
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe amevunja ukimya na kusema hayuko tayari kwa sasa kuwataja Watanzania wenye mabilioni huko Uswisi na kuitaka Serikali ifanye uchunguzi.
Zitto ndiye aliyeibua hoja bungeni kuwa kuna Watanzania walioficha Sh315 bilioni katika taasisi za fedha nchini Uswisi.
Katika taarifa yake aliyoitoa jana, Zitto alisema
anasita kutaja majina hayo sasa ili kuepusha kile alichosema majina hayo
kutumiwa vibaya bila kujali kama Watanzania walizipata fedha hizo
kihalali au la na kuzihifadhi nje ya nchi.
Alisema ameshauri mchunguzi wa kimataifa anafaa kufanya kazi hiyo.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), amesema wastani wa Sh729.3
bilioni hutoroshwa kila mwaka kwenda nje ya nchi.
Alisema kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Fredrick Werema kwamba yeye (Zitto) hakutoa ushirikiano wa kamati
inayochunguza sakata hilo si ya kweli.
“Nataka niwahakikishie, nimekutana mara nne na
kamati hii. Nimewapa mpaka jina la mchunguzi wa kimataifa atakayeweza
kuwasaidia katika uchunguzi huu, leo naambiwa sitoi ushirikiano,”
alisema Zitto.
Alisema mchunguzi huyo wa kimataifa ana uzoefu
katika uchunguzi wa suala kama hilo na angeweza kuwatambua kwa majina na
kiasi cha fedha na pia uhalali na uharamu wa fedha hizo.
Alisema ameshangazwa na hatua ya Serikali kumbeza
pale alipopendekeza suala la kutafutwa mchunguzi wa kimataifa lakini
siku chache baadaye ikatangaza magazetini nafasi ya kazi hiyo.
Tangazo hilo lilichapwa Desemba 17, mwaka huu siku
ambayo Zitto alisema kwamba angesoma maelezo binafsi kujibu kauli ya
Jaji Werema. Hata hivyo, alisema alikosa nafasi. Zitto amesema
hashurutishwi na azimio la Bunge kutaja majina hayo kwa sababu yeye siyo
chombo cha uchunguzi ambacho kinapaswa kuwa na mkono mrefu.
Alisema wakati akikabidhi majina ya Watanzania
hao, angependa ushahidi huo uwe umefanyiwa uhakiki na vyanzo vyake vya
kimataifa na vyombo vya usalama vya Serikali nchini.
“Siko tayari kutaja kwa sasa. Narudia tena kwa
sasa hayo majina maana naweza kusababisha wahukumiwe na umma bila
kupitia utaratibu uliowekwa na sheria zetu hapa nchini,” alisema Zito
Alisema inawezekana pengine shinikizo hili linatoka kwa
watuhumiwa wenyewe baada ya kuona watu wengine waliokumbwa na kashfa
nyingine walitajwa majina na hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Mimi kama kiongozi makini na kama wasiwasi huu
nilionao utakuwa wa kweli basi siko tayari kurudia makosa yaleyale ya
kutaja majina halafu ikaishia hapo bila wahusika kushughulikiwa,”
alisema.
Alisema suala la utoroshaji wa fedha nje ya nchi
ni kubwa kuliko Watanzania wa kawaida wanavyolifahamu na kusema hilo ni
janga la kitaifa na kimataifa na si la Zitto pekee.
Akitoa mfano, Zitto alisema uchunguzi unaonyesha
mwaka 2010 pekee, kiasi cha Sh2.1 trilioni kilitoroshwa hapahapa nchini
na mwaka 2011 kiasi cha Sh1.3 trilioni kilitoroshwa kwenda nje.
Alisema taarifa za mashirika ya kimataifa
zinaonyesha kuwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, kiasi cha fedha
kilichotoroshwa hapa nchini na kupelekwa nje ya nchi ni Sh7.3 trilioni.
Zitto alisema hali hiyo si nzuri hata kidogo kwani
inatokea wakati kuna Watanzania wanaoishi katika lindi kubwa la
umaskini na kutahadharisha kuwa ipo siku kundi hilo linaweza kuchukua
hatua.
“Nawaomba wenzangu waifanye vita hii kama ya
Watanzania wote, wafahamu wale wenye masilahi na fedha hizi hawataacha
kufanya kila njia kubeza vita hiyo. Mimi ni mpuliza filimbi tu katika
vita hii na Watanzania wajue sina uwezo wa kuishinda vita hii peke yangu
bila kuungwa mkono na wabunge, wananchi na hata Serikali.”
No comments:
Post a Comment