
KIPA mwenye heshima kubwa nchini ambaye sasa anaichezea Yanga, Juma Kaseja amewaambia mashabiki wa timu hiyo kwamba hakufungwa makusudi bao la tatu dhidi ya Simba kwenye mechi ya Mtani Jembe. Simba ilishinda mabao 3-1.
Kaseja alifungwa bao hilo dakika ya 62 baada ya
kushindwa kumiliki vizuri mpira aliorudishiwa na Mbuyu Twite, ambapo
mshambuliaji wa Simba, Awadh Juma alimuwahi na kumpokonya mpira halafu
akafunga.
“Lengo lilikuwa nimiliki mpira na kupiga sehemu
nyingine, sasa wakati nafanya hayo ndipo nilipowahiwa na jamaa akafunga.
Hakuna maana nyingine hapo hilo ni kosa la kimchezo.”
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema;
“Kipa yeyote anaweza kukutana na hali kama ile, haifai kumlaumu Kaseja
moja kwa moja tunapaswa kutazama tatizo la timu na kurekebisha makosa
yetu.”
Licha ya kufungwa bao hilo lililozua mjadala kwa
mashabiki wa Yanga, Kaseja alifanya vizuri kipindi cha kwanza kwa kuokoa
hatari nyingi zilizokuwa zikielekezwa langoni kwake.
Kaseja anaichezea Yanga kwa mara ya pili baada ya
kuwahi kufanya hivyo mwaka 2008 akitokea Simba kabla ya kurejea tena
katika klabu hiyo hiyo mwaka 2011.
No comments:
Post a Comment