Mayoo mayoo namulaga ushing’weng’we, mayoo mayo namulaga ushing’weng’we, usambo wamalaga mitugo jisee lelo namulaga. Ushing’weng’we tongejagi asimize na bake bakwe.
Huu ni wimbo wa Kisukuma ambao kwa Kiswahili
tafsiri ya wimbo huu ni kwamba; “Mama mama nimeliua zimwi, zimwi hilo ni
mhalifu aliyemaliza mifugo yetu, leo nimeliua. Tumtenge aondoke zake na
wanawake kake.
Wimbo huu ulikuwa maarufu Kanda ya Ziwa na
ulikuwa ukitumiwa mara nyingi na walinzi wa jadi wa Sungusungu, kama
ishara ya kuonyesha kuwa wamekamata mhalifu na wanakwenda kumwadhibu.
Katika jamii ya watu wenyeji wa Kanda ya Ziwa,
hasa Kabila la Wasukuma wakisikia wimbo huo walijua ni hali ya hatari.
Walijua kuna mhalifu anakwenda kuuawa au kufanyiwa mambo mabaya zaidi na
walinzi hao wa jadi maarufu kwa jina la Sungusungu.
Hali hiyo ilizua woga hata baadhi ya kujifungia
nyumbani au kwa walio na roho ngumu, walijitokeza kutaka kujionea na
kuambulia viboko hasa kwa wale waliotaka kujua kulikoni hali hiyo,
walijibiwa kwamba Sungusungu hawaulizwi maswali.
Ushuhuda wa mwandishi
Kabla sijasonga mbele nitoe ushuhuda wangu mwaka
1984, nikiwa kijana mmojawapo wa vijana wa Sungusungu; ilipigwa filimbi
ya hatari, baadaye nikasikia wimbo huo ukiimbwa na vijana 20 wakitoka
kijiji jirani cha Bumanda, wilayani Nyangh’wale Mkoa wa Geita.
Baada ya kufika katika Kijiji cha Karumwa vijana
hao walipokewa na Msaidizi wa Mtemi wa Sungusungu (Mtwale), wa eneo
hilo. Namkumbuka kwa jina moja la Maholelo. Walikuwa wamemtanguliza bibi
kizee mmoja akiwa na kifurushi kichwani.
Kutokana na umri mdogo niliokuwa nao, sikujua
kinachoendelea, baadaye Mtwale aliteua vijana 20 na wengine wakaondoka
na bibi kizee huyo. Ilikuwa yapata saa1 usiku na yule Mtwale akawaambia;
shindikilagi (Msindikizeni), wale vijana waliondoka na bibi kizee
huyo.
Lakini sisi tulibaki kwenye eneo hilo tukisubiria
amri ya Mtwale, baada ya saa mbili walirudi na kudai yule bibi
amewakimbia, hali ambayo ilibainika baadaye kwamba kumbe kwa utaratibu
wa Sungusungu, Shindikilagi ilimaanisha nendeni mkamuue na ile taarifa
ya bibi kuwakimbia ilimaanisha kwamba wametekeleza mauaji.
Sungusungu walivyoanza
Ulinzi huo wa jadi ambao sasa upo nchi nzima na nchi jirani za
Kenye na Uganda, walianzia wilayani Kahama Kata ya Janna na baadaye
kuzinduliwa rasmi Kata ya Mwaluguru, mwaka 1982.
Kishosha Sitta (78), Mtemi wa Sungusungu wa Wilaya
ya Kahama ambaye baba yake, Sitta Kishosha ndiye mwanzilishi wa
Sungusungu mwaka 1982.
Katika makala haya anasimulia misukosuko aliyoipata wakati wa baba yake akizindua kikundi cha ulinzi wa Sungusungu.
Anaanza kwa kueleza kuwa kabla ya kuzinduliwa
rasmi, kwa Sungusungu, wananchi walikuwa wakifanya vikao vyao usiku wa
manane porini kwa kuhofia kukamatwa na polisi, hasa kwa kuwa mtandao wa
wahalifu uliwagusa hadi baadhi ya viongozi wa Serikali kwa wakati huo.
Sitta anasema kuwa wananchi walichoshwa na wizi
wa ng’ombe uliokuwa umeshamiri katika maeneo hayo ambapo walikuwa
wakiwakamata wahalifu lakini wakiwafikisha polisi, waliwaachilia na
ng’ombe walizoiba walikabidhiwa wahalifu husika.
Kutokana na hali hiyo, wananchi walianzisha
ulinzi huo ambapo walianza kwa kupiga yowe kuashiria mktano wao na
kufanya mipango ya kukabiliana na wezi hao wa ng’ombe ambao waliwaua
baada ya kuwakamata.
Matokeo ya mauaji hayo ya wahalifu yaliwazindua
polisi ambao walianza kuwasaka wananchi na kuwakamata popote walipokutwa
wakifanya mikutano yao ya kawaida, hivyo kuamua kufanya mikutano yao
kwa siri usiku.
Sitta anaeleza kuwa katika mikutano yao
walikubaliana kuacha kutumia yowe wakati wa kualikana kufuatilia wezi
hao wa ng’ombe, badala yake waliamua kutumia filimbi maarufu kwa
Ndolilo.
Anasimulia kwamba Ndolilo zilizokuwa zikipigwa
ziliwachanganya wezi wa ng’ombe, ambao mara nyingi walijikuta
wamezingirwa na kuuawa,kisha kufungwa kamba kwenye ng’ombe walioiba.
Wakati yakifanyika hayo kwa siri, mpango huo wa
Sungusungu uliendelea kupanuka, ambapo Sitta anasema kwamba ulianza
kuungwa mkono na wananchi wote wa Wilaya ya Kahama hadi mwaka 1982.
Baba yake aliteuliwa kuwa Mtemi.
Sitta anaeleza kuwa baada ya kuteuliwa kuwa mtemi,
baba yake, Mzee Kishosha, alikataa kufanya suala hilo kuwa siri, badala
yake aliitisha mkutano wa hadhara mwaka huohuo Kijiji cha Mwaluguru na
kutangaza rasmi kuundwa kwa Sungusungu.
Wakati akiitangaza rasmi kuundwa kwa Sungusungu, Serikali
iliendelea kuwakamata viongozi wake na wengine walihukumiwa ambapo Sitta
anasema kuwa, kutokana na upeo wa baba yake aliyewahi kuwa Katibu wa
TANU mkoani Shinyanga mwaka 1967, aliunda kamati ya watu saba
iliyokwenda kumwona Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Julius Nyerere
mwaka 1983.
Baada ya kuonana na kamati hiyo, Nyerere aliunda
tume iliyofika wilayani Kahama kufanya uchunguzi na kubaini kwamba
baadhi ya viongozi wa Serikali wa wakati huo walikuwa wanachama wa
makundi ya wezi wa mifugo na ndiyo waliokuwa wakipiga vita kuwepo kwa
vikundi vya ulinzi Sungusungu.
Sitta anakumbuka kuwa baada ya tume hiyo kumaliza
kazi yake, kuna mtu mmoja alitoka Ikulu aliyemtaja kwa jina la Kulwa
Mvanga, alifika Kahama na kufanya mkutano mkubwa mjini humo
akishirikisha viongozi wa Serikali, wakiwemo mahakimu na kutangaza kuwa
Sungusungu waachwe wakifanya kazi ya ulinzi, lakini wasikiuke sheria.
Hata hivyo, Sitta anasema kuwa baada ya mkutano
huo alikwenda kwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama wa wakati huo wakiwa na
mwenzake kwa lengo la kuuliza hatima ya wenzao waliokuwa magerezani.
Anakumbuka pia kwamba wakati huo DC alikuwa pia ndiye Katibu wa CCM.
Anaeleza kuwa siku hiyo hataisahau kwa sababu mkuu
wa wilaya hakuwepo, alikwenda kwa Ofisa wa Usalama wa Wilaya ambaye
wakati huo alikuwa Augustine Mrema.
Anasema kuwa ambaye baada ya kumweleza kuwa
alimpigia simu Mkuu wa Wilaya ya Kahama na baadaye wao waliwekwa chini
ya ulinzi na kupelekwa ofisini kwa DC.
Baada ya kufika huko, DC aliwahoji jambo moja
akitaka kujua kama wao ndiyo walioanzisha ulinzi pasipo kufuata
utaratibu na kusema atawafunga gerezani kwa kuwa majeshi yote eneo hilo
yapo chini yake.
Sitta anasimulia kuwa walipelekwa rumande na kesho yake walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela pasipo kujitetea.
Mawasiliano yake na Nyerere
Wakati wakiwa gerezani baba yake ambaye alifariki
mwaka 1990, aliwasiliana na Rais Nyerere, akamweleza hali halisi
ilivyokuwa ambapo licha yaSerikali kuagiza wawaache wafanye kazi yao ya
ulinzi kwa kuwa jukumu la ulinzi ni la kila raia wa Tanzania.
Akiwa gerezani Sitta pia alikutana na watu wengi
kutoka maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kahama, ambao walikuwa
wakijihusisha na ulinzi wa Sungusungu, ambapo tarehe Agosti 17 mwaka
1983, Nyerere akiwa Bukoba mkoani Kagera, alitangaza tena kupitia vyombo
vya habari amri ya kutaka Sungusungu wote waachiwe huru, ndipo siku
iliyofuata walitoka wote, baada ya kukaa gerezani miezi mitatu.
Anabainisha kuwa alipotoka gerezani kuna mtu mmoja
alimwambia kwamba aachane na kuunda vikundi vya Sungusungu ili asiibiwe
mifugo aliyemtaka pia ajiunge kwenye kundi la wezi wa ng’ombe, kwa
gharama ya Sh30,000 kama kiingilio
Anafafanua kuwa Sitta aliitafakari kauli hiyo, lakini aliendelea
na msimamo wake wa kuimarisha ulinzi wa Sungusungu, huku ikianza
kuungwa mkono na wananchi katika Wilaya za Geita, Nzega na Sengerema
hadi mwaka 1990, baba yake alipofariki.
Kazi ya Sungusungu
Pamoja na hayo Sitta anasema kuwa lengo kubwa la
kuanzishwa ulinzi wa Sungusungu lilikuwa kudhibiti wizi wa mifugo,
lakini kadiri ulinzi huo ulivyoenea ulipokewa tofauti hata kuingilia
mambo ya ushirikina, ambapo vikongwe walikuwa wakiuawa.
Sitta ni mjukuu wa Mwanamalundi
Sitta ambaye ni mtoto wa Sita Kishosha ambaye babu
yake ni mtemi Mwanamalundi aliyefariki mwaka 1936 mkoani Shinyanga na
kuacha historia kubwa ya Wasukuma kwa matukio yake ya kunyooshea miti
kidole kisha inakauka.
Sitta ambaye tangu mwaka 1995, amekuwa Mtemi wa
Sungusungu, Wilaya ya Kahama anasema kuwa upotoshwaji wa mapokeo ya
mpango huo wa ulinzi, ndiyo uliosababisha watu wengi waliokuwa
wakituhumiwa kufanya uhalifu kuuawa bila kuwapo ushahidi wa kutosha.
No comments:
Post a Comment