
Huenda safari ya kisiasa kama za waziri kwa Dk Emmanuel Nchimbi na wenzake watatu kuwa imekamilika.
Ni baada ya wiki jana Rais Jakaya Kikwete kutengua
uteuzi wake pamoja na kina Dk Mathayo David Mathayo (Mifugo na Uvuvi),
Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Shamsi Vuai Nahodha
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).
Hata hivyo, Dk Nchimbi amekuwa ni mmoja kati ya
viongozi ambao ni vigumu kuwasahau katika uongozi wao kama waziri kwani
alionekana mcheshi au mtu mkarimu.
Mbali na hilo pia alikuwa waziri asiyependa
kujinadi, hakuwa mwenye hasira mbele ya umma, pengine ilitokana na
wizara aliyokabidhiwa.
Aliteuliwa mwaka 2010 akiwa Waziri wa Habari,
Vijana, Utamaduni na Michezo kabla ya kuhamishiwa Mambo ya Ndani ambako
Operesheni Tokomeza imemwondoa.
Dk Nchimbi ameondolewa katika nafasi hiyo huenda
wako ambao wamepumua au kusherehekea wakati huu wa sikukuu hizi za
mwisho wa mwaka. Kwa kipindi cha miaka mitatu aliyokaa katika nafasi
hiyo wako ambao wamekiona ‘cha mtema kuni’ huku baadhi yao wakipoteza
maisha mikononi mwa polisi, idara ambayo ilikuwa chini yake.
Muda wa miaka mitatu, mwanasiasa huyu binafsi au
wizara yake imekutana na changamoto lukuki ambazo ni pamoja na machafuko
katika sehemu mbalimbali ya nchi yaliyohusishwa na siasa, dini, sanjari
na ajali. Matukio ya uchomaji moto wa makanisa kule Zanzibar katika
kipindi cha uongozi wa Dk Nchimbi pale Mambo ya Ndani ni matukio ambayo
wengi watamkumbuka nayo.
Tukio la Mei 5, mwaka huu, lile la mlipuko wa bomu
uliotokea kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi,
Olasiti mkoani Arusha na kusababisha vifo kwa watu watatu na kujeruhi
wengine 67 ni miongoni mwa yale ambayo mwanasiasa huyo ameyaacha nyuma
yake.
Mei mwaka huu kule Iringa, vurugu baina ya polisi
(FFU) na wafanyabiashara ambako watu 50 walikamatwa kutokana na tukio
hilo akiwamo Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema)
kwa madai ya uchochezi, ni mwendelezo wa visa katika uongozi wake.
Mei 22, mwaka huu, vurugu zilizotokea Mtwara na
kusasabisha athari kadhaa, zikiwamo majeruhi na watu kupoteza, uhai na
makazi ni kumbukumbu nyingine mbaya kwa mwanasiasa huyu.
Bomu lililorushwa kwenye mkutano wa Chadema mjini
Arusha na kusababisha majeruhi 10 na watu wawili kufariki dunia ni doa
jingine katika zama hizo za Dk Nchimbi.
Hata hivyo, jambo la kushangaza katika mazungumzo
yake na waandishi wa habari kuhusu changamoto hizo, Dk Nchimbi
alionyesha mfano wa jirani aliyealikwa kwenye msiba usiomhusu.
Ripoti ya matukio ya mauaji iliyotolewa na Kituo cha Sheria na
Haki za binadamu ilibainisha kuwa Watanzania 40 waliuawa lakini wahusika
hawakukamatwa au kuwajibishwa.
Kwa hiyo, heshima ya Tanzania kama kisiwa cha amani ilianza kuyeyuka na kuacha madoa.
Kwa hiyo, kuondolewa kwa Nchimbi pale Mambo ya
Ndani kwa sasa kunaweza kutafsiriwa kwa mitazamo mbalimbali, ingawa si
kuhusishwa na uwezo binafsi wa mwanasiasa huyu kijana.
Kwa ufupi, Dk Nchimbi ameondoka Mambo ya Ndani,
tumtakie kila heri ila tufungue ukurasa mpya mwaka 2014 na kumkaribisha
mrithi wake.
Namwomba Rais Kikwete wakati tukisubiri waziri
atakayevaa kiatu hicho kwamba tunahitaji kiongozi makini, mwenye uwezo
mkubwa katika kudhibiti mbinu zote zikiwamo uhalifu.
Kikubwa ni kusaidiwa na Jeshi la Polisi lenye viongozi waadilifu, wanaotimiza wajibu wao ipasavyo.
Ninaamini Rais Kikwete atasikia kilio cha
Watanzania, hatasita kuwang’oa mawaziri wengine wasio na uadilifu na
uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment