kazi
katika eneo la Corwen, Clwyd, kaskazini mwa Wales alilazimika kuhamia
Buckingham kikazi, lakini baada ya mjukuu wake kumpatia noti hizo sasa
anarejea kwa mkewe Dorothy, 58 kwa ajili ya kupumzika.
“Mke wangu amefurahi sana. Mimi ninastaafu moja
kwa moja. Nilimwambia Meneja wangu jana (Jumatatu kabla ya mechi) kama
Harry akicheza basi siji kazini tena,” alisema Edwards akizungumzia
kutoka nyumbani kwake.
“Nimestaafu mwaka mmoja kabla ya wakati. Nimerudi
zangu nyumbani na sitarudi tena kazini (Buckingham). Sio mbaya kwa pesa
nilizopata.”
Edwards anakiri kwamba aliweka pesa zake baada ya
kugundua kwamba mjukuu wake, Harry, alionekana kupenda kucheza soka hata
alipokuwa bado mtoto mchanga.
“Alipendelea kuukimbiza mpira kwa mikono wakati
akitambaa kabla hata hajaanza kutembea. Hilo ndilo lilinipa wazo la
kwenda kucheza kamari. Nilikuwa na matumaini kwamba siku moja mambo
yangeenda sawa,” anaongeza Edwards.
Mara baada ya Harry kuonyesha kipaji maridhawa
katika shule ya soka ya watoto ya Liverpool, babu huyo alirudi tena
katika kampuni ya kamari ya William Hill kwa lengo la kwenda kuongeza
fedha lakini alikataliwa.
“Harry alikuwa na miaka 12 wakati huo. Hata hivyo walinikatalia
kwa madai kwamba tayari nilikuwa nimeshaweka kiasi cha kutosha kwao.
Walitabiri nibashiri kama angechagua kuichezea timu ya taifa ya
England.”
Hii ilikuwa na maana kuwa Edwards angeondoka na
kitita kikubwa cha pesa kama Harry angeamua kuichezea England kwa vile
bibi yake amezaliwa katika mji wa Chester England.
Ushindi huo wa kitita kinene cha pesa kwa Edwards
unatarajiwa kumnufaisha Harry kwa sababu safari zake kwenda kufanya
mazoezi na Liverpool pia zitagharimiwa na babu huyo.
Akiwa mchezaji kinda, bado Harry hapati pesa
nyingi katika soka na Edwards amedhamiria kutumia kiasi cha pesa
alizopata kwa ajili ya kumsaidia Harry katika nauli na mambo mengine.
“Hii ina maana nitamsaidia Harry katika matatizo yake. Kuwa na uhakika kuwa lazima na yeye atanufaika katika hili,” alisema.
Kwa kufanya alichofanya, Edwards anafuata nyayo za
baba wa kipa wa zamani wa Liverpool, Chris Kirkland, Eddie ambaye
aliwahi kupata noti baada ya kuweka pesa katika kampuni ya kamari akidai
kwamba mwanaye angeichezea timu ya taifa ya England siku moja.
Akiwa na umri wa miaka 11, baba yake Kirkland
pamoja na ndugu zake wengine waliweka Pauni 100 kila mmoja wakitabiri
kwamba kipa huyo kinda angeidakia timu ya taifa ya England kabla
hajafikisha umri wa miaka 30.
Kuanzia hapo kila mmoja alikuwa akisubiri pesa
zake baada ya kipa huyo kuanza kuichezea timu ya England chini ya miaka
21. Kuanzia mwaka 2003, Kirkland alianza kuitwa katika timu ya taifa ya
wakubwa ya England lakini hakuweza kukaa langoni mpaka Agosti 2006
alipoingia katika kipindi cha pili cha pambano dhidi ya Ugiriki.
Kutokana na mafanikio hayo ya kukaa langoni siku
hiyo, baba yake na wale wote walioweka Pauni 100 kila mmoja, walijikuta
akiondoka na kiasi cha Pauni 10,000.
No comments:
Post a Comment