Baada ya Chadema kuwavua nyadhifa zao aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto Kabwe, aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Dk Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, uamuzi huo ulilalamikiwa na baadhi ya watu kuwa haukufuata demokrasia.
Viongozi hao walipewa siku 14 kupeleka utetezi wao katika Kamati Kuu kueleza kwa nini wasifukuzwe.
Sasa tayari Dk Kitila na Mwigamba wameshafukuzwa uanachama huku Zitto akikimbilia mahakamani akipinga hatua hiyo.
Moja kati ya tuhuma zilizosababisha Zitto na
wenzake kuvuliwa nyadhifa na hatimaye kutimuliwa uanachama ni kuandaa
kile kinachoitwa ‘Waraka wa mabadiliko 2013’, japo Zitto anaukana huku
akisema kinachomponza ni kutangaza kugombea urais na uenyekiti wa chama.
Ni kweli, Zitto alitaka kugombea uenyekiti mwaka
2009 ila ikadaiwa kuwa ameshauriwa kujitoa, pia amekuwa kitangaza kutaka
kugombea urais kupitia chama hicho.
Chadema kimetumia mbinu nyingi kumtuliza Zitto,
lakini zimetafsiriwa kuwa ni kubinya demokrasia ndani ya chama. Baadhi
wamekituhumu kuwa ni chama cha kikabila, ukanda, cha wanaukoo.
Ajabu zaidi ni pale makada wa CCM wanaojitokeza
wakimlilia Zitto kuwa ameonewa na kwamba Chadema hakuna demokrasia ya
kweli. Lakini CCM hao hao sasa wanamshambulia Mbunge wa Monduli, Edward
Lowassa baada ya ‘ku-beep’ urais 2015. Akizungumza katika ibada ya
shukrani na kuupokea mwaka mpya, katika Kanisa la KKKT, Usharika ya
Monduli Mjini, Lowassa alitangaza kuanza rasmi kwa safari aliyoiita ya
matumaini ya ndoto zake.
Hatua hiyo imeonekana kuwachoma mno CCM, kwani haikupita muda, Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema kuwa wanaoonyesha nia ya kugombea urais kupitia chama hicho kabla ya wakati wameshapoteza sifa.
Kama hiyo haitoshi, Makamu Mwenyekiti wa chama
hicho, Philip Mangula akasema kuwa wanachama wake walioanza mbio za
kuwania urais mwaka 2015 watachukuliwa hatua kali za kinidhamu.
Ukilinganisha tambo alizokuwa akipiga Zitto katika
kutafuta uenyekiti wa Chadema na urais kupitia chama hicho, utaona
hakuna tofauti na za Lowassa.
Iwe ni kupitia harambee kanisani na misikitini,
kupitia mitandao ya jamii, kashfa kwa chama, viongozi wake na mengineyo,
zote ni mbinu wanazotumia kujitangaza Zitto na Lowassa na mashabiki
wao.
Kila chama kina kanuni na taratibu zake za kupata viongozi wa ndani na nje. Utaratibu huo hauzuii demokrasia kufanya kazi yake.
Huenda Chadema walikuwa wakifuata taratibu zao za kuwajibishana, kama ambavyo sasa CCM wanavyomdhibiti Lowassa.
Kumbe mkuki kwa nguruwe mtamu, kwa binadamu
mchungu. Kitendo cha Lowassa kujitutumua tu, CCM wameshaanza kutoa
vitisho kwa wanaoonyesha nia ya urais 2015. Wanaogopa nini? Hiyo si
ndiyo demokrasia ndani ya Chama?
No comments:
Post a Comment