Klabu ya Tottenham Hotspurs imekubali kuilipa Valencia ya Hispania kiasi cha Euro Milioni 30 kwa ajili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Hispania Roberto Soldado . Hii ni baada ya klabu hizo mbili (Valencia & Tottenham) kufikia makubaliano katika mazungumzo yaliyofanyika hapo jana (siku ya jumamosi).
Mkurugenzi wa masuala ya ufundi wa Tottenhma Mtaliano Franco Baldini alikuwepo jijini Valencia kukamilisha mazungumzo hayo ambapo Spurs wanatarajiwa kumthibitisha Soldado kama mchezaji wao rasmi baadaye wiki inayofuata .
Usajili wa Soldado unamfanya kuwa mchezaji wa tatu kusajiliwa na Spurs baada ya kiungo wa Brazil Paulinho aliyesajiliwa toka klabu ya Corinthians na Winga wa Ubelgiji Nacer Chadli toka klabu ya Fc Twente ya Uholanzi.
Awali mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy alitegemea kumsajili Soldado kwa angalau euro milioni 26 lakini alilazimika kuongeza mkwanja baada ya Valencia kukomaa huku kukiwa na ofa toka kwa klabu ya Liverpool ambayo ilikuwa ikiangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji huyo .
Tayari Spurs imekamilisha mazungumzo ya masuala binafsi na mchezaji mwenyewe(Soldado) na kilichobaki ni kukamilisha jinsi malipo yatakavyofanyika baina ya klabu mbili ambapo Valencia wangependa kulipwa kwa mikupuo miwili ya Euro milioni 15 huku Spurs wakijaribu kufanya malipo hayo kwa mikupuo mingi kwa nyakati tofauti .
Soldado anakubali kujiunga na Spurs baada ya kukataa kujiunga na klabu hiyo msimu uliopita wakati Spurs ilipojaribu kumsajili . Mshambuliaji huyo alijiungana Valencia mwaka 2010 akitokea Getafe ambako alikuwa amesajili toka klabu yake ya kwanza ya Real Madrid
No comments:
Post a Comment