Kwa hisani ya bbc
Wanawake wa Kenya wanaofanya biashara ya kuuza Samaki
katika ufuo wa ziwa Victoria mjini Kisumu Magharibi mwa nchi,
wanajaribu kukomesha tabia ya kujihusisha na wavuvi kingono ili wapewe
Samaki bila malipo.
Tabia hii imelaumiwa pakubwa kwa kuchochea ongezeko la maambukizi ya HIV.Biashara hii inayojulikana na wenyeji kama 'Jaboya', ambapo mwanamke anafanya Ngono na wavuvi ili apate Samaki wa kuuza, imelaumiwa pakubwa kwa kueneza maradhi ya Ukimwi miongoni mwa watu wanaoishi katika maeneo ya Ziwa Victoria.
Sasa wanawake katika eneo hilo wamezindua kampeni inayolenga kukomesha biashara hiyo.
Mradi uliozinduliwa na taasisi ya utafiti wa mazingira ya Victoria, umeanza kuwapa wanawake hao maboti yao ili waweze kufanya uvuvi wenyewe.
Dan Abuto, afisaa mmoja wa shirika hilo, anasema kuwa pesa watakazopokea wanawake hao kutokana na biashara zao za Samaki, zitawaruhusu kutengeza boti zao wenyewe.
"mradi huu unalenga kushughulikia 'Jaboya' kama swala la afya ya umma , kupunguza viwango vya umasikini na kuleta usawa wa kijinsia,'' alisema afisaa huyo.
Wajane pia wanasemekana kuwa katika hatari kubwa zaidi kutokana na biashara hiyo hasa ikiwa ni jukumu lao kulisha familia zao.
Makundi ya wanawake yanasema kuwa boti hizo za thamani ya dola 920, hazitamaliza tu biashara hiyo bali pia zitapunguza kuenea kwa maradhi ya Ukimwi. Ikiwa mradi huu utafanikiwa basi maambikizi nayo yatapungua pakubwa.
No comments:
Post a Comment