Blogger Widgets

Saturday, 9 November 2013

Nyama hatari yauzwa nchini


Afya za maelfu ya walaji wa nyama katika Jiji la Dar es Salaam zipo hatarini baada ya kubainika kuwa nyama inayochinjwa katika machinjio mengi haifai kwa matumizi ya binadamu.
Hali hiyo inatokana na mifugo kuchinjwa bila kufuata taratibu za afya na kuingizwa sokoni, ikiwamo nyama hizo kutokaguliwa na wataalamu wa mifugo kabla ya kuchinjwa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika machinjio mbalimbali ya maeneo ya Vingunguti, Ukonga, Kimara Suka, Tegeta na Mbagala, umebaini taratibu za kuchinja hazifuatwi huku maeneo hayo yakiwa yamejaa uchafu.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika machinjio hayo kwa nyakati tofauti alfajiri na kushuhudia ukiukwaji wa taratibu za uchinjaji, ambapo nyama zinatupwa ovyo, kwenye mazingira hatari, huku nyingine zikiwekwa karibu na  madimbwi ya maji machafu.
TMB: Machinjio hayafai
Alipotafutwa kuzungumzia hali hiyo, Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB),  Suzana Kiango alisema kuwa machinjio yote yaliyopo jijini Dar es Salaam hayafai.
Kiango alisema kuwa endapo kila mmoja aliye na jukumu la kusimamia sheria na kanuni za uchinjaji nyama akizitekeleza, basi machinjio yote ya jijini Dar es Salaam yanastahili kufungwa. Suzana alisema kuwa Sheria ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) namba 1 ya mwaka 2003 na Sheria ya Magonjwa ya Mifugo Namba 17 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2007 zote kwa pamoja hazisimamiwi ipasavyo.
Anataja baadhi ya sifa ambazo machinjio yanatakiwa kuwa nazo ni mabomba ya kutoa maji safi na salama, maabara ndogo, mifereji ya kutolea maji machafu, mabanda ya kutunza mifugo kabla ya kuchinjwa na chumba cha kuhifadhia nyama kabla ya mkaguzi kuifanyia uchunguzi.
“Hayo ni baadhi tu, yote hayo hayazingatiwi na TMB tunasema kwamba iwapo sheria na kanuni zitafuatwa, hakika machinjio yote ya Dar es Salaam yatafungwa,” anasema Suzana na kuongeza:
“Mifugo inapochinjwa inashauriwa iwe imepoteza fahamu kabla ya kukatwa shingo ili kuwezesha damu kutoka yote katika misuli, lakini haya hayazingatiwi na uchinjaji unafanyika chini, kila kitu kinafanyika chini, jambo ambalo ni kinyume na kanuni za uchinjaji.”
Kauli za Wataalamu
Mkaguzi wa nyama ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini alisema kuwa, asilimia kubwa ya nyama inayoliwa na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam siyo salama kiafya kutokana na uchinjaji wake kutofuata taratibu zinazokubaliwa
Takwimu zinaonyesha kuwa, katika machinjio ya Vingunguti na Ukonga, ng’ombe kati ya 250 hadi 300 huchinjwa kila siku, huku yale ya Kimara Suka, Tegeta na Mbagala yakichinja ng’ombe 100 hadi 120 kwa siku.
“Sisi tunapima ng’ombe au mbuzi kabla na baada ya kuchinjwa, lakini mazingira ya kuchinjia ndiyo tatizo, kwa kweli hayaridhishi kabisa,” alisema.
Alifafanua kuwa, endapo masharti ya kiafya ya uchinjaji wa mifugo na ubebaji wa nyama kutoka sehemu moja mpaka nyingine vingezingatiwa, nyama inayochinjwa Dar es Salaam isingekuwa na sifa ya kwenda kwa walaji.
“Wanapotaka kuchinja wanamwangusha ng’ombe au mbuzi chini kitendo ambacho kitaalamu haitakiwi, lakini hata hao wanaochinja, baadhi bado hawajapima afya zao. Yote haya ni hatari kwa usalama wa maisha yetu kwa pamoja,” alisema.
Mtaalamu wa mifugo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Aron Urassa, alisema endapo ng’ombe atachinjwa kwa kutofuata taratibu anaweza kusababisha vifo kwa watakaokula.
Anaeleza kuwa mazingira ya kuchinjia yanatakiwa kuwa safi na salama kwa kuwa yapo baadhi ya magonjwa kama kimeta, ambayo yanaweza kuangamiza maisha ya maelfu ya watu.
Akifafanua zaidi alisema ili ng’ombe aweze kufanyiwa vipimo sahihi ni lazima awepo eneo la machinjio kwa saa tano au sita kabla ya kuchinjwa na siyo  vinginevyo.
Mizoga huchinjwa
Mmoja wa wafanyakazi katika machinjio ya Kimara Suka wilayani Kinondoni aliyejitambulisha kwa jina la Dogo Mwilo, alilidokeza gazeti hili kuwa  baadhi ya ng’ombe huchinjwa na kuuzwa kinyemela wakiwa tayari wamekufa (mizoga) kutokana na kusafirishwa umbali mrefu.
“Mwanangu unakuta masela wanawachukua hao ng’ombe, wanawaichinja na kwenda kuuza nyama. Sasa sijui huwa wanakwenda kuziuzia wapi, lakini maofisa afya wanakuwa hawajui, si unajua tena ‘life’ (maisha) ngumu,” alisema Dogo Mwilo.
Kwa upande wake, mmoja wa wafanyabiashara wa ng’ombe kutoka Arusha alisema: “Huwezi kusafirisha ng’ombe zaidi ya 50 halafu wakafa watano, utawatupa wote? Hiyo ni ngumu.”
Alibainisha kuwa licha ya kuwapo wakaguzi, lakini hakuna linaloshindikana kwani njia za mkato hutumika kuhakikisha ngombe hao wanachinjwa na kuingizwa sokoni.
“Wewe ndugu yangu, kweli ng’ombe watano wote uwatupe? Hiyo itakuwa hasara kubwa. Sisi tunajua tunavyofanya hadi kuhakikisha wanachinjwa pasipo watu kujua, lakini ni makosa kutokana na imani za dini kupingana na hilo.
Hali ilivyo machinjioni
Ukifika kwenye machinjio yote ya Dar es Salaam, utapokewa na harufu mbaya na kali, huku mifereji mingi ya kupitisha maji taka ikiwa imeziba na damu kusambaa eneo kubwa la machinjio husika.
Uoshaji wa utumbo ndiyo kero zaidi, kwani wengi huoshea kwenye sakafu isiyo safi huku pia maji  yanayotumika yakiwa siyo salama. Kwa upande mwingine maini yalionekana yamewekwa sehemu chafu na mafuta ya ng’ombe kuanikwa juani kama nafaka.
Ofisa Mfawidhi wa Machinjio ya Vingunguti, Juma Nghanyanga alisema kuwa, biashara ndani ya machinjio ni jambo linalosababisha hali ya uchafu kuendelea kuwapo na udhibiti wake ni mgumu.
Alisema kuwa hairuhusiwi kuwa na soko ndani ya machinjio, kwa kuwa sehemu hiyo ni maalumu kwa kuchinjia mifugo na kuipeleka nyama sokoni kwa ajili ya kuuzwa. Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dk Severin Assenga alisema kuwa wanajipanga kuhakikisha wanakuwa na maduka 10 yenye hadhi ya kuuzia nyama nje ya machinjio hayo ya Vingunguti.
“Katika mwaka huu wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya kujenga maduka 10 yatakayokuwa na hadhi ya kuuzia nyama ili kukabiliana na hali ya usafi wa mazingira ndani ya machinjio hayo,” alisema Dk Assenga.
Wakataji, wanunuzi wanena
Benedict Julius anayejishughulisha na ukataji wa nyama katika machinjio ya Ukonga alisema: “Hali ya usafi ni mbaya na kinachohitajika ni Serikali kujenga machinjio ya kisasa ili kuepuka adha hiyo.”
Naye Sokoine John aliye katika machinjio ya Vingunguti alibainisha bei ya huduma akisema kukata bega moja la ng’ombe ni Sh1,000 na mbavu Sh1,500, lakini akasema kuwa sehemu inayotumika kuikatakata nyama hiyo ni mbaya.
Mmoja wa wanunuzi wa nyama Abdallah Hussein alisema, hali ya mazingira katika machinjio yote inatisha na Serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo kwa jicho la karibu.
Alisema kuwa Serikali inaweza kujenga hospitali nyingi na za kutosha, lakini kama vyanzo vya magonjwa haviangaliwi ni kazi bure.
Kwa upande wake, Ofisa Mifugo Mkuu wa TMB, Jeremiah Temu alisema kuwa mabadiliko makubwa yanahitajika ya uchinjaji ili kuvutia wafanyabiashara wakubwa wa nyama kununua nyama zinazochinjwa nchini.
“Utakuta Supermarket na hoteli zinaagiza nyama kutoka nje, yote haya ni kwa kuwa bado sisi tunachinja nyama chini ya viwango,” alisema Temu.
Alisema kuwa kwa Tanzania ni machinjio manne pekee yaliyo bora akiyataja ya mkoani Dodoma, Arusha  na  Sumbawanga mkoani Rukwa, akisema hayo yana hadhi ya kimataifa na kushauri ng’ombe wachinjwe huko na kuletwa Dar es Salaam.
Sifa za duka bora
Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Namba  namba 1 ya mwaka 2003 ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) inaelekeza wafanyabiashara wote kuwa na maduka yaliyojengwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria hiyo.
Baadhi ya sifa hizo ni wafanyakazi kuwa wamepimwa  afya zao na kuvaa nguo za kujikinga jozi  mbili nyeupe zilizo safi muda wote, kuwepo kwa vifaa vya kukatia nyama kama meza, kibao maalumu, mapanga, visu na misumeno ya umeme, badala ya magogo na kuwe na ndoano zisizopata kutu za kuning’iniza  nyama.
Kauli za majirani
Mkazi wa Ukonga, Bakadi Juma alisema kuwa hali ya uchafu katika machinjio hayo wameizoea kwani imekuwapo kwa kipindi kirefu.
Jirani wa machinjio ya Vingunguti,  Frank Thobias alisema hali ni mbaya kwani harufu ni kali lakini hawajui wafanye nini. Alisema kuwa Serikali inatakiwa kuliangalia suala hilo kwa umakini zaidi kwani wanaoathirika ni wananchi wake, akishauri waboreshe machinjio au kuyahamisha na kuyapeleka nje ya jiji.
Kauli ya Serikali
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David Mathayo alisema kuwa, mpango wa Serikali ni kujenga machinjio ya kisasa  Ruvu mkoani Pwani.
Kuhusu machinjio ya Vingunguti, alisema kuwa Manispaa ya Ilala ndiyo yenye jukumu la kuisimamia na siyo Serikaki Kuu.
Mkakati upo na mchakato wa kumpata mkandarasi atakayejenga machinjio hayo Ruvu unaendelea, ndani ya miaka  miwili au mitatu utakuwa umekamilika,” alisema Dk Mathayo

No comments:

- See more at: http://www.helperblogger.com/2012/06/jquery-facebook-like-box-popup-with.html#sthash.AGJhd6Gy.dpuf