Wednesday, 31 July 2013
MAKALA: DILI LA AZAM MEDIA NA LIGI YA TANZANIA - SUPERSPORT NA ASILI YA SOKO LETU.
Wiki iliyopita kamati ya ligi ya VPL na TFF ziliingia mkataba na kampuni ya Azam Media Group kwa kuwauzia haki za matangazo ya Television kwa ajili ya kuonyesha ligi kuu ya Tanzania bara.
Pia zilitoka ripoti kutoka kwa baadhi ya vyombo vya habari kwamba kampuni nyingine kutoka nje ya Supersport ilionyesha kuvutiwa na dili hilo lakini ikashindwa na Azam Media ambao walitoa ofa kubwa zaidi. Hii ni habari ngumu kuiamini kwa kuzingatia hakuna mtu yoyote anahusika aliyethibitisha kama kweli SuperSport walitoa ofa rasmi ambayo ilizidiwa na wapinzani wao.
Tena ukiangalia uzoefu na ubavu wao wa kifedha na teknolojia katika uonyeshwaji wa michezo kwenye upande wa kusini mwa jangwa la Sahara, ni vigumu kuamini wangeweza kushindwa kirahisi kama kweli walikuwa wanahitaji kwa nia ya dhati kuonyesha ligi ya Tanzania. ukiliangalia Hili kwa mtazamo wa kibiashara zaidi utagundua kuwa kwenye nchi za Kenya na Uganda wana watumiaji wengi wa DSTV, Kenya wakiwa na asilimia 44 na Uganda 28, ukilinganisha na asilimia 12 ya Tanzania.
Kwa maana hiyo Tanzania imekuwa na wateja wachache wa huduma za DSTV, na wengi wao wanatumia kwa kuangalia mchezo wa soka, tofauti na nchi za Uganda na Kenya.
Kenya na Uganda wote wanashiriki kwenye michezo tofauti, rugby na riadha ambayo yote inaonyeshwa. Tanzania mchezo wetu mkuu ni soka, na michezo mengine hata kama ipo lakini haina dili kubwa kwenye masuala ya kuuza haki za matangazo ya TV. DSTV kama wangeamua kuja kuonyesha soka hapa Tanzania, basi uwekezaji wao mkubwa wa vifaa ungewagharimu zaidi ikizingatiwa ni soka tu ambalo wangeonyesha kwa maana kipindi kingine wakati ligi imesimama mitambo yao isingekuwa inatengeneza fedha za ziada - tofauti na nchi za Uganda na Kenya ambao muda wote inakuwa inafanya kazi kutoka na wingi wa michezo tofauti inayoonyeshwa kutoka kwenye nchi hizo.
Azam Media wanaweza kuwa wametoa ofa nzuri ya kifedha lakini kama Supersport wangetaka kweli kuonyesha umwamba wao wa kiuchumi, basi ingekuwa vita nzuri ya kibiashara - ambayo ingeviacha vilabu vyetu vikienda benki huku vinatabasamu.
Wakati GTV ilipotaka kuchukua haki za matangazo ya Kenya Premier league, SuperSport waligundua walikuwa wanapoteza kitu kikubwa sana kibiashara. GTV tayari walikuwa wameshakamata haki za matangazo ya ligi za Uganda na Tanzania na walikuwa wakitaka kumalizia na Kenya. Hivyo Supersport wakalazimika kuja na ofa nzuri zaidi na mwishowe wakafanikiwa kushinda tenda ya haki za matangazo za KPL. Hivyo ndivyo ushindani wa kibiashara ulivyo.
Ingekuwa SuperSport wanataka kweli na kuona kuna fursa ya kibiashara kuja kuwekeza kwenye ligi ya Tanzania basi wangeweza kutoa ofa nzuri zaidi waliyotoa Azam Media Limited. Lakini pia, kamati ya ligi ingeweza kufanya kazi nzuri zaidi kama wangetangaza tenda ambayo ingevutia media tofauti kuja kushindana kwa kutoa ofa tofauti.
vigumu kupata dili zuri zaidi ya walilitoa Azam Media limited ukiangalia na asili ya soko letu. Ambalo ni dogo na limejitenga kiasi kuwa na uwezo mdogo wa kuvutia Media kubwa kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kama ambavyo Azam wameweza.
Pia kama taratibu zote zingefuatwa, labda klabu zetu zingeweza kupata fedha nyingi zaidi kutokana na ushindani wa makampuni ambao ungekuwepo kugombea tenda hiyo. Lakini katikati ya maneno maneno yaliyojitokeza katika dili hili - tusisahau kwamba Azam wametoa nafasi kwenye mkataba kwa media nyingine kushirikiana nayo.
Azam kwa kutokuwa wabinafsi inasemekana waliamua kisiwepo kipengele ambacho kingefunga njia kwa wawekazaji wengine ambao wangetaka kushirikiana nao. Kwa mfano Zuku , StarTimes au SuperSport kirahisi tu wanaweza kushirikiana kibiashara na Azam katika kurusha matangazo hayo ya mechi za ligi kuu. Kwa kifupi, Azam TV hawajabana milango kwa wengine kwa maana ya 'exclusive rights', kuna nafasi kubwa ya Media nyingine zitakazojisikia kushirikiana nao kwa makubalianao watakayokubaliana.
Japokuwa dili bado dogo kwa baadhi ya vilabu vyenye bajeti kubwa, lakini bado ni tamu kwa vilabu vyenye bajeti ndogo japokuwa ni vigumu kuacha kuyasemea makosa yaliyofanywa na kamati ya ligi pamoja na TFF ya kutaka kulazimisha kusainisha mkataba na Azam Media.
Labels:
sports
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment