Imezoeleka kuwa klabu za usiku zimekuwa zikitumika kwa mambo ya starehe huku viongozi wa dini wakizichukulia kama maeneo hatari kwa waumini wao.
Tofauti na maeneo mengine ya starehe, klabu za
usiku huwa na kumbi za muziki zenye taa za kumweka za rangi mbalimbali
huku giza likitawala. Wakati huo huo muziku hupigwa kwa sauti ya juu.
Mbali na muziki, klabu hizo husheheni vileo vya
kila aina huku watu wakiruhusiwa kuingia na mavazi yoyote wakiwemo wale
wanaopenda kuvaa nuzu uchi.
Hata hivyo kwa watumishi wengine wa Mungu, klabu sasa ndiyo pamekuwa mahali pa kuvunia waumini.
Mchungaji Harris Kapiga wa kanisa la Nchi ya Ahadi
lililoko Sinza Kamanyola, ameamua kuanzisha klabu ya usiku kama zilivyo
klabu nyingine za starehe.
Klabu hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni maeneo ya
Mbezi Tangibovu katika hoteli inayoitwa Mak Hotel, imeonekana kuvutia
vijana wengi ambao walionekana wakifurahia mandhari na muziki uliokuwa
ukipigwa ndani yake.
Tofauti na klabu nyinginezo, Mchungaji Kapiga
anasema kutakuwa na udhibiti wa vishawishi vya dhambi ikiwa pamoja na
ulevi, mavazi yasiyo na staha na aina ya muziki unaopigwa.
Anasema tangu alipoanzisha wazo hilo, watu wengi hasa wachungaji walikuwa na wasiwasi kuhusu vishawishi hivyo.
“Tangu nimeanza wazo langu hili nimekumbana na
vikwazo vingi. Imeshtua watu wengi, japo wengi wamelikubali na kuna
baadhi hawakubali ila hawawezi kusema wazi,” anasema na kuongeza:
“Wengine wanajiuliza nitawezaje kudhibiti vipi
hali ya klabu kwa sababu maeneo haya kunakuwa na anasa, ulevi na masuala
ya mavazi watu watavaaje, na mimi nawajibu.”
“Mtu akija hapa na mavazi mabaya hataingia,
tutakuwa makini sana katika hili. Mtu avae nguo yenye staha, siyo mtu
aje nusu uchi, tutamtoa kwa nia njema tu. Hata mtu aliyelewa tutamtoa
labda tusimgundue.”
Kwa nini ameanzisha klabu ya usiku? Mchungaji
Kapiga anasema alianza kupata wazo hilo siku alipokuwa kwenye sherehe za
kuadhimisha kuzaliwa kwa Clouds Media ambako pia ameajiriwa kama
mtangazaji.
“Kilichonifanya nianzishe wazo hili wakati tulipokuwa
tukiadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Clouds Media pale Billicanas club.
Nilikwenda pale kama mfanyakazi wao. Kulikuwa na vijana wengi mno siku
hiyo,” anasema na kuongeza:
“Kila mtu alikuwa akiitwa mbele na kusema
chochote. Mimi nilipoitwa nikaanza kuimba ‘wewe ni Alfa na Omega….” Watu
wakashangilia sana. Ile ilitia moyo kwamba kumbe hata nyimbo hizi
zinakubalika club? Nikasema kumbe inawezekana? Ndiyo nikaona nianzishe
kitu kama hiki.”
Anaongeza kuwa analenga kuwapata vijana ambao
hawapatikani makanisani wala kwenye mikutano ya injili bali kwenye kumbi
za starehe tu.
“Kuna watu wasiopatikana kanisani, kuna kizazi cha
watu ambao hatuwapati. Hapa siyo kwamba tuna cheza tu muziki, na
tutafanya maombezi kwa sababu tunafanya kiroho zaidi,” anasema na
kuongeza:
“Hata wakati mtandao wa ‘Facebook’ unaanza baadhi
ya watu waliookoka waliikataa wakisema ni mapepo na sehemu ya
kutongozana tu. Lakini kumbe ni mtandao unaoweza kupata marafiki wengi
unaoweza kushiriki nao mambo mengi.”
No comments:
Post a Comment