Kamanda wa Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova |
Tukio
jipya na la aina yake limefichuliwa na mtoto wa marehemu ambaye
alisema, kabla ya kufikwa na mauti baba yake, alikamatwa na kupigwa na
polisi katika maeneo ya Kurasini jijini Dar es Salaam.
Taarifa
za polisi kuhusika na mauaji ya mwananchi huyo aliyetajwa kwa jina la
Selemani Mwinyimsanga mwenye umri wa kati ya miaka 35 na 40 zilitolewa
kwa mara ya kwanza na mtoto wa marehemu ambaye alishuhudia askari hao
wakimpa kipigo baba yake.
Kuvuja
kwa taarifa hizo za polisi kuhusishwa na tukio hilo, kulielezwa jana na
binamu wa marehemu, Joachim Mgembe wakati alipozungumza na vyombo vya
habari jijini Dar es Salaam.
Akisimulia
mkasa huo uliotokea Jumanne ya wiki iliyopita, Mgembe alimkariri mtoto
huyo wa marehemu ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu aliyemtaja kwa
jina moja la Geoffrey akisema aliona namna baba yake alivyokuwa
amedhoofika baada ya kipigo hicho.
“Nilipata
taarifa juzi kutoka kwa mtoto wa kaka wa marehemu anayeitwa,Nasoro
Hamadi, kuwa baba yake mdogo ambaye ni marehemu, amefariki dunia.
“Alinieleza
kuwa, Selemani alikamatwa na polisi katika eneo ambalo halikufahamika
na kisha askari hao wakamchukua na kumpeleka nyumbani kwake Kurasini.
“Walipomfikisha nyumbani kwake, walianza kupekua ndani na inaonekana hawakukuta kitu.
“Baada
ya upekuzi huo, wakaanza kumpiga, inasemekana walimpiga sana hadi
akadhoofika na kwa bahati nzuri wakati wanampiga marehemu, alikuwapo
mtoto wa mke wake.
Mgembe
alimkariri mtoto huyo akisema mara baada ya kipigo hicho polisi hao
waliondoka na baba yake na wakaenda naye eneo lisilojulikana.
Alisema mara tu baada ya tukio hilo, kijana huyo alimpigia simu mama yake akimueleza kuhusu kile kilichotokea.
Mawasiliano
hayo yalisababisha mke huyo wa marehemu kurejea nyumbani kwa dharura na
kutoa taarifa kwa ndugu na jamaa zake kabla ya kuanza kumtafuta mumewe
katika vituo mbalimbali ya polisi.
Kwa
mujibu wa Mgembe, polisi hao walimchukua marehemu hadi kituo cha polisi
cha Oysterbay ambako inadaiwa marehemu akiwa hapo kabla mauti kumfika
aliwasiliana kwa simu na dada yake kwa njia ya simu akimueleza namna
alivyopigwa na polisi kwa kiwango cha kuhitaji msaada wa matibabu.
“Ndugu
walikwenda pale Polisi Oysterbay ili kumdhamini lakini walipofika
kituoni hapo, waliambiwa hakukuwa na taarifa za ndugu yetu na
wakawashauri waende Kituo cha Polisi, Stakishari Ukonga ambako ndiko
walikohisi marehemu angeweza kukutwa.
“Ndugu
zangu hawakukata tamaa, walikwenda Stakishari, ambako nako
hawakuambulia kitu zaidi ya kupewa majibu kuwa hawajamkamata mtu wa
namna hiyo.
Baada
ya majibu hayo, Mgembe alisema majibu hayo yalisababisha ndugu hao
kurejea tena Polisi Oysterbay ambako ndugu yao aliwaeleza awali kwamba
ndiko alikokuwa akishikiliwa. Wakiwa kituoni hapo, Mgembe anasema ndipo
baadhi ya askari polisi wawili ambao hawakuweza kuwataja walipowaeleza
kwamba ndugu yao waliyekuwa wakimtafuta alipoteza maisha kutokana na
kipigo.
“Walipokuwa
kituoni hapo, waliibiwa siri na askari wawili waliokutana nao kwenye
ngazi na kuambiwa kuwa, ndugu yetu alifikishwa kituoni hapo, lakini
kutokana na kipigo alichokuwa amepata, alikuwa amefariki dunia.
Mgembe
alisema taarifa hizo zilisababisha dada wa marehemu kuangua kilio hapo
hapo, tukio lililosababisha polisi waliofichua siri hiyo kutoweka,
pengine kwa kuhofia usalama wao wa kikazi baada ya kufichua siri hiyo.
Baada
ya taarifa hizo, ndugu wa marehemu walianza kuzunguka katika hospitali
mbalimbali kumtafuta ndugu yao, wakianzia na Hospitali ya Taifa
Muhimbili ambako hawakufanikiwa. Baada ya kutoka hapo, walikwenda katika
hospitali ya Mwananyamala, ambako walikuta mwili wa marehemu ndugu yao.
Akizungumzia
tukio hilo, kaka mwingine wa marehemu, Hassan Mwinyimsanga alitaka
uchunguzi ufanywe kuhusu mazingira tatanishi ya kifo cha ndugu yake.
No comments:
Post a Comment