Waziri wa zamani katika Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa na katika Awamu ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, Dk Juma Ngasongwa amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinababaika katika kutekeleza majukumu yake.
Vilevile, chama hicho kimekumbwa mgawanyiko kati ya watendaji wake na Serikali na kwamba taifa lina ombwe la uongozi.
Kutokana na hali hiyo, Dk Ngasongwa ambaye pia ni
kada wa CCM amemshauri Rais Kikwete kuwa mkali katika kusimamia
watendaji wake anaowateua ndani ya chama na Serikali yake na kufuatilia
na kupima utekelezaji wa yanayokubaliwa .
Alikuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na
gazeti hili nyumbani kwake mkoani Morogoro anakoendesha maisha yake kwa
kilimo cha mpunga baada ya kustaafu.
Dk Ngasongwa alisema kuwa mgawanyiko huo kati ya
watendaji wa Serikali na CCM, umeondoa umoja siyo tu katika vyombo
hivyo, bali pia miongoni mwa wabunge wa chama hicho tawala.
Alisema kuwa hali hiyo inasababisha kutokea mambo
mengi ikiwamo matukio ya mawaziri kushinikizwa kujiuzulu kama
ilivyotokea hivi karibuni na kwamba kwa Serikali ya Awamu ya Nne hali
hiyo imekuwa ikijirudia.
“Chama tawala kinababaika sana, tena hata
watendaji wa CCM, wanawasema vibaya mawaziri hadharani, wakati wote ni
wateuliwa wa Rais (Jakaya Kikwete) na ndiye mwenyekiti wetu wa CCM. Hii
inakigawa chama. CCM ina utaratibu wake, kwa nini wasiitwe wakahojiwa
ndani ya chama, badala ya kutajana hadharani:
“Sielewi kwa nini CCM inababaika. Inachotakiwa ni
kuwa na mshikamano kwa wabunge wake kukutana mara kwa mara na kujenga
msimamo. Hii ni kazi ya mawaziri na wabunge pia,” alisema Dk Ngasongwa
na kuongeza:
“…Tatizo uongozi haufanyi kazi vizuri, ndani ya
chama chetu kuna mgawanyiko mkubwa hata katika Serikali, mfano
Mwanasheria Mkuu (AG) anaposema baadhi ya mawaziri hawamsikilizi, hii
‘No’ (hapana), lazima kanuni za uendeshaji wa Serikali zifuatwe, hii ni
muhimu.”
Alisema hali hiyo inaonekana hata kwenye Baraza la Mawaziri na kwamba mgawanyiko pia upo ndani ya Bunge kwa wapinzani.
“Lakini kugawanyika kwa upinzani ni afadhali
kuliko CCM, kwani matokeo yake ni kupunguza imani ya watu kwa Serikali
yao na chama tawala,” alisema.
Akinukuu maneno ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, Dk Ngasongwa alisema: “Nyerere alisema, bila CCM
madhubuti nchi itayumba na ndiyo yanayotokea sasa.
“Msingi wa yote yanayotokea ni ubinafsi, ubepari…;
turudi kwenye Ilani ya chama, tuzungumze, tufikie mwafaka, siyo
kutukanana hadharani. CCM itoe mwongozo siyo kugawa wananchi.”
Ngasongwa aliyeshika nyadhifa mbalimbali za
kisiasa katika CCM na Serikali ikiwamo ujumbe wa Kamati Kuu (CC), ubunge
wa Ulanga Magharibi, Waziri wa Maliasili na Utalii na baadaye Waziri wa
Mipango, Viwanda na Uwezeshaji, alifafanua kwamba kuna ombwe la uongozi
katika chama tawala, upinzani, Serikali hata bungeni.
“Kuna ombwe la uongozi siyo tu kwa wapinzani, hata
sisi chama tawala CCM, Serikali, hata bungeni pia kuna mchanganyiko na
yanaonekana waziwazi. Tunaona Spika anavyodharauliwa na wabunge. Bunge
linaonyesha picha ya hali halisi ya nchi yetu ilivyo,”alisema Dk
Ngasongwa.
Alipotakiwa kuzungumzia zaidi tukio la hivi
karibuni la Rais Jakaya Kikwete kutengua uteuzi wa mawaziri wanne
walioshinikizwa kujiuzulu kutokana na Ripoti ya Kamati ya Ardhi,
Maliasili na Mazingira kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, alieleza
kuwa hajaisoma kwa undani ripoti hiyo, lakini inaonyesha kuwa
utekelezaji wake ulikuwa mbaya.
Hata hivyo, alisema kuwa kamati hiyo ilitakiwa
kuainisha makosa ya watendaji wa operesheni hiyo na kuwaacha mawaziri
wajipime na kujiuzulu wenyewe.
Alisema kwamba hatua ya wabunge na kamati
kushinikiza mawaziri hao wajiuzulu iliwachongea kwa Rais Kikwete
aliyeamua kuwafukuza kazi kwa lugha ya kistaarabu, hali ambayo alielezea
kuwa inaweza kujenga uhasama baina ya wabunge, kamati na mawaziri
walioondolewa.
Hivi karibuni Rais Kikwete alitengua uteuzi wa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, Waziri wa Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamshi Vuai Nahodha, Waziri wa Mambo ya
Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi pia Waziri wa Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi,
Dk Mathayo David Mathayo baada ya wizara zao kutajwa kushindwa kusimamia
Operesheni Tokomeza Ujangili, iliyopoteza maisha ya watu, mifugo na
vitendo vya ukatili kwa binadamu.
Kuhusu kubadilika kwa mawaziri, Dk Ngasongwa
alieleza kuwa jambo hilo siyo baya, lakini akasema kwamba likifanyika
mara kwa mara linadumaza wizara kwa kukosekana mwendelezo wa utendaji.
“…Ikitokea mara kwa mara inadumaza utendaji,
hupati ‘continuity’ (mwendelezo mzuri), kwani mawaziri huhitaji
kujifunza na utekelezaji huhitaji muda. Continuity ni muhimu kwa
mawaziri, hata watendaji wengine,” alisema.
Hii ni mara ya tatu kufanyika kwa mabadiliko ya
Baraza la Mawaziri tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Nne
ya Rais Jakaya Kikwete, likiwamo lililotokea baada ya aliyekuwa Waziri
Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu.
No comments:
Post a Comment