LIGI Kuu England kwa miaka mingi tu imeshuhudia vipaji vya
uhakika vya wachezaji wanaotumia miguu ya kushoto. Baada ya Mjerumani
Mesut Ozil kutua Arsenal, huku Gareth Bale akihamia Hispania, bado
kwenye ligi hiyo kuna wachezaji wanaotisha kwa ufundi wa kutumia miguu
ya kushoto.
5. Moussa Dembele - Tottenham

Mbelgiji mwenye uwezo mkubwa wa kutamba kwenye
safu ya kiungo na msumbufu wa wapinzani. Kwenye kulifanya hilo, silaha
kubwa ya staa huyo ni mguu wake wa kushoto unaomwezesha pia kupiga
mashuti makali. Uwezo wake wa kuwachambua wengine kwenye sehemu ya
kiungo umemfanya afananishwe na Patrick Vieira. Ujuzi wake wa kumiliki
mpira umewafanya wachambuzi wa soka kumfananisha na Ozil, lakini kazi
kubwa inafanywa na mguu wake wa kushoto.
4. John Arne Riise - Fulham


Ujuzi wake alianza kuonekana wakati alipokuwa
kwenye kikosi cha Liverpool kabla ya kuhamia Fulham. Amekuwa akifunga
mabao muhimu kwenye kikosi hicho. Uwezo wake wa mguu wa kushoto
umemfanya aimudu vyema nafasi ya beki wa kushoto na winga. Staa huyo wa
Norway pia ni fundi wa mipira iliyokufa.
3. Robin van Persie - Man United


Kwenye orodha ya washambuliaji wa Ligi Kuu England
kama kuna mchezaji ambaye mabeki wanakuwa na hofu pindi mpira unapokuwa
kwenye mguu wake wa kushoto basi ni straika wa Kidachi, Robin van
Persie.
Fowadi huyo anafahamu namna ya kuutumia mguu wake
huo na kufunga mabao ya aina tofauti ikiwamo mipira ya adhabu. Hakika
ndiye straika anayetisha zaidi na mguu wake wa kushoto.
Moja ya mabao yake ni lile alilofunga akiwa
Arsenal kipindi ilipomenyana na Charlton Athletic, bao ambalo linatajwa
kuwa bora zaidi lililowahi kufungwa kwa mguu wa kushoto kwenye Ligi Kuu
England.
2. Mesut Ozil - Arsenal


Ndiyo yuko katika msimu wa kwanza kwenye Ligi Kuu
England, lakini tayari ameonyesha cheche kali kutokana na ujuzi mkubwa
wa kucheza soka kwa kutumia mguu wake wa kushoto.
Mguu huo ndiyo uliotengeneza nafasi kadhaa za
kufunga kwenye ligi hiyo na kuipa faida kubwa Arsenal msimu huu kwenye
Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Akiwa amewahi kuwa chini ya
Jose Mourinho walipokuwa pamoja Real Madrid, Mreno huyo alikiri kwamba
hakuna mchezaji mwenye ujuzi wa kutumia mguu wa kushoto kama alivyo
Ozil.
1. Ryan Giggs - Man United

Gwiji lao. Giggs kwa karibu miongo miwili
mfululizo amekuwa akiwakimbiza mabeki wa timu pinzani kwa kutumia mguu
wake wa kushoto na kuwa mchezaji mwenye hadhi kubwa kwenye Ligi Kuu
England. Umahiri wa mguu wake huo umemtambulisha kiungo huyo wa
Manchester United kuwa nyota hatari kwa miaka yote 20 aliyodumu kwenye
ligi hiyo.
Amefunga mabao zaidi ya 114 kwenye kikosi hicho
cha Manchester United, huku bao lake alilofunga dhidi ya Arsenal kwenye
Kombe la FA likibaki kuwa kwenye kumbukumbu ya kipekee.
No comments:
Post a Comment