
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa leo atakuwa na ziara ya siku moja katika Jimbo la Kigoma Kaskazini ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku tisa mkoani Kigoma kwa ajili ya kuimarisha chama.
Jana jioni, Dk Slaa alifanya mkutano wa hadhara
Mjini Manyovu na kusema kuwa hatishwi na waandamanaji wala vitisho vya
kuuawa na kusisitiza kuwa ataendelea na ziara yake kama kawaida hadi
Kigoma Mjini.
Awali, akihutubia katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika Kijiji cha Malumba wilayani Kasulu, juzi Dk Slaa
alisema siyo mara yake ya kwanza kutishwa na kusema analindwa na Mungu.
Licha ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi
ya wanachama wanaodai kupinga hatua ya Kamati Kuu kumvua nyadhifa zake
zote, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe alisema ataendeleza
kazi kuimarisha uhai wa chama kama ratiba ilivyopangwa.
Akiwa katika jimbo hilo linaloongozwa na Zitto, Dk
Slaa atatembelea Vijiji vya Nyarubanda na Kidahwe na kufanya mikutano
ya hadhara inayosubiriwa kwa hamu na wadau wa siasa nchini kutokana na
mzozo huo uliokikumba chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Kigoma Kaskazini,
Ally Kisala alisema maandalizi ya mikutano hiyo yamekamilika na kwamba
hakuna hofu yoyote ya kutokea vurugu katika mikutano hiyo.
“Tumedhibiti aina yoyote ya vurugu iliyokusudiwa
licha ya kuwapo baadhi ya watu wanaotamani hayo yatokee kwa lengo lao
binafsi, sambamba na kunufaisha masilahi ya makundi binafsi, lakini
hayatatokea,” alisema.
Juzi, wanachama na wafuasi wa Chadema wanaomuunga
mkono Zitto waliandamana kupinga ziara ya Dk Slaa katika jimbo lao
kupinga hatua ya kumvua mbunge wao madakara.
“Tunaamini mikutano yote ya kesho (leo Jumanne)
itafanyika vizuri na watu watapata ujumbe kutoka kwa Katibu Mkuu wetu
(Dk Slaa), na pengine wale wanaopiga kelele na kutaka kuleta mgawanyiko
ndani ya chama watapata fursa ya kuujua ukweli wa mambo ndani ya chama.
“Vita yetu si kukigawa chama, bali ni kuhakikisha tunaingia Ikulu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015,” alisema Kisala.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Zedekia
Makunja alisema jeshi lake limejipanga kuhakikisha usalama unakuwapo
katika ziara hiyo.
“Tunawajibika kuhakikisha usalama unakuwa vizuri
na kila jambo linaendelea kama lilivyopangwa. Mwito wangu kwa viongozi,
wanachama na wapenzi wa Chadema ni kuhakikisha wanamaliza tofauti zao
mapema ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza, hatupendi kuona
askari wetu wakilazimishwa kutumia nguvu kudhibiti hali ya usalama,”
alisema Makunja.
Dk Slaa anatarajia kukamilisha ziara yake mkoani Kigoma
keshokutwa kwa kuzungumza na viongozi wa mkoa kabla ya kwenda Tabora
ambako atafanya kikao cha viongozi wa Kanda ya Magharibi inayounganisha
Mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi.
Mkutano wa Bavicha Dar
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema
chama hicho hakiwezi kuwavumilia watu wanaoendeleza ghasia katika
mikutano ya Dk Slaa huko Kigoma.
Akizungumza katika Kongamano la Miaka 52 ya Uhuru
lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Dar es Salaam
jana, Lissu alisema: “Naomba niseme suala la Zitto Kabwe ambalo kama
wiki tatu hivi limekuwa likizungumzwa sana. Chadema siyo chama cha mtu
mmoja, sisi tunaangalia nidhamu, tutaendelea kuwafukuza watu wa aina
kama hiyo ambao ni wasaliti na watovu wa nidhamu kwenye chama.”
Mbali ya Lissu, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema huku akishangiliwa alisema, Chadema ina nguvu ya kushika dola mwaka
2015 hivyo lazima iwe na watu wenye nidhamu na si wapenda madaraka.
“Ni vyema ikafahamika kuwa kilio chetu siyo
madaraka ni mabadiliko. Hivyo sisi hatuwezi kuwafumbia macho watu ambao
hawakitakii mema Chadema... uongozi siku zote ni changamoto, hivyo
kufanyika kwa mabadiliko ni kitu cha lazima.”
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa
alisema: “Tukiwa tunasherehekea miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara ni
vyema vijana tukatafakari kitu gani kimefanyika kwa miaka yote hiyo.
“Miaka 52 ya Uhuru tumeshuhudia ufisadi, rushwa na
masuala mengine ya kuwakandamiza wananchi. Kitu cha msingi ni kupambana
na mambo haya. Ni wajibu wetu vijana kuamka na kuchukua hatua ya
kulitetea Taifa letu.”
Akifungua kongamano hilo, Mbunge wa Ubungo, John
Mnyika alisema tukiwa tunaadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara
chini ya uongozi wa CCM, hakuna mabadiliko yoyote na kwamba ahadi ya
maisha bora kwa kila Mtanzania haipo.
No comments:
Post a Comment