
KOCHA wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson, amewaonya wachezaji wa zamani na wa sasa wa klabu hiyo akiwaambia hataficha kitu chochote katika kitabu cha maisha yake kinachotazamiwa kuzinduliwa keshokutwa Alhamisi.
Kitabu cha Ferguson kitaandika matukio aliyoyaona
kuanzia mwaka 1999 alipotoa kitabu chake cha kwanza mpaka Mei mwaka huu
alipostaafu kuifundisha timu hiyo.
Ferguson ameahidi kufichua siri za sakata
linalomzunguka mshambuliaji, Wayne Rooney, pamoja na sakata
lililozunguka katika uuzwaji wa mastaa wa zamani, David Beckham na Ruud
van Nistelrooy, ambao kwa nyakati tofauti walikwenda Real Madrid.
Wakati inasemekana Beckham aliuzwa kwa sababu ya
kubadili mfumo wake wa maisha mara baada ya kumuoa mwanamuziki wa kundi
la Spice Girls, Victoria Adams ‘Posh’, Van Nistelrooy inasemekana
aliondoka baada ya mzozo wake na Cristiano Ronaldo mazoezini.
“Unajua tatizo la kuandika kitabu ni kwamba
inabidi uandike vitu vidogo vidogo ambavyo vinaathiri au kupima uwezo
wako wa kufanya maamuzi. Lakini kwa sababu nimekuwa katika klabu hii kwa
muda mrefu, nikijenga timu baada ya timu, kuna maeneo ambayo hauwezi
kuyapuuza,” alisema.
“Kwa mfano tuliwahi kuwauza wachezaji kama David
Beckham na Ruud van Nistelrooy. Hauwezi kupuuza mambo haya kwa sababu
hawa walikuwa wachezaji wakubwa, wenye mamlaka makubwa katika historia
ya Manchester United.”
Ferguson pia anatarajiwa kueleza jinsi ambavyo
Wayne Rooney alitazamiwa kuondoka Old Trafford mwaka 2011 kabla
hajasaini mkataba mpya siku chache zilizofuata.
Anatarajiwa pia kueleza tena jinsi Rooney
alivyoomba kuhama kwa mara nyingi katika dirisha lililopita, kama
ambavyo Ferguson mwenyewe alikaririwa akiwaambia mashabiki waliojazana
kuhudhuria pambano kati ya Manchester United na Swansea Mei mwaka huu
wakati akiwaaga pale Old Trafford.
Katika kitabu hicho, Ferguson anakiri kwamba
kupoteza ubingwa kwenda kwa Manchester City mwaka 2012 ilikuwa moja kati
ya pigo kubwa katika maisha yake ya soka Manchester United.
Kocha huyo raia wa Scotland pia anatazamiwa
kufichua ugomvi uliojificha na nahodha wake wa zamani, Roy Keane, ambaye
awali alikuwa rafiki yake mkubwa, lakini katika siku za karibuni Keane
amekuwa akimshambulia Ferguson kwa madai kwamba hakumlinda wakati
anaondoka zake Old Trafford.
No comments:
Post a Comment