Moshi. Mambo mazito yameibuka kufuatia tukio la kutekwa nyara kwa mwanamke mmoja wa mjini Moshi wiki iliyopita.
Mambo hayo ni pamoja na kubainika kuwa aliyetekwa ni mke wa mtoto wa kigogo mmoja wa Serikali mkoani Dar es Salaam.
Mwanamke huyo aliyesafirishwa na watekaji hadi
jijini Dar es Salaam ni mke wa mfanyabiashara Jerome Mushi ambaye ni
mtoto wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala iliyoko mkoani Dar es Salaam, Raymond
Mushi.
Taarifa za uhakika zilizopatikana jana zilisema
watekaji hao akiwemo mwanamke mmoja waliojifanya kuwa ni maofisa wa
upelelezi wa polisi, waliondoka na kitita cha Dola 11,000 sawa na Sh18
milioni.
Habari hizo zinadai kuwa baadaye mwanamke huyo
aliahidi kuwalipa watekaji hao Sh100 milioni lakini angezilipa fedha
hizo jijini Dar es Salaam kupitia kwa mtu anayetajwa kwa jina la utani
la White.
“Aliwaambia atawapa Sh100 milioni na kwamba katika
akaunti yake kuna Sh30 milioni na walisafiri naye hadi Dar es Salaam
kwa kutumia gari la watekaji aina ya Toyota.
RAV4,”kilidokeza chanzo chetu.
Ilielezwa kuwa baada ya kufika jijini Dar es
Salaam Ijumaa iliyopita, mwanamke huyo pamoja na watekaji wake walifikia
katika hoteli moja na kumpigia simu White ili amnasue katika jambo
hilo.
Hata hivyo, White inadaiwa alitilia mashaka
uhalali wa polisi hao na akauliza kwa baadhi ya polisi anaowafahamu
ambao walimjulisha kuwa watu hao ni mtandao wa genge la matapeli wa
jijini.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz amethibitisha habari kuhusu kutekwa nyara kwa mwanamke huyo.
“Ni kweli hao watu walifika nyumbani kwa huyo mwanamke na kujitambulisha kuwa ni maofisa wa polisi wakimtuhumu
kuwa anajihusisha na biashara ya dawa za kulevya,”alisema Kamanda.
Kamanda Boaz alisema baada ya mumewe kurudi nyumbani na kuelezwa
kuwa mkewe amepelekwa Kituo cha Polisi mjini Moshi, alifuatilia ili
kujua kulikoni.
Alisema hata hivyo walimweleza kuwa hakuna shauri la aina hiyo.
No comments:
Post a Comment