
Naingia katika lango kuu la chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Watu wengi wamesimama katika makundi, baadhi yao wakiwa na sura zilizojaa simanzi.
Hawa wanasubiri kuchukua au kuaga miili ya
marehemu waliolala katika chumba hiki. Mlango wa kwanza wa chumba hiki
ni mapokezi, hapa kuna vurugu za hapa na pale kwa kuwa ndipo watu
wanapopata stakabadhi za kutunzia miili ya ndugu zao.
Wengine wamekuja kuwatafuta jamaa zao waliopotea na baadhi wamekuja kuchukua miili iliyopo.
Mlango wa pili yapo majeneza matatu ambayo tayari
yana miili ya marehemu ndani, hawa wameshasafishwa, kupambwa tayari kwa
kusafirishwa, kuagwa kisha kwenda kuzikwa.
Kushoto kuna njia ndogo inayoelekea yalipo
majokofu ya rangi ya fedha. Simanzi imetawala katika eneo hilo lenye
harufu ya mauti, kwani humu ndimo ilimolala miili ya marehemu, ambao
wanaweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki zetu.
Katika njia hii kushoto, kuna chumba, humu wapo wanaume watatu wanamsafisha maiti mwenye jinsi ya kiume.
Amelala katika sinki, mpira wa maji ukimimina maji juu yake, huku mikono ya mmoja wa wanaume, ikimsafisha kwa ustadi mkubwa.
Katika moja ya dirisha, kuna kitu mfano wa kabati
ambacho kimejaa vipodozi vya kila aina, kuanzia wanja, rangi ya mdomo,
mafuta, manukato, mkasi, viwembe na sabuni.
Mmoja kati ya watu wanaofanya kazi hii adimu ya
kusafisha miili ya marehemu ni Selemani Uliza anayesema, amesafisha
miili ya marehemu kwa miaka 30 sasa.
Anasema kwa kawaida maiti inapofika huhifadhiwa
katika jokofu hadi pale ndugu watakapofika na kutaka huduma nyingine
zaidi ya kuhifadhi.
“Ndugu huja kumtambua marehemu wao, wakitaka
kusafishiwa, basi sisi hufanya kazi hiyo kwa moyo mweupe tena na kwa ari
kuu ya kazi,” anaeleza.
Anasema kiutaratibu, Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili hawalazimishi ndugu kuwatumia wahudumu wa chumba cha maiti
kusafisha miili hiyo, bali iwapo ndugu watahitaji kupata huduma hiyo,
basi watalipia na marehemu atasafishwa
Gogo Mzome, Mkuu wa kitengo hiki cha kuhifadhi miili anasema bei
iliyowekwa na Hospitali ya Muhimbili kusafisha miili ya marehemu ni
Sh40,000 kwa maiti moja.
Wanavyofanya kazi
Uliza anasema wakati wa kusafisha miili hiyo
kwanza maiti hutolewa katika jokofu, baada ya hapo huwekwa katika sinki
maalumu ambalo lina bomba na mpira mwembamba wa kupitisha maji.
Maiti ikishawekwa vyema katika sinki, bomba la
maji hufunguliwa na kwa kutumia mpira, maiti huanza kuogeshwa na
kusuguliwa kwa sabuni na brashi laini.
“Tunamsafisha kama binadamu yeyote yule
anavyotakiwa kusafishwa, tunamsugua na kuhakikisha amekuwa safi. Wakati
mwingine tunatumia brashi zenye uwezo wa kutoa uchafu vyema,” anasema.
Baada ya hapo, anasema maiti hufutwa vyema kwa
shuka kisha taratibu nyingine huendelea iwapo ndugu watahitaji msaada
wa aina yeyote kuhusu ndugu yao.
Kwa mfano, iwapo ndugu hawawezi kumvalisha
marehemu, Uliza na wenzake humvalisha nguo ambazo zimeletwa kwa ajili ya
safari yake hiyo ya mwisho.
Vilevile, iwapo ndugu watahitaji marehemu wao
apambwe, basi Uliza huifanya kazi hiyo ambapo kwa kipindi hicho, chumba
hiki hugeuka kuwa saluni ya muda.
“Tunampamba marehemu kwa kutumia kila kifaa
ambacho ndugu watahitaji, kwa mfano poda, kama ni mwanamke lipstiki,
wanja na manukato. Kama ni mwanaume basi tunamvalisha na kumpaka
mafuta,” anasema.
Anaongeza kuwa: “Kama ndugu watahitaji marehemu
avalishwe kito cha dhahabu, huwaita waje kuthibitisha kuwa ndugu yao
amevalishwa kito hicho. Unajua siku hizi binadamu hatuaminiki.”
Baadhi ya ndugu huamua kuleta vito vya thamani
vya ndugu zao kama saa, pete, au mavazi yao waliyovaa katika harusi ili
kuwaenzi au kuwaonyesha upendo wa mwisho.
Uliza anasema mbali ya wanawake na wanaume pia
husafisha miili ya watoto wachanga. “Naona kawaida tu ninaposafisha
miili hii kwa sababu najua huyu ni ndugu yangu, na ninapomsafisha,
simchukulii kuwa ni mwanamke, bali marehemu tu wa kawaida,” anasema.
Anasema kwa kawaida maiti inapotayarishwa huanza kuvalishwa nguo
iwapo ndugu watataka na kisha sanda hufuatia mwishoni, kabla ya
kuingizwa kwenye jeneza.
Iwapo maiti inasafirishwa basi huchomwa dawa aina ya ‘Formalin’ maalum kwa ajili ya kuhifadhi mwili wa marehemu usiharibike.
Sindano hiyo huchomwa katika mshipa mkubwa wa
damu na mara nyingi paja hupasuliwa ili kuupata mshipa huo na kiasi cha
lita tano ya formalin huwekwa katika mwili huo.
“Lita tano za formalin huifanya maiti isiharibike kwa zaidi ya miezi miwili,” anasema.
Miongo mitatu ya kazi
Uliza alianza kazi hii Januari 1983, na tangu
wakati huo anasema hajawahi kuacha kufanya kazi licha ya kupata
mapumziko ya wiki moja au mbili tu.
Anasema alipoanza kazi hii alikuwa na umri wa
miaka 28 na alikuwa hajaoa, lakini hata baada ya kuoa na sasa ana watoto
wanane, ameendelea kuifanya kazi hii kwa moyo.
“Si umaskini tu unaomfanya mtu afanye kazi fulani,
lakini kama ni moyo na uzalendo. Ningeweza hata kufanya kazi ya kuuza
samaki au kupika pombe, lakini nilishawishika kuifanya hii” anasema.
Tangu mwaka 1983, Uliza amekuwa akisafisha si
chini ya miili mitatu hadi minne kwa siku, jambo ambalo huenda
likamfanya kuwa mmoja wa watu wanaosafisha miili mingi zaidi hapa
nchini.
Anasema tangu alipoanza kazi hii amekuwa akiingia
zamu tatu, yaani anaingia asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na anatoka ili
kupumzika na kurudi tena saa 2:00 usiku hadi saa 9:00 alasiri ya siku
inayofuata.
Hata hivyo, anasema kazi yake huwa nyepesi kidogo
usiku kwa sababu hakuna watu wengi wanaokuja kuchukua miili ya ndugu
zao, ukilinganisha na mchana.
“Mara nyingi usiku, maiti chache hufika hasa zile
za wodini au polisi wanaweza kuleta mwizi aliyepigwa, jambazi au mtu
aliyepata ajali” anasema.
Siku asiyoweza kusahau
Siku asiyoweza kusahau
Mzee Uliza anasema licha ya kuifanya kazi hii kwa
miaka 30 sasa na kukutana na mambo mengi , lakini siku asiyoweza kusahau
ni hivi karibuni ambapo maiti ya kijana aliyegongwa na treni huko Pugu
ilipoletwa chumba cha maiti.
“Nimeifanya kazi hii kwa miaka mingi na nina
ujasiri mkubwa tu wa kusafisha miili ya marehemu, lakini juzi niliingiwa
na simanzi na picha niliyoiona ilikuwa ya kutisha” anasema.
Anasema maiti hiyo ya kijana John Urassa
aliyegongwa na treni maeneo ya Pugu, ilikuwa imecharangwa vipande
vipande kiasi cha kushindwa kutazamika.
Kutokana na hali ya maiti hiyo ilimbidi Uliza na
wenzake waanze kuishona maiti hiyo kwa kuunganisha kipande hadi kipande
hadi ikarudi katika umbo kamili kisha wakaanza kuifanyia huduma
nyingine.
“Kuna sindano maalumu na tunatumia uzi wa kushonea
viatu ambao tulitumia katika kuunganisha kila kiungo kwa yule kijana.
Baada ya hapo tulimsafisha kuondoa damu, kisha akavalishwa sanda na
kuwekwa katika jeneza,” anasema.
Changamoto za kazi
Uliza anasema yeye pamoja na wenzake hukumbana na
wakati mgumu pale inapoletwa maiti ya mama mjamzito na kisha ndugu zake
kuomba mtoto aliye tumboni atenganishwe na mama yake.
“Inabidi tumchane tumboni, tumtoe mtoto kisha
kumshona mama yule kwa uzi na sindano. Ni kazi ambayo inatisha
kidogo…yahitaji moyo,” anasema.
Hata hivyo, Uliza anasema, iwapo ndugu watakubali
azikwe hivyohivyo basi marehemu huoshwa akiwa na mimba hiyo na kuzikwa
kama kawaida.
Changamoto nyingine wanayokutana nayo Uliza
anasema ni baadhi ya watu ambao hupenda kulalamika na kuwakosoa bila ya
kujua taratibu za kazi zao.
“Kwa mfano, kwa kawaida mwili wa marehemu
hufanyiwa uchunguzi na daktari kila siku saa 4:00 asubuhi, lakini mtu
hufika hapa saa 6:00 mchana na kulazimisha marehemu wake afanyiwe
uchunguzi wakati anaotaka yeye,” anasema.
Uliza anasema tatizo lingine la maiti kukosa ndugu hasa zile
zinaletwa na askari Polisi na kwamba zikikaa sana huwaita manispaa
kuzichukua kwa ajili ya kuzika.
Mzome anasema kisheria maiti hutakiwa kuhifadhiwa
kwa siku 14 tu kama ni mkazi wa Dar es Salaam na siku 30 kwa wanaotoka
mikoani, hivyo muda huo ukipita basi manispaa huzichukua na kwenda
kuzika.
No comments:
Post a Comment