Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadik, amesema zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama 'wamachinga' na ombaomba mitaani, litaanza kesho.
Alisema wafanyabiashara hao ni pamoja na
wale wenye ulemavu wa viungo na kwamba zoezi lina lengo la kuendeleza
Jiji la Dar es Salaam kuwa katika hali ya usafi.
Aidha, alisema ombaomba wote waliozagaa katikati ya mitaa ya Jiji watakusanywa na kurudishwa makwao.
Sadik aliliambia gazeti hili jana kuwa
uchunguzi uliofanywa na ofisi yake, umegundua kuwa ombaomba asilimia 90
wanatoka nje ya mkoa wa Dar es Saalam na asilimia 10 ni wa jijini ambao
wanandugu wenye uwezo.
“Tumeamua kuwarudisha ombaomba wote vijijini kwao," alisema.
Aliongeza kuwa wamachinga wanaofanyabiashara katika maeneo yasiyo rasmi watapelekwa kwenye masoko rasmi waliyopangiwa.
Alisema magari kwa ajili ya kuwasambaza
wamachinga wanaofanyabiashara za vyakula na mbogamboga barabarani
watapelekwa kwenye masoko ya vyakula, na wale wa bidhaa za madukani
watatakiwa kukodisha fremu.
Alisema ofisi yake imeandaa kikosi cha askari wa jiji na magari yatakayobeba bidhaa za machinga hao kwenye masoko waliyopangiwa.
Sadik alisema kuwa lengo la zoezi hilo ni
kuliweka jiji la Dar es Salaam katika hali ya usafi na kufanana na
majiji mengine duniani yaliyokaa kibiashara.
Alisema wageni kutoka nje ya nchi wana nia yakuja kuwekeza jijini na fursa hizo zipo kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wote.
Uchunguzi uliofanywa umegundua
kuwa baada ya ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama, Jiji la Dar es
Salaam liliendelea kuwa katika hali yake ya uchafu baada ya
wafanyabiashara hao kurudi kwa staili ya kuweka meza ndogo na kuuza vitu
vidogovidogo, wakati wanaouza nguo huanza kazi yao majira ya saa 11
jioni.
Maeneo ambayo yalishuhudiwa biashara hizo zikiendelea kama kawaida ni Mwenge, Mabibo Posta na Ubungo.
No comments:
Post a Comment