
Soweto: Saa chache kabla ya kuanza kwa tukio maalumu la kihistoria la Ibada ya Kitaifa ya kumuaga Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, makomandoo wa Marekani wameshika jukumu la ulinzi katika maeneo nyeti nchini hapa. Ulinzi huo unatokana na ujio wa Rais wa Marekani, Barrack Obama, mkewe Michelle pamoja na viongozi wa nchi mbalimbali, ambao watahudhuria tukio linalotarajiwa kushuhudiwa na mamilioni ya watu; ndani na nje ya Afrika Kusini.
Rais Jacob Zuma atahutubia katika ibada hiyo,
ambayo itafanyika katika Uwanja wa FNB (Soccer City), wenye uwezo wa
kuchukua watu 95,000 kwa wakati mmoja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na
Mawasiliano ya Afrika Kusini inasema milango ya uwanja huo ambao
ulitumika wakati wa sherehe za ufunguzi na fainali za Kombe la Dunia
2010, itakuwa wazi kuanzia saa 12:00 na Ibada ya kwaheri inatarajiwa
kuanza saa 5:00 asubuhi.
Karibu barabara zote za kuingia uwanjani hapo
zimetangazwa kufungwa kwa ajili ya magari yote, badala yake Serikali
imeandaa usafiri wa bure kwa wananchi watakaokwenda katika tukio hilo.
Jana, kutwa nzima, helikopta zilikuwa zikiruka
katika anga la Jiji la Johannesburg lakini zilitumia muda mwingi zaidi
kuzunguka juu ya Uwanja wa FNB ulioko Soweto, huku kukiwa na taarifa
kwamba makomandoo wa Marekani walikuwa kazini, kuhakikisha usalama wa
kiongozi wao.
Pamoja nao, mamia ya polisi wa Afrika Kusini
walionekana katika maeneo yanayozunguka uwanja huo, huku baadhi ya
vyombo vya habari vikiwanukuu maofisa wa Serikali kwamba askari 11,000
watashiriki katika ulinzi wakati wa maombolezo na mazishi.
Ulinzi pia umeimarishwa katika sehemu mbalimbali
za Jiji la Johannesburg pamoja na kule atakakozikwa katika Kijiji cha
Qunu, Mthatha ambako wanajeshi wenye silaha wamelizunguka eneo la makazi
ya kiongozi huyo.
Maeneo mengine yaliyowekewa ulinzi mkali ni katika
viwanja vya ndege na katika Majengo ya Umoja (Union Buildings) jijini
Pretoria ambako mwili wa Mandela utawekwa kwa ajili ya wananchi kutoa
heshima za mwisho kati ya keshokutwa na Ijumaa.
Vituo vya televisheni vya Afrika Kusini
vilionyesha magari ya kijeshi zaidi ya 10 yakiwa yameegeshwa katika eneo
linalozunguka makazi ya Mandela, Qunu.
Waandishi waliokuwa wamepiga kambi karibu na
makazi ya Mandela, Qunu walihamishwa na kuwekwa mbali zaidi kutokana na
sababu walizoelezwa kuwa ni za kiusalama.
No comments:
Post a Comment